Maelezo ya jumla

Mara nyingi kunapokuwepo na damu kwenye kinyesi huashiria kuwa kuna tatizo au jeraha kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula. Damu kwenye kinyesi inaweza kutoka mahali popote kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula, kuanzia mdomoni hadi kwenye sehemu ya kutolea haja kubwa. Damu inaweza kuwepo kwa kiasi kidogo sana kiasi kwamba huwezi kuiona kwa macho bila kipimo.
Kinyesi cheusi mara nyingi huashiria kuwa damu inavuja sehemu ya juu ya mfumo wa kumeng’enya chakula. Sehemu ya juu ya mfumo wa kumeng’enya chakula hujumuisha umio ”esophagus”, tumbo, na sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo. Damu kwa kawaida huonekana kama lami baada ya kuchanganyikana na juisi za kumeng’enya chakula wakati ikipita kwenye utumbo. Kinyesi chekundu au chenye michirizi mwekundu huashiria kuwa damu inatoka sehemu ya chini ya mfumo wa kumeng’enya chakula (utumbo mpana, rektamu, au mkundu). Hata hivyo, wakati mwingine damu nyingi inapotoka kwenye tumbo inaweza kusababisha kinyesi kuwa  chekundu.

Ni nini husababisha damu kwenye kinyesi?damu kwenye kinyesi

  • Damu ikitoka kwenye sehemu ya juu ya mfumo wa kumeng’enya chakula husababisha kinyesi kuwa cheusi, na hutokana na:
    • Kupasuka mishipa ya damu isiyo ya kawaida (mishipa ya damu yenye matatizo)
    • Kuchanika kwa umio ”esophagus, hasa baada ya kutapika sana (Mallory-Weiss tear)
    • Kutokwa damu tumboni au kwenye vidonda vya tumbo
    • Kuvimba kwa utando wa ndani ya tumbo ”gastritis”
    • Ukosefu wa mtiririko mzuri wa damu kwenye utumbo
    • Jeraha
    • Kupasuka kwa mishipa ya damu iliyopanuka (inavyoitwa varisi) kwenye umio na tumbo
  • Kutokwa na damu kwenye sehemu ya chini ya mfumo wa kumeng’enya chakula husababisha kinyesi kuwa chekundu au chenye michirizi ya damu, hii inaweza kutokana na:
    • Ufa kwenye njia ya haja kubwa
    • Mtiririko mbaya wa damu unaosababisha damu kutofika kwenye sehemu fulani ya utumbo na kusababisha sehemu hiyo kufa na kuanza kuoza
    • Uvimbe kwenye utumbo mpana / saratani ya koloni
    • Kuwepo kwa pochi zisizo za kawaida kwenye utumbo mpana – ”Diverticulosis”
    • Bawasiri/kikundu
    • Maambukizi kwenye tumbo
    • Uvimbe mdogo tumboni
    • Jeraha au kitu kigeni mwilini
    • Kula urukususu mweusi ”licorice”, dawa zenye madini ya chuma, dawa aina ya bismuth , au ”blueberries zinaweza kusababisha kinyesi kuwa cheusi. Kula nyanya kwa wingi wakati mwingine kunanaweza kufanya kinyesi kuonekana chekundu kama kuna damu kwenye kinyesi. Katika hali kama hii, daktari anaweza kukipima kinyesi ili kuona kama kuna damu.
    • Kutokwa na damu kwenye umio au tumboni (Kwa wenye vidonda vya tumbo) kunaweza kusababisha mtu kutapika damu.

Ukiwa na damu kwenye kinyesi ni wakati gani utafute matibabu ya haraka ?

  • Mwone daktari haraka kama kuna damu kwenye kinyesi au mabadiliko ya rangi ya kinyesi.
  • Kwa watoto wadogo, kiasi kidogo cha damu kwenye kinyesi ni kawaida. Hii ni inaweza kutokea kwa sababu ya kinyesi kigumu anachopata mtoto au anaweza kuwa na mzio wa maziwa. Hata hivyo, bado ni muhimu kumwambia daktari kuhusu swala hili.

Uchaguzi wa matibabu unapokuwa na damu kwenye kinyesi

  • Kama umetokwa na damu nyingi sana, unahitaji kupata matibabu ya dharura, ambayo yanaweza kujumuisha:
    • Kuongezewa damu
    • Kuongezewa maji kupitia kwenye mshipa
    • Kufanyiwa upasuaji mdogo ili kuziba mshipa unaovuja damu
    • Dawa za kupunguza asidi ya tumbo
    • Upasuaji unaweza kufanywa kama damu haitasimama kutoka.

Utambuzi unafanykaje unapokuwa na damu kwenye kinyesi

  • Daktari atachukua historia na kufanya uchunguzi wa mwili, atazingatia zaidi sehemu ya tumbo na rektumu.
  • Maswali yafuatayo yanaweza kuulizwa na daktari ili kuelewa nini chanzo cha damu kwenye kinyesi:
    • Je, unatumia dawa za kuzuia damu kuganda (dawa hizi hufanya damu kuwa nyepesi sana na kupunguza sana uwezo wa damu kuganda) mf: ”aspirin”, ”warfarin”, ”clopidogrel”, ”Aggrenox”) au NSAIDs (”ibuprofen”, ”naproxen”)?
    • Je! Umepata jeraha lolote tumboni au kwenye rektumu, au umemeza kitu chochote kigeni au chenye ncha mf. wembe?
    • Je, umekula urukususu mweusi, nyanya, dawa za kuongeza damu au ”bismuth”?
    • Je! Umeona kinyesi chenye damu mara ngapi? Ni kila mara kinyesi chako huwa hivi?
    • Umepungua uzito hivi karibuni?
    • Rangi ya kinyesi chako ni ipi?
    • Shida hii ilianza lini?
    • Je una dalili gani nyingine – maumivu ya tumbo, kutapika damu, kuvimbewa, gesi nyingi, kuhara, au homa?

Damu inapotoka kwa wingi mpaka kubadilisha rangi ya kinyesi chako daktari atataka kujua rangi halisi ya kinyesi chako ili kutambua eneo inakotoka damu hiyo. Ili kufanya utambuzi daktari anaweza kufanya endoscopy au tafiti maalum za eksirei.
Matibabu hutegemea sana sababu na wingi wa damu inayotoka. Damu inapotoka nyingi, unaweza kulazwa hospitalini ili uangaliwe kwa umakini. Kama damu inatoka kwa wingi zaidi unaweza kuweka kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Matibabu ya dharura yanaweza kujumuisha kuongezewa damu.
Vipimo vifuatavyo vinaweza kufanyika:

  • ”Angiography”- Kipimo hiki huchunguza mishipa ya damu, mionzi ya x-ray hutumika kupiga picha ya mishipa ya damu.
  • Vipimo vya damu, kama vile, ”Complete blood count” – hutumika kuchunguza maambukizi kwenye damu na clotting studies- hupima uwezo wa damu kuganda
  • ”Colonoscopy”- Kamera nyembamba huingizwa kupitia njia ya haja kubwa ili kuchunguza sehemu ya koloni inayovuja damu
  • ”Esophagogastroduodenoscopy” kwa kifupi ”EGD” –Kamera ndogo huingizwa kupitia mdomoni ili kuchunguza koromeo, umio, tumbo na utumbo (kipimo hiki hufanyika baada ya kupewa dawa ya usingizi na ganzi)
  • Vipimo vya uwepo wa maambukizo ya ”Helicobacter pylori”
  • Ekisrei ya tumbo

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/003130.htm

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *