Nisafishe vipi kidonda nikiwa nyumbani?
Dumbukiza kidonda kwenye maji ya uvuguvugu. Tumia sabuni na kitambaa laini kusafisha ngozi inayozunguka kidonda. Jaribu kuhakikisha sabuni haingii kwenye kidonda. Muulize daktari kama unapasawa kutumia kitu kingine chochote isipokuwa maji na sabuni, baadhi ya vitakasaji (kama vile hydrogen peroxide au iodine) vinaweza kupunguza kasi ya kidonda kupona.
- Kabla ya kuhudumia kidonda, hakikisha unanawa mikono na kuvaa mipira/glavu
- Uchafu wote unapaswa kuoshwa kwanza kutoka kwenye kidonda; kwa baadhi ya wagonjwa, hatua hii inaweza kuhitaji kuonana na daktari. Unaweza kutumia maji ya uvuguvugu, yasiwe ya baridi au unaweza kutumia dawa ya kusafishia kidonda, kutegemea na jeraha. Kuondoa vipande vya uchafu na vimelea hupunguza uwezekano wa kupata maambukizi.
- Unaweza kubana/ukaweka shinikizo moja kwa moja kwenye kidonda kama kinavuja damu. Epuka kufanya hivi kwa kidonda cha kuungua.
- Mazingira ya unyevunyevu huruhusu tishu kujirekebisha zenyewe na kupunguza uwezekano wa kupata kovu. Kupaka dawa ya antibiotiki au mafuta, ikifuatiwa na kufunga kidonda kwa “gauze” husaidia kuongeza unyevunyevu.
- Kulingana na kiasi cha majimaji yanayotoka kwenye kidonda, kidonda kinapaswa kusafishwa na kufungwa tena kila siku au mara mbili kwa siku, au kila “bandage” inapochafuka / kuonekana imelowa sana. Paka dawa au mafuta kwenye kidonda na kisha kifunge tena.
- Kadri kidonda kinavyopona, angalia ishara za maambukizi, hii ni pamoja na wekundu, kuhisi joto kwenye kidonda, kuvimba, usaha, maumivu kwenye sehemu ya jeraha au ugumu kupona.
- Kutoa vizuri vitambaa vya kufunga kidonda ni muhimu kama ilivyo kwenye kukifunga. Inapunguza uwezekano wa kusambaza majimaji ya mwili na kupunguza uharibifu kwa sehemu ya ngozi inayozunguka. Ni muhimu kuondoa kwa uangalifu “dressing” iliyokuwepo kabla ya kuweka nyingine.
Nitazuiaje kidonda kuvuja damu?
Kandamiza na weka shinikizo kwenye kidonda kwa kutumia kitambaa safi, gauze au bandeji kwa dakika 30. Kama ikiwezekana nyanyua kidonda kuwa juu ya usawa wa moyo.
Ni wakati gani niongee na daktari?
Ongea na dakatari kama kidonda kimeingia ndani sana, kama unashindwa kukutanisha ncha za kidonda au kama ncha za kidonda zimetawanyika au kuharibika. Daktari anaweza kuhitaji kukishona kidonda kwa kutumia nyuzi. Ni vizuri pia kuongea na daktari kama unaona kuna dalili za maambukizi kwenye kidonda, kama vile;
- Maumivu yanayozidi kuongezeka
- Wekundu na kuvimba
- Ngozi yenye joto kuzunguka kidonda
- Harufu mbaya inayotoka kwenye kidonda baada ya kushonwa au kufungwa
- Kubadilika kwa rangi au kiasi cha majimaji yanayotoka kwenye kidonda
- Homa
- Kutetemeka/ kuhisi baridi
- Kichefuchefu
- Kutapika
Je, ninahitaji kupatiwa chanjo ya tetenasi/pepopunda?
Unaweza kupata ugonjwa wa tetenasi kama ngozi imepata kidonda. Unaweza kuwa umepata chanjo ya pepopunda ukiwa mtoto, lakini bado unahitaji kupatiwa chanjo ya nyongeza mara kwa mara. Kama una kidonda kidogo ambacho kiko safi, unaweza kuhitaji kupatiwa chanjo ya tetenasi ya nyongeza kama haujapatiwa chanjo ya nyongeza kwa miaka 10 iliyopita. Kama kidonda ni kikubwa au kibaya sana, unapaswa kupata chanjo ya nyongeza kama haujapata chanjo kwa miaka mitano iliyopita. Ongea na daktari ili kuhakikisha umepata chanjo zote unazohitaji