Maelezo ya jumla
Kitambi (obesity) humaanisha kuwa una mafuta mengi mwilini. Kuwa na kitambi si sawa na kuwa na uzito mkubwa (overweight), kuwa na uzito mkubwa humaanisha mtu ana uzito mkubwa sana kuliko ilivyokawaida. Mtu anaweza kuwa na uzito mkubwa kutokana na ziada ya misuli, mifupa au maji mwilini, mafuta pia yanaweza kuongeza uzito wa mwili.
Maneno yote haya humaanisha kuwa mtu ana uzito mkubwa kuliko kiwango kinachodhaniwa ni bora kiafya kulingana na urefu wake.
Bonyeza hapa kujua njia za kupima kujua kama una kitambi
Ni nini husababisha kitambi?
Kula kalori nyingi kuliko mahitaji ya mwili wako hupelekea kutapata kitambi. Hii ni kwa sababu kalori zisizotumika huhifadhiwa mwilini mwako kama mafuta.
Kitambi kinaweza kusababishwa na:
- Kula chakula kingi kuliko mahitaji ya mwili wako
- Kunywa pombe sana
- Kutofanya mazoezi ya kutosha
Watu wengi wanaojaribu kupunguza uzito, hupunguza kiasi fulani cha uzito na baadae uzito huanza kuongezeka tena, hili huwafanya wajihisi wenye hatia. Watu hawa hujilaumu sana kwa kushindwa kudhibiti kuongezeka kwa uzito. Watu wengine huongezeka uzito maradufu kuliko waliopunguza hapo awali.
Sababu nyingine zinazoathiri uzito ni pamoja na zifuatazo:
- Jinsi tunavyokula/tulivyokula wakati tukiwa watoto wadogo huathiri kwa kiasi kikubwa jinsi tunavyokula tukiwa watu wazima. Jinsi tunavyokula kwa miaka mingi hugeuka na kuwa tabia. Jinsi tunavyokula, muda tunaokula, kiasi tunachokula na hata chakula tunachokula ni tabia inayojengeka kwa miaka mingi.
- Kama tumezungukwa na vitu vinavyofanya iwe rahisi kula sana au kupunguza uwezekano wa kufanya mazoezi:
- Watu wengi hawana muda wa kutengeneza au kupika chakula bora.
- Watu wengi siku hizi hufanya kazi maofisini ikilinganishwa na kazi za kujishughulisha kimwili zilizofanyika hao zamani.
- Watu wenye kazi nyingi sana huwa na muda mchache sana wa kufanya mazoezi.
Neno “Matatizo ya ulaji”, humaanisha aina ya matatizo ya kiafya yanayosababishwa na ulaji mbaya. Watu wengine hujinyima sana chakula kupita kiasi na hii husababisha kupungua sana uzito mpaka kufikia viwango vya hatari, wengine hula sana au mara kwa mara na kusababisha kuongezeka sana uzito.
Wakati mwingine, matatizo ya kitabibu au tiba ya matatizo hayo husababisha kuongezeka kwa uzito, mfano:
- Kushindwa kwa tezi dundumio kufanya kazi yake vyema (hypothyroidism)
- Madawa kama vile dawa za kupanga uzazi, dawa za kudhibiti msongo wa mawazo, na dawa za kudhibiti wendawazimu.
Mambo mengine yanayoweza kusababisha kuongezeka kwa uzito ni:
- Kuacha kuvuta sigara. Watu wengi wanaoacha kuvuta sigara huongezeka uzito, kilo 2 – 5 katika miezi 6 ya mwanzo baada ya kuacha kuvuta. Watu wengine huongezeka kilo 12 – 15.
- Msongo, wasiwasi, huzuni, au kutopata usingizi vizuri
- Kwa wanawake:
- Wakati wa kukatika damu ya hedhi (menopause) – wanawake wanaweza kuongezeka kilo 6 – 7.5 baada ya damu ya hedhi kukatika.
- Kushindwa kupunguz uzito ulioongezeka wakati wa ujauzito
Utambuzi wa kitambi
Uchunguzi wa kitambi unapaswa kufanyika angalau mara moja kwa mwaka kwa watu wazima. Kuna njia mbili zinazotumika zaidi kupima kama una kitambi nazo ni:
- Body mass index (BMI)
- Mzunguko wa kiuno (waist circumference)
BMI inapimwa kwa kutumia urefu na uzito. Mtoa huduma ya afya anaweza kutumia BMI kukadiria kiwango cha mafuta mwilini. Upimaji wa mzunguko wa kiuno ni njia nyingine bora ya kukadiria mafuta mwilini. Kuongezeka kwa uzito wa ziada karibu maeneo ya kati au tumbo huongeza hatari ya kupata kisukari aina ya pili, magonjwa ya moyo na kiharusi. Watu wenye kiuno kipana kuliko nyonga (hips) zao, wako kwenye hatari kubwa ya kupata kitambi. Vipimo vya damu vinaweza kufanyika ili kuangalia kama kuna tatizo la tezi dundumio au homoni ambalo husababisha kuongezeka uzito.
Body mass index (BMI)
Body mass index ni hesabu za kihisabati ambazo hufanyika ili kutathmini hatari za kiafya zinazohusiana na uzito wa mwili. Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa uzito wa mwili chini au juu ya kiwango fulani huongeza hatari ya kupata matatizo ya kiafya kama magonjwa ya moyo, kisukari na hata kansa.
Body mass Index hutoa uwakilishi wa kiasi cha mafuta yaliyomo mwilini, kadri kiasi cha mafuta kinapoongezeka mwilini, ndivyo na hatari za kiafya zinavyoongezeka. Wataalamu wa afya wanajua kuwa, kuongezeka uzito wa mwili unaosababishwa na mafuta mengi mwilini, ndio sababu kuu ya magonjwa ya moyo.
Wanaume na wanawake wenye urefu na uzito sawa wana BMI sawa.
BMI =
- BMI inayokubalika kiafya na jumuiya ya kitabibu ni kati ya 18.5 hadi 24.9. Kiwango hiki kinawakilisha uwiano kati ya uzito na urefu ambao haukuweki katika hatari ya kupata madhara kiafya.
- BMI chini ya 18.5 inaonyesha kuwa uko katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya kiafya yanayosababishwa na uzito mdogo sana (underweight).
- BMI kuanzia 25 hadi 29.9 inaashiria kuwa uzito wako ni mkubwa kwa 10-15% zaidi ya kiwango kinachokubalika, na kwa sababu hiyo uwezekano wa kupata shinikizo la juu la damu huongezeka mara mbili zaidi.
- BMI zaidi ya 30 huonyesha uzito wa mwili ambao ni 20% zaidi ya uzito wa kawaida. Uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo, huongezeka mara 2 – 6 kwa mtu mwenye kiwango hiki cha BMI.
- BMI zaidi ya 35 , Mtu mwenye kiwango hiki cha BMI mara nyingi atakuwa na matatizo ya kiafya yanayohusiana na uzito tayari. Matatizo hayo ni pamoja na Shinikizo la juu la damu, magonjwa ya mishipa ya moyo na kushindwa kwa moyo.
1.BMI [Kg/m2 ] | MATOKEO | USHAURI |
18.5 mpaka 24.9 | Uzito wako ni wa kawaida | Una hali njema, endelea kujitunza ili usiongezeke uzito |
25 mpaka 29.9 | Uzito wako ni mkubwa | Haupaswi kuongezeka uzito. Unapaswa kupunguza uzito hasa kama una hatari zinazoongeza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo |
Zaidi ya 30 | Una kitambi | Unapaswa kupunguza uzito. Punguza uzito taratibu. Mwone daktari kwa msaada Zaidi kuhusu kupunguza uzito |
Mzunguko wa kiuno
BMI haizingatii uwiano na utofauti wa mafuta katika sehemu mbalimbali za mwili. Mafuta yanayojaa sehemu ya tumbo na kusababisha kitambi cha tumbo, huhusanishwa kwa ukaribu zaidi na magonjwa ya moyo kuliko ilivyo kwa mafuta mengine yanayojaa sehemu zingine za mwili na kusababisha mtu kuwa mnene. BMI haiwezi kutofautisha hili.
- Mzunguko wa kiuno zaidi ya 102 sm kwa wanaume na zaidi ya 88 sm kwa wanawake humaanisha kuwa una kitambi au
- Uwiano wa kiuno- nyonga wa zaidi ya 9 kwa wanaume na zaidi ya 0.85 kwa wanawake humaanisha una kitambi
Upimaji wa mafuta ya Mwili
Njia mbadala ya kutambua kama una kitambi ni kupima asilimia ya mafuta mwilini. Madaktari na wanasayansi kwa ujumla wanakubaliana kuwa wanaume wenye mafuta zaidi ya 25% ya mwili na wanawake wenye mafuta zaidi ya 30% wana kitambi. Hata hivyo, ni vigumu kupima mafuta ya mwili kwa usahihi. Njia inayokubaliwa zaidi ni ile ya kupima uzito wa mtu akiwa ndani ya maji, lakini njia hii hufanyika tu kwenye maabara zenye vifaa maalumu.
Njia nyingine ya kupima asilimia za mafuta mwilini, ni ile ya kukata kipande kidogo cha ngozi na kupima kiasi cha mafuta yaliyo kwenye safu ya ngozi. Matumizi ya njia hizi hayashauriwi sana.
Uchaguzi wa matibabu ya kitambi
Mabadiliko ya mtindo wa maisha
Mtindo wa maisha unaohusisha mazoezi ya mara kwa mara, pamoja na ulaji wa chakula bora ndio njia bora zaidi ya kupunguza uzito. Kupungua kwa uzito, hata kama ni kidogo tu, kunaboresha afya ya mtu. Msaada kutoka kwa familia na marafiki ni muhimu sana.
Wakati unapochagua aina ya chakula na muda wa kula, lengo lako kuu linapaswa kuwa kujifunza njia mpya za mtindo wa maisha ili uzifanye kuwa utaratibu wa kila siku wa maisha yako.
Watu wengi wanaona vigumu kubadili tabia zao za ulaji. Watu hawa wanahitaji kuhamasishwa kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha.Unapaswa kuyafanya mabadiliko hayo kuwa sehemu ya maisha yako.
Kushauriwa na mtaalamu wa chakula na mlo (dietitian) husaidia kuweka malengo safi, bora kiafya na yanayotekelezeka, hii husaidia kupunguza uzito huku ukiendelea kuwa na afya njema. Mtaalamu wa chakula na mlo anaweza kukufundisha kuhusu:
- Uchaguzi wa chakula bora
- Vutafunio bora
- Vinywaji vyenye sukari nyingi
- Ukubwa au wingi wa chakula unachotakiwa kula
- Njia mpya za kuandaa chakula
Kujinyima chakula kulikokithiri (chini ya kalori 1,100 kwa siku) si salama na mara nyingi hakufanyi kazi vizuri. Kujinyima chakula kulikopitiliza husababisha mtu kula vyakula visivyo na vitamini na madini ya kutosha. Watu wengi wanaojaribu kupunguza uzito kwa namna hii hujikuta wamerudi kwenye mtindo wao mbovu wa kula chakula na huongezeka tena uzito maradufu.
Watu wengi wanapokuwa na msongo wa mawazo hujikuta wakila chakula kila wakati na hii husababisha wao kuongezeka uzito. Jifunze njia mpya za kudhibiti msongo, badala ya kujifukia kwenye chakula. Kwa mfano, fanya mazoezi, ongea na mtoa huduma ya afya kama una sonona ili akusaidie.
Dawa na Tiba za mitishamba
Unaweza kuona matangazo ya virutubisho na dawa za mitishamba ambayo hudai kuwa watakusaidia kupunguza uzito. Mengi ya madai haya si kweli, na baadhi ya virutubisho huwa na madhara mabaya kwa mtumiaji. Ongea na mtoa huduma ya afya kabla ya kuzitumia.
Kuna dawa kadhaa zinazotolewa na daktari zinazosaidia kupunguza uzito. Watu wengi hupunguza kati ya kilo 2.5 – 5 baada ya kutumia dawa hizi. Watu wengi pia huongezeka uzito tena baada ya kuacha kutumia dawa hizi, hasa kama hawakufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha, kama kufanya mazoezi na kupunguza ulaji wa vyakula visivyo na afya.
Upasuaji
Upasuaji hufanyika ili kupunguza hatari ya mtu mwenye kitambi kupata magonjwa mengine. Magonjwa haya ni pamoja na:
Upasuaji unaweza kuwasaidia watu ambao wamekuwa na kitambi kwa zaidi kwa miaka 5 au zaidi na hawajaweza kupungua uzito kwa njia nyingine za matibabu, kama vile kula mlo bora, mazoezi, au kwa kutumia dawa.
Upasuaji peke yake sio jibu la kupungua uzito. Upasuaji utakusaidia kula kwa kiasi, lakini kwa sehemu kubwa utapaswa kufuata masharti kadhaa. Unapaswa kujizatiti kwa kula mlo bora na kufanya mazoezi ya mara kwa mara baada ya upasuaji. Ongea na daktari wako ili kuona kama upasuaji ni chaguo zuri kwako.
Aina mbili za upasuaji zinazofanyika ili kupunguza uzito ni:
- Laparoscopic gastric banding
- Gastric bypass surgery
Aina hizi za upasuaji hufanyika ili kupunguza ukubwa wa tumbo. Ukubwa wa tumbo ukipungua na kiasi cha chakula mtu anachokula hupungua pia.
Unaweza kupata matatizo kutokana na upasuaji huu. Tatizo moja linalowapata baadhi ya watu ni kutapika baada ya kula chakula zaidi ya kiwango kinachoweza kutunzwa na tumbo lako jipya
Kuzuia kitambi
Nini cha kutarajia ukiwa na kitambi?
Matatizo yanayoweza kutokea ukiwa na kitambi
Kitambi ni hatari kwa afya. Uzito wa ziada huongeza shinikizo katika sehemu zote za mwili. Watu wenye kitambi wako katika hatari kubwa ya kupata matatizo mengi ya kiafya:
- Matatizo ya mifupa na maungio- uzito wa ziada huiongezea mzigo mifupa na maungio. Hii inaweza kusababisha yabisi kavu inayosababishwa na kusagika kwa maungio (osteoathritis), ugonjwa huu husababisha maumivu makali na kukakamaa kwa viungo.
- Mawe kwenye mfuko wa nyongo (gallstones) na matatizo ya ini
- Mshtuko wa moyo unaotokana na ugonjwa wa moyo unaosababishwa na matatizo ya mishipa ya moyo, kushindwa kwa moyo kufanya kazi yake, na kiharusi
- Kuwa na kiwango kikubwa cha mafuta mabaya mwilini, kunakoongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo
- Shinikizo la juu damu
- Kisukari
- Kuacha kupumua wakati ukiwa usingizini (sleep apnea). Hii inaweza kusababisha uchovu wakati wa mchana au kusinzia sinzia mchana,kukosa umakini na matatizo mengine kazini.