Maelezo ya jumla

Kisonono (Gonorrhea) ni ugonjwa wa zinaa.

Je, Nini dalili za kisonono?

Dalili za kisonono huanza kuonekana siku 2 – 5 baada ya kuambukizwa. Hata hivyo, kwa wanaume, dalili zinaweza kuchelewa mpaka mwezi. Watu wengine hawapati dalili kabisa. Wanaweza kuwa hawajui kabisa kwamba wameambukizwa ugonjwa huu, na kwa sababu hiyo hawatafuti matibabu. Hii huongeza uwezekano wa kupata matatizo na hatari ya kuambukiza wengine.
Dalili kwa wanaume ni pamoja na:

  • Maumivu wakati wa kukojoa
  • Kukojoa mara kwa mara au kushindwa kuzuia mkojo (mgonjwa akibanwa mkojo, ni lazima akakojoe haraka sana)
  • Kutoa uchafu kwenye uume (uchafu unaweza kuwa mweupe, njano, au rangi ya kijani)
  • Wekundu au kuvimba kwa urethra (huu ni mrija unaobeba mkojo kutoka kwenye kibofu kwenda nje)
  • Kuvimba na kuuma kwa korodani
  • Maumivu kwenye koo

Dalili kwa wanawake zinaweza kuwa ndogo sana na zisizo maalam, na huenda zikachanganywa na dalili za maambukizi mengine.
Dalili kwa wanawake ni pamoja na:

  • Kutoa uchafu ukeni
  • Maumivu wakati wa kukojoa
  • Kukojoa mara kwa mara/mara nyingi
  • Maumivu kwenye koo
  • Maumivu wakati wa ngono
  • Maumivu makali kwenye sehemu ya chini ya tumbo (kama maambukizi yataenea mpaka kwenye mirija ya uzazi)
  • Homa (Kama maambukizi yataenea mpaka kwenye mirija ya uzazi au eneo zima la tumbo)

Kama maambukizi yataenea kwenye damu, homa, kuwashwa, na dalili kama za yabisi kavu zinaweza kutokea.

Kisonono husababishwa na nini?

kisonono
Neisseria gonorrhoeae

Kisonono husababishwa na bakteria anayeitwa  Neisseria gonorrhoeae. Mtu yeyote anayefanya ngono ya aina yoyote anaweza kuambukizwa kisonono. Maambukizi yanaweza kuenezwa kwa mdomo, uke, uume au mk*ndu. Bakteria  huyu hukua kwenye maeneo ya joto na yenye unyevu, hii ni pamoja na mrija unaotoa mkojo mwilini (urethra). Kwa wanawake, bakteria hupatikana kwenye via vya uzazi ( hii hujumuisha mirija ya uzazi, mji wa mimba, na mlango wa mji wa mimba). Bakteria hawa wanaweza kukua hata machoni.

Nani yuko kwenye hatari zaidi kupata kisonono?

Kuna uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya kisonono kama:

  • Una washirika wengi wa ngono
  • Una mpenzi mwenye historia ya kupata magonjwa ya zinaa
  • Hautumii kondomu wakati wa ngono
  • Wewe ni mwanaume unayefanya ngono na mwanaume mwingine
  • Unatumia madawa ya kulevya

Utambuzi wa ugonjwa wa kisonono

  • Kisonono hutambuliwa baada ya sampuli ya tishu au uchafu unaotoka ukeni/ kwenye uume kutiwa rangi (gram stain) na kisha kuchunguzwa chini ya darubini. Japo njia hii ya utambuzi ni ya haraka, si ya kuaminika sana. Sampuli kwa ajili ya gram stain huchukuliwa:
    • Kwenye mlango wa kizazi cha mwanamke
    • Uchafu unaotoka kwenye uume wa mwanaume
    • Majimaji kutoka kwenye maungio ya mwili-joints
  • Culture (sampuli huchukuliwa na kupandwa kwenye sahani maalumu ya maabara, njia hii huwaruhusu bakteria kukua – utambuzi hufanyika kwa urahisi wakikua ), njia hii ni ya kuaminika zaidi. Sampuli kwa ajili ya culture huchukuliwa:
    • Kwenye kizazi na mlango wa kizazi cha mwanamke
    • Uchafu unaotoka kwenye uume wa mwanaume
    • Kooni kwa wanaume na wanawake
    • Mk*nduni kwa wanaume na wanawake
    • Majimaji kutoka kwenye maungio ya mwili- joints
    • Damu

Matokeo ya awali ya culture hutoka baada ya masaa 24 na matokeo thabiti ndani ya masaa 72.

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Kama una dalili za kisonono unapaswa kumwona daktari mapema iwezekanavyo.

Uchaguzi wa matibabu ya kisonono

Kuna malengo mawili katika kutibu magonjwa ya zinaa, hasa ambayo yanaenea kwa urahisi kama kisonono. La kwanza ni kutibu maambukizi ya mgonjwa. La pili ni kuwatafuta na kuwapima watu wengine wote ambao wamefanya ngono na mgonjwa, ili kuwatibu na kuzuia maambukizi zaidi. Usijitibu mwenyewe bila kuonwa na daktari kwanza. Mtoa huduma wa afya ataamua ni matibabu gani yaliyo bora zaidi. Matibabu yanayopendekezwa ni pamoja na:

  • Sindano moja ya ceftriaxone 125 mg au kumeza dozi moja ya cefixime 400mg.
  • Dozi moja ya Azithromycin 2g inaweza kutumika kwa watu wenye mzio kwa ceftriaxone, cefixime, au penicillin.

Mgonjwa anapaswa kurejea hospitalini baada ya siku 7. Vipimo vitafanywa tena, kuhakikisha maambukizi yamekwisha. Watu wote waliofanya ngono na mgonjwa wanapaswa kutafutwa ili wapimwe na kutibiwa. Hii hupunguza kuenea kwa kisonono.

Nini cha kutarajia ukiwa na kisonono?

Kwa karibu mara zote, maambukizi ya kisonono ambayo hayajaenea kwenye damu au maeneo mengine hupona vyema baada ya kutumia antibiotiki. Kisonono ambayo imeenea ni tatizo kubwa, lakini pia hupona baada ya matibabu.

Matatizo yanayoweza kutokea ukiwa na kisonono

Matatizo yanayoweza kutokea kwa wanawake ni pamoja:

  • Kuharibika kwa mirija ya uzazi (salpingitis ) – hii inaweza kusababisha ashindwe kupata mimba au kusababisha mimba itungwe nje ya mji wa mimba (ectopic pregnancy).
  • Ugumba (kukosa uwezo wa kuwa mjamzito)
  • Maumivu wakati wa ngono
  • Wanawake wajawazito wenye kisonono wanaweza kuwaambukiza watoto wao wakiwa tumboni au wakati wa kuzaliwa

Matatizo kwa wanaume ni pamoja na:

  • Mgonjwa anaweza kupata makovu yanayoweza kusababisha kuziba kwa njia ya mkojo (urethra)- hii inaweza kusababisha shida wakati wa kukojoa
  • Jipu (usaha kwenye urethra)
  • Matatizo wakati wa kukojoa
  • Maambukizi kwenye njia ya mkojo
  • Kushindwa kwa figo kufanya kazi

Matatizo yanayoweza kuwapata wanaume na wanawake ni pamoja na:

  • Kusambaa kwa maambukizi mwili mzima- hii inaweza kuwa hatari sana
  • Kama mgonjwa hatatibiwa mapema, anaweza kuwa na maumivu ya muda mrefu ya maungio (joints).
  • Maambukizo ya vali za moyo
  • Kuvimba kwa tando za uti wa mgongo au ubongo

MAELEZO ZAIDI KUHUSU UGONJWA WA KISONONO

Maelezo ya jumla

Ni ugonjwa unaosababisha kutokwa usaha kwenye via vya uzazi

Sababu

Neisseria gonorrhea

Epidemiolojia

Unapatikana dunia nzima, unaathiri jinsi zote mbili, hasa vijna na watu wazima wanaojihusisha na ngono kwa wingo. Inawapata zaidi watu wenye uchumi duni. Katika nchi nyingi zilizoendelea kiwango cha maambukizi kimepungua katika miongo hii miwili iliyopita

Uambukizo

Kwa kushiriki ngono na mtu aliyeambukizwa

Muda kabla dalili kuanza

Siku 2-7

Muda wa uambukizo

Mtu anaweza kuendelea kuambukiza wengine kwa miezi mingi kama asipotibiwa. Matibabu ya uhakika yananamaliza uwezo wa kuambukiza baada ya masaa tu.

Nani yuko kwenye hatari

Mtu yeyote anaweza kuambukizwa. Hakuna mtu anayepata kinga na mtu anaweza kuambukizwa mara nyingi sana kisonono

Dalili

  1. Wanaume
    • Unahusisha njia ya kutoa mkojo (urethra)
    • Kutoa uchafu kama usaha kwenye uume, maumivu wakati wa kukojoa na kukojoa mara kwa amra
  1. Wanawake
    • Wanawake wengi hawapati dalili.
    • Wanaweza kutokwa na majimaji ukeni.
    • Sehemu inayoathiriwa na kisonono mara nyingi ni mlango wa kizazi, mkundu na koo.
    • Tezi iliyoko ukeni inayoitwa Bartholin inaweza kuvimba.
    • Kuvimba kwa mirija ya uzazi kunatokea kwa 20% wanawake
    • Watoto waliozaliwa na kina mama walioambukizwa hutoa usaha kwenye macho, kuwa mekundu na kuvimba kwa siku 2-3

Utambuzi

  • Kuangalia kwa darubini sampuli kutoka ukeni, mrija wa kojo, mlango wa kizazi, kope za macho – gram stain
  • Culture

Matibabu

  1. Co – trimoxazole AU
  2. Erythromycin AU
  3. Ceftriaxone

Kuzuia

  1. Toa matibabu kwa wagonjwa
  2. Tibu wapenzi wa wagonjwa pia
  3. Toa elimu kuhusu ngono salama
  4. Dhibiti magonjwa ya ngono kwa wanaouza milii (Malaya)
    • Vipimo vya kila mwezi na kutoa matibabu
    • Kuwagawia kondomu
  1. Kuchunguza wanawake wajawazito na kutoa matibabu mapema ili kuzuia kuambukiza mtoto
  2. Kupaka dawa aina 1% tetracycline kwenye macho ya mtoto baada tu ya kuzaliwa

Vyanzo

http://wikidoc.org/index.php/Gonorrhea

Shares:
11 Comments
  • asante sana kwa makala hii dokta
    asante sana kwa makala hii dokta
    September 2, 2021 at 9:34 pm

    asante kwa makala hii watalaamu

    Reply
    • Dr.Mniko
      Dr.Mniko
      December 24, 2021 at 10:25 am

      Karibu

      Reply
      • Pierre
        Pierre
        June 4, 2022 at 12:59 pm

        Je kisonono kinaweza kusabababisha mchubuko mwekundu juu ya kichwa cha uume

        Reply
        • Dr Mniko
          Dr Mniko
          June 6, 2022 at 8:18 pm

          hAPANA, Kisonono haisababishi vidonda, kisonono inasababishwa kutoka na uchafu ukeni au kwenye uume , uchafu unakuwa mzito, wa njano kama usaha

          Reply
    • Dr.Mniko
      Dr.Mniko
      December 24, 2021 at 10:31 am

      Karibu sana

      Reply
  • Jasmin
    Jasmin
    January 3, 2022 at 9:59 pm

    Kisonono linaweza sababisha mowasho ukeni?

    Reply
    • Dr Mniko
      Dr Mniko
      January 30, 2022 at 9:22 pm

      Ndio unaweza kuwashwa ukeni, mwasho kama unaungua hasa unapokojoa. inaweza kuambatana na kutokwa uchafu mzito kama usaha . Mwone dakatari akuandikie dawa

      Reply
  • Jasmin
    Jasmin
    January 3, 2022 at 10:01 pm

    Kisonono kinaweza sababisha miwasho ukeni?

    Reply
    • Dr Mniko
      Dr Mniko
      January 30, 2022 at 9:22 pm

      Ndio unaweza kuwashwa ukeni, mwasho kama unaungua hasa unapokojoa. inaweza kuambatana na kutokwa uchafu mzito kama usaha . Mwone dakatari akuandikie dawa

      Reply
  • Eva
    Eva
    June 17, 2022 at 1:25 am

    Je Kwa mwanamkee Kuwa na dalili moja kati ya hayo ni dalili za kisonono? mfano kutokwaa na uchafu ukeni.

    Reply
  • Ballo
    Ballo
    August 11, 2022 at 10:33 pm

    Dr kitu gani kinachofanya uume kua na vidonda vinavyowasha sana unajikuna hadi kuchubuka sana

    Reply
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *