Chakula na lishe

Chakula ni muhimu kwa binadamu wote kwani huupatia mwili virutubishi mbalimbali kwa ajili ya kazi mbalimbali mwilini na hivyo kuwezesha kuwa na afya bora. Karibu vyakula vyote huwa na virutubishi zaidi ya kimoja ila hutofautiana kwa kiasi na ubora.

Kila kirutubishi kina kazi yake muhimu mwilini na mara nyingi virutubishi hutegemeana ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi. Kuna makundi matano makuu ya vyakula ambayo yanamuwezesha mtu kupanga mlo kamili kwa kuchagua angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi.

Vyakula ambavyo vina virutubishi vingi vinavyofanana huwekwa kwenye kundi moja. Mlo kamili huwa na virutubishi vyote muhimu kwa ajili ya lishe na afya bora.

Nchini Tanzania kuna matatizo mengi ya utapiamlo ambayo yanatokana na kuzidi au kupungua kwa virutubishi. Tatizo la kuzidi kwa virutubishi ambalo linakua katika baadhi ya jamii linahusishwa kwa karibu na magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza.Chakula

Utapiamlo uwe wa kupungua au kuzidi kwa virutubishi huleta athari kwa jamii ikiwa ni pamoja na zile za kibinafsi, kijamii na kiuchumi. Tathmini ya hali ya lishe ya mtu ni muhimu ili kuwezesha kugundulika mapema dalili zozote za matatizo ya kiafya au ulaji usiofaa unaoweza kuongeza uwezekano wa mtu kupata maradhi hususan yale sugu yasiyo ya kuambukiza.

Maendeleo ya kiuchumi yamechangia sana kuwafanya watu kuwa na mtindo wa maisha ambao siyo bora. Mtindo huu wa maisha umechangia kwa watu kulimbikiza nishati-lishe mwilini na hivyo kujiweka katika uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza

Faida za chakula kwa binadamu: ­

  • Kutengeneza seli za mwili na kurudishia seli zilizokufa au kuharibika; ­
  • Kusaidia ukuaji wa akili na mwili; ­
  • Kuupa mwili nguvu, joto na uwezo wa kufanya kazi; na ­
  • Kuupa mwili kinga dhidi ya maradhi mbalimbali.

Faida za kuwa na hali nzuri ya lishe

Ni muhimu kuzingatia ulaji unaofaa ili kuwa na hali nzuri ya lishe. Ulaji bora usipozingatiwa virutubishi huzidi au kupungua mwilini na hivyo kusababisha utapiamlo. Hali nzuri ya lishe huuwezesha mwili: ­

  • Kukua kikamilifu kimwili na kiakili; ­
  • Kuwa na nguvu na uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi; ­
  • Kuwa na uwezo wa kujilinda na kukabiliana na maradhi na hivyo kuwa na afya nzuri; na ­
  • Kuzuia magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza na pia maradhi mengine.

Vyanzo

https://diabetesatlas.org/upload/resources/previous/files/3/Diabetes-Atlas-3rd-edition.pdf

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *