Maelezo ya jumla

Sababu kubwa ya kukohoa ni usumbufu au kuvimba kwa mapafu au koo kwa sababu ya mafua, maambukizi kwenye kifua au pumu. Vitu vinavyosababisha usumbufu kama moshi wa tumbaku, vumbi na chamvua za mimea, zinaweza kusababisha ukakohoa. Kamasi zinazotiririka kutoka juu kwenda chini kwenye sehemu nyuma ya koo ‘’postnasal drip’’ au kucheua asidi ya tumboni inayosababisha kiungulia inasababisha kikohozi pia. Kuna baadhi ya watu wana tabia ya kukohoa wanapokuwa na wasiwasi mwingi.
Kikohozi kinaweza kuwa kikavu, kinachowasha na kukusumbua au kinaweza kibichi kinachotoa makohozi. Baadhi ya madawa unayopewa na daktari yanaweza pia kusababisha kukohoa. Kwa mara chache, kukohoa kunaweza kuwa dalili ya ugonjwa hatari kama kansa.

Mwone daktari kama

Ni vizuri kupanga kumwona daktari kama:

  • Unapata shida au ugumu kupumua au una maumivu ya kifua
  • Unakohoa damu au una makohozi yenye rangi usiyoitambua
  • Una homa au unatokwa jasho jingi
  • Unapungua uzito
  • Unatumia madawa ambayo yanaweza kusababisha kikohozi, kama vile madawa fulani ya kudhibiti shinikizo la damu

Kukohoa – unachoweza kufanya mwenyewe

Kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya ili kudhibiti kikohozi na kutegemeza matibabu yaliyoshauriwa na daktari

  • Kunywa maji angalau glass 8 kwa siku. Unaweza pia kunywa vinywaji vya moto kama vile supu na chai, hizi zinasaidia kupunguza uzito wa makohozi na inakuwa rahisi kuyatoa
  • Jaribu kupooza koo kwa kutumia asali na kinywaji chenye limau. Weka kijiko kimoja cha asali na kipande cha limao ndani ya kikombe cha chai.
  • Kwa kawaida haipaswi kuzuia au kupoza kikohozi, kwa sababu kunasaidia kusafisha kifua. Lakini kama una kikohozi kikavu, kinachowasha na kusababisa iwe ngumu kulala au kufanya kazi, unaweza kutumia dawa za kupooza kikohozi ‘’cough suppressants’’.
    • Dawa za kupooza kukohoa zina ‘’dextromethorpha’’ ambayo itasaidia kudhibiti kikohozi kikavu kinachokusumbua na kusababisha ukose usingizi au ushindwe kufanya kazi. Usinywe pombe unapokuwa unatumia dawa za kudhibiti kukohoa.
    • Kama una kikohozi kinachotoa makohozi ni vyema usitumia madawa ya kudhibiti kukohoa kwa sababu kukohoa kunasaidia kusafisha kifua (Dawa ya kulainisha makohozi ‘’extpectorants’’ huwa hazisaidii sana)
    • Kuwa makini unapokuwa unatumia madawa ya kudhibiti kukohoa wakati wa mchana, baadhi yao yanaweza kukusababishia usingizi
  • Kuvuta hewa yenye mvuke inasaidia kulainisha makohozi na kupooza kikohozi. KUJIFUKIZA kunasaidia kuyeyusha kamasi kwenye pua, koo na kwenye uwazi wa mianzi ya pua ‘’sinus’’ na kulainisha kohozi ili litoke kwa urahisi
    • Weka maji ya moto kwenye bakuli, yasiwe yanachemka yakakuunguza. Unaweza kuongeza ndani miti yenye harufu nzuri ili kuongeza aroma, lakini sio lazima
    • Inamia bakuli na funika kichwa kwa taulo, na taratibu vuta mvuke. Kama pua zimeziba vuta kwa mdomo mpaka pua zitakapozibuka.

      kukohoa
      Kujifukizia
  • Kutumia mto mmoja au zaidi unapokuwa umelala kunasaidia kupunguza kukohoa sana wakati wa usiku. Tumia mto.
  • Epuka maeneo yenye moshi au yenye uchafuzi mkubwa wa mazingira au kuwa karibu na watu wanaovuta sigara. Kama unavuta, ACHA.

Kukohoa – mwone daktari

Panga kumwona daktari kama:

  • Unaona kikohozi kinazidi kuwa kibaya zaidi au kama unaona hakijaanza kupoa baada ya wiki ya kukohoa
  • Unachoka sana baada ya kukohoa
  • Unaona makohozi yamebadilika rangi na kuwa ya kijani, njano au kama yana damu

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ency/article/003072.htm

Shares:
2 Comments
  • Abasi Zuberi Shabani
    Abasi Zuberi Shabani
    June 6, 2021 at 8:09 pm

    Asante kwa mafunzo yako, ntayafanyia kazi

    Reply
    • Dr.Mniko
      Dr.Mniko
      June 9, 2021 at 6:24 pm

      Asante pia na endelea kuwa nasi

      Reply
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *