i Maelezo ya jumla

Dawa za kujikinga na ukimwi

Dawa za kujikinga na ukimwi ni dawa ambazo hutumiwa na watu ambao hawana virusi vya ukimwi lakini wanadhani kuwa wako kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa.  PrEP, ambayo ni kifupi cha Pre-Exposure Prophylaxis ni njia mojawapo inayotumika kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kumeza kidonge kila siku.

Dawa za kujikinga na vvu (PrEP) zinafanya kazi kwa kupunguza uwezekano wa VVU kuingia ndani ya seli za mwili na kuzaliana. Hii inamaanisha kuwa ikiwa mtu atafanya ngono na mtu mwenye VVU au ataongezewa damu yenye VVU, dawa za kujikinga na ukimwi zitamkinga asipate maambukizi. Tafiti zinaonesha kuwa dawa hizi zinaweza kupunguza uwezekano wa kuambukizwa kwa zaidi ya asilimia 90 ikiwa zitatumiwa ipasavyo.

Dawa za kujikinga na ukimwi (PrEP) ni kwa ajili nani?

Dawa hizi ni kwa ajili ya watu ambao hawana maambukizi ya VVU lakini wako kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa. Hii ni pamoja na:

  • Watu ambao wanafanya ngono bila kutumia kondomu na mtu ambaye ana VVU au hajui hali yake ya VVU.
  • Watu ambao wanafanya ngono na washirika wengi au wanabadilisha washirika mara kwa mara.
  • Watu ambao wanatumia madawa ya kulevya au sindano zilizotumiwa na wengine.
  • Watu ambao wamepata magonjwa ya zinaa au mimba zisizotarajiwa katika miezi sita iliyopita.
  • Watu ambao wana washirika wa ngono ambao wako katika makundi yaliyotajwa hapo juu.

Dawa za kujikinga na ukimwi (PrEP) ni zipi?

Dawa za kujikinga na vvu (PrEP) zinatolewa kama kidonge cha rangi ya samawati kinachoitwa Truvada. Kidonge hiki kina dawa mbili za kupambana na VVU: tenofovir na emtricitabine. Mtu anayetaka kutumia dawa hizi anapaswa kupimwa VVU kabla ya kuanza kuzitumia ili kuhakikisha hana maambukizi. Pia anapaswa kupimwa figo, ini na magonjwa mengine ya zinaa.

Mtu anayetumia dawa hizi anapaswa kumeza kidonge kimoja cha Truvada kila siku. Kama utasahau kumeza dozi moja au zaidi, ufanisi wa dawa hizi utapungua na hatari ya kuambukizwa VVU itaongezeka. Mtu anayetumia dawa PrEP, pia anapaswa kuendelea kutumia njia nyingine za kinga, kama vile kondomu, ili kupunguza hatari zaidi na kujilinda dhidi ya magonjwa mengine ya zinaa.

Mtu anayetumia dawa ya kujikinga na ukimwi (PrEP) anapaswa kupimwa VVU angalau mara nne kwa mwaka ili kujua ikiwa bado hana maambukizi. Pia anapaswa kupimwa figo, ini na magonjwa mengine ya zinaa mara kwa mara ili kutambua na kutibu tatizo lolote mapema. Mtu anayetumia dawa hizi anaweza kuamua kuacha kuzitumia wakati wowote kama ataamua kupunguza tabia hatarishi.

Dawa za kujikinga na ukimwi (PrEP) zina faida gani?

Dawa hizi ni njia yenye ufanisi ya kuzuia maambukizi ya VVU. Inawapa watu uhuru, kuondoa hofu  na kuwapa nafasi ya kufurahia wanaposhiriki ngono.  Dawa hizi zinaweza kusaidia kupunguza unyanyapaa  unaowakabili watu wanaoishi na VVU au wanaohusishwa na VVU. Matumizi ya dawa za kujikinga yanaweza kuchangia katika kumaliza janga la VVU kwa kupunguza idadi ya watu wanaoambukizwa virusi.

Dawa za kujikinga na ukimwi (PrEP) zina changamoto gani?

  • Dawa hizi si njia kamili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa asilimia 100, hii ni kwa sababu njia hii inategemea mtu kujitolea kutumia kwa usahihi dawa na kufuata maelekezo ya daktari.
  • Changamoto nyingine ni kwamba, watu wanotumia dawa hizi ni watu ambao hawa ugonjwa kabisa, hivyo kupunguza msukumo wa kuzitumia kila siku kwa baadhi ya watu.
  •  Dawa hizi haziwezi kuzuia maambukizi ya VVU kama mtu ana maambukizi mengine au anatumia dawa nyingine ambazo zinaweza kupunguza ufanisi wa dawa hizi.
  • Mwisho, dawa hizi haziwezi kukulinda dhidi ya magonjwa mengine ya zinaa au mimba zisizotarajiwa.

Unapata wapi dawa za kujikinga na ukimwi ?

Dawa za kujikinga na vvu (PrEP) zinapatikana katika baadhi ya vituo vya afya nchini Tanzania. Mtu anayetaka kutumia dawa hizi anapaswa kuwasiliana na kituo cha afya kilicho karibu naye ili kupata ushauri na huduma.

Matumizi ya PrEP ni uamuzi wa mtu binafsi. Ni muhimu kujua faida na changamoto za dawa za hizi kabla ya kuanza matibabu. Ni muhimu pia kuzingatia njia nyingine za kuzuia maambukizi ya VVU, kama vile kutumia kondomu, kupunguza washirika wa ngono, kupima VVU mara kwa mara na kutibu magonjwa ya zinaa. Kuzuia ni bora kuliko tiba.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/hiv.html

Shares:
1 Comment
  • ⚖ Notification- TRANSFER 0.75901539 BTC. Continue => https://telegra.ph/Get-BTC-right-now-01-22?hs=eaeefc17339ddb893bfa09ae477ec38e& ⚖
    ⚖ Notification- TRANSFER 0.75901539 BTC. Continue => https://telegra.ph/Get-BTC-right-now-01-22?hs=eaeefc17339ddb893bfa09ae477ec38e& ⚖
    February 5, 2025 at 4:14 am

    i641a5

    Reply
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *