Maelezo ya jumla

Kibole (appendicitis) ni uvimbe wa kidole tumbo (appendix) unaosababishwa na maambukizi. Kidole tumbo ni kiungo kidogo kinachoonekana kama kidole kilichopachikwa kwenye sehemu ya mwanzo ya utumbo mpana. Kidole tumbo kiko tumboni upande wa chini-kulia. Kazi yake haijulikani. Kuziba kwa kidole tumbo husababisha Kibole. Kuziba husababisha kuongezeka kwa shinikizo ndani ya kidole tumbo na kusababisha matatizo ya mtiririko wa damu hutokea na kuvimba. Kama uzibe usiposhughulikiwa mapema kidole tumbo kinaweza kupasuka na kusambaza maambukizi mwili mzima. Tatizo hil ni dharura ya kimatibabu. Matibabu karibu kila mara huhusisha upasuaji wa kuondoa kidole tumbo. Mtu yeyote anaweza kupata Kibole. Kibole huwapata zaidi watu kati ya umri wa miaka 10 na 30.

kibole

Je! Nini dalili za Kibole?

Watu wengi wenye shida hii huwa na dalili mahususi zinazoweza kutambuliwa na daktari kwa urahisi. Dalili kuu ya kibole ni maumivu ya tumbo.
Maumivu ya tumbo:

  • Hutokea ghafla, mara nyingi husababisha mtu kuamka usiku
  • Hutokea kabla ya dalili nyingine
  • Huanzia karibu na kitovu na kisha huelekea chini-kulia mwa tumbo
  • Ni mapya na tofauti na maumivu yoyote uliyowahi kuhisi kabla
  • Huzidi kuwa makali zaidi kadri muda unavyopita na ndani ya masaa machache tu
  • Huwa makali zaidi mgonjwa anapojongea, anapovuta pumzi ndani, anapokohoa au anapopiga chafya.

Dalili nyingine za Kibole zinaweza kujumuisha:

Dalili hutofautiana kwa kila mtu na zinaweza kusababishwa na vyanzo vingine vya maumivu ya tumbo, ikiwa ni pamoja na:

  • Kuziba kwa utumbo
  • Ugonjwa unaosababisha kuvimba kwa matumbo (inflammatory bowel disease)
  • Magonjwa ya nyonga na matatizo ya kijinakolojia
  • Kufunga choo
  • n.k

Ni nini husababisha kibole?

Kuziba kwa uwazi wa kidole tumbo husababisha kibole. Uteute hujaa ndani ya uwazi wa kidole tumbo na kusababisha bakteria wanaoishi hapo kuongezeka sana. Matokeo yake, kidole tumbo huvimba. Kuziba kwa uwazi wa kidole tumbo husababishwa na:

  • Kinyesi, vimelea, au uvimbe unaoziba uwazi wa kidole tumbo
  • Kuongezeka kwa ukubwa wa tezi za limfu kunakosababishwa na maambukizi kwenye mfumo wa kumeng’enya chakula au mahala pengine mwilini
  • Ugonjwa unaosababisha kuvimba kwa matumbo, hii ni pamoja na ugonjwa wa Crohn na ugonjwa wa ulcerative colitis
  • Jeraha tumboni

Kibole kinaweza kupasuka na kusambaza maambukizi kwenye tumbo lote kama hakitaondolewa.

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Mtu yeyote anaweza kupata appendicitis, lakini ni kawaida zaidi kati ya watu wa miaka 10 hadi 30. Appendicitis inaongoza kwa upasuaji wa tumbo zaidi ya dharura kuliko sababu nyingine yoyote.

Utambuzi

Daktari au mtoa huduma mwingine wa afya anaweza kutambua kesi nyingi za kibole kwa historia ya mgonjwa na uchunguzi wa mwili.  Kama mtu ataonesha dalili mahususi za kibole, daktari atashauri ufanyiwe upasuaji mara moja kuondoa kidole tumbo kabla hakijapasuka. Madaktari wanaweza kutumia vipimo vya maabara na vipimo vya picha ili kuhakiki kibole kwa mtu mwenye dalili mahususi za kibole. Vipimo pia vinaweza kusaidia kugundua kibole kwa watu wasioweza kuelezea vyema dalili zao, kama watoto au watu wenye ugonjwa wa akili.
Historia ya kitabibu
Daktari atauliza maswali maalum juu ya dalili unazopata na historia ya kiafya. Majibu ya maswali haya yatamsaidia daktari kufanya utambuzi. Daktari atataka kujua ni wakati gani maumivu yalianza na mahali halisi yalipo na ukali wa maumivu hayo. Kujua ni wakati gani dalili nyingine zilijitokeza sambamba na maumivu husaidia pia. Daktari atauliza maswali kuhusu hali nyingine za kitibabu, magonjwa uliyowahi kuugua na kama umewahi kufanyiwa upasuaji, matumizi ya dawa, pombe, au madawa ya kulevya.
Uchunguzi wa mwili
Maelezo juu ya maumivu ya tumbo ni muhimu sana ili kutambua kibole. Daktari atapima maumivu kwa kugusa tumbo. Daktari anaweza pia kuchunguza rektamu, ambayo inaweza kuwa na maumivu kutokana na kibole.
Vipimo vya Maabara
Vipimo vya damu hutumiwa kuchunguza dalili za maambukizi. Vipimo vya damu vinaweza pia kuonyesha usawa wa majimaji na chumvichumvi mwilini. Kipimo cha mkojo (urinalysis) hupima kama kuna maambukizi kwenye njia ya mkojo. Madaktari wanaweza pia kuagiza kupimwa mimba kwa wanawake.
Vipimo vya picha                                               

  • Computerized tomography (CT) scans, huunda picha za mwili, na husaidia kugundua kibole
  • Ultrasound wakati mwingine hutumiwa kugundua ishara za kibole.
  • X ray ya tumbo haisaidii sana katika uchunguzi wa kibole, lakini inaweza kutumika kutafuta vyanzo vingine vya maumivu ya tumbo. Wanawake walio kwenye umri wa kuzaa wanapaswa kupimwa mimba kabla ya kupigwa x-ray au CT scan. Vipimo hivi hutumia mionzi na vinaweza kuleta shida kwa mtoto. Ultrasound haitumii mionzi na sio hatari kwa mtoto.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Kibole ni dharura ambayo inahitaji huduma ya haraka. Watu wanaofikiria wana kibole wanapaswa kumwona daktari mara moja. Uchunguzi na tiba ya haraka hupunguza uwezekano wa kupasuka kwa kibole.

kidole tumboUchaguzi wa matibabu

Upasuaji
Mara nyingi kibole hutibiwa kwa upasuaji. Kama daktari atahisi una kibole, anaweza kupendekeza ufanyiwe upasuaji bila kufanya uchunguzi wa kina. Upasuaji wa haraka hupunguza uwezekano wa kibole kupasuka.
Upasuaji wa kuondoa kidole tumbo huitwa appendectomy na unaweza kufanyika kwa njia mbili.

  • Njia ya zamani, inayoitwa laparotomy – hii huondoa kidole tumbo baada ya kufanya upasuaji mdogo kwenye sehemu ya chini-kulia mwa tumbo (hii ndiyo njia inayotumika zaidi katika hospital a Afrika).
  • Njia mpya, inayoitwa laparoscopic surgery – Daktari hutoboa matundu madogo sana tumboni na kutumia vifaa maalumu kuondoa kidole tumbo kupitia mashimo hayo bila kupasua tumbo. Aina hii ya upasuaji hupunguza sana madhara yanayotokana na upasuaji na hupunguza muda wa kulazwa hospitalini pia.

Upasuji mara kadhaa unaweza kukuta kidole tumbo hakina tatizo. Katika hali kama hiyo daktari huondoa kabisa kidole tumbo ili kisiweze kusababisha kibole hapo baadae. Wakati mwingine daktari anaweza kukuta matatizo mengine tumboni wakati wa upasuaji na kuyasahihisha
Matibabu mengine
Matibabu mengine yanaweza kutumika kama upasuaji hauwezi kufanyika au kama mgonjwa hawezi kuhimili upasuaji kwa sababu ya afya yake duni. Tafiti kadhaa zimeonesha kuwa baadhi ya kesi za kibole zinaweza kupona bila upasuaji. Tiba hii ni pamoja na antibiotics kutibu maambukizi na mlo laini hadi maambukizi yatakapoondoka.

Kuzuia Kibole

Hakuna njia inayojulikana inaweza kuzuia kibole.

Nini cha kutarajia ukiwa na kibole?

Wagonjwa wengi wa kibole hupata nafuu mapema baada ya matibabu. lakini matatizo yanaweza kutokea kama matibabu yatacheleweshwa.
Muda wa kupona hutegemea umri, hali ya mgonjwa, matatizo yaliyojitokeza baada ya upasuaji, na hali nyingine, kama vile kiasi cha matumizi ya pombe n.k. lakini kwa kawaida muda wa kupona ni kati ya siku 10 hadi 28. Kwa watoto wadogo (umri wa miaka 10 hivi) hupona baada ya wiki tatu.
Kuna uwezekano wa kutokea kwa uvimbe wa ngozi ya fumbatio (peritonitis) na unaweza kutishia maisha, na hii ndiyo sababu uchunguzi na matibabu ya kibole hufanyika haraka na mapema.
Ugonjwa wa kidole tumbo kwa kawaida hupona vyema baada ya upasuaji wa kuondoa kidole tumbo na wakati mwingine unaweza kupona bila tiba yoyote. Ugonjwa huu unapopona wenyewe kunabakia na utata kama mgonjwa anahitaji kufanyiwa upasuaji ili kuzuia kutokea kwa tatizo hili tena hapo baadae au la. Ni ngumu kutambua kibole chenye dalili zisizo za kawaida na mara nyingi matatizo hujitokeza hata baada ya matibabu kufanyika mapema. Uchunguzi na upasuaji ukifanyika mapema katika hali yoyote ya ugonjwa, huleta matokeo bora zaidi. Japo si kawaida, vifo na matatizo mabaya hutokea, hasa baada ya kutokea kwa uvimbe wa ngozi ya fumbatio (peritonitis).

Matatizo yanayoweza kutokea ukiwa na kibole

  • fistula
  • Jipu
  • Maambukizi kwenye kidonda cha upasuaji.
  • Uvimbe wa ngozi ya fumbatio (peritonitis)

Vyanzo

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *