Maelezo ya jumla
Kuongeza njia wakati wa kujifungua ( Episiotomy) ni utaratibu unaofanyika kwa kuchana ngozi iliyo kati ya uke na mkundu. Utaratibu huu hufanyika wakati wa kujifungua ili kupanua uke wa mwanamke ili mtoto anayezaliwa apite kwa urahisi.
Je, kuongeza njia wakati wa kujifungua kunafanyikaje?
Kabla tu ya mtoto kuzaliwa, mkunga au daktari hutia dawa ya ngazi na kisha hukata mara moja au mara mbili.
Mkato huu huwa wa ulalo (kutoka kulia kwenda kushoto au kushoto kwenda kulia). Aina nyingine ya mkato, hufanyika moja kwa moja kutoka kwenye uke kuelekea kwenye mkundu. Mikato yote hii hufanya uke kuongezeka upana. Baada ya mtoto na kondo la nyuma kuzaliwa, mkato huu hushonwa vyema kwa nyuzi maalumu
Nani anahitaji kuongeza njia wakati wa ujauzito?
Zamani, kuongezewa njia kulikuwa jambo la kawaida, na utaratibu huu ulikusudiwa kupunguza uwezekano wa kuchanika kwa uke wakati wa kujifungua. Siku hizi, haishauriwi kufanya utaratibu huu bila sababu ya msingi.
Kuongeza njia hufanyika kunapokuwepo ugumu wakati wa kujifungua. Kuongeza njia wakati wa kujifungua kunaweza kukahitajika kichwa au mabega ya mtoto yanapokua makubwa kuliko uke wa mama, au kama mtoto amekaa vibaya (kama ametanguliza miguu au matako) wakati wa kujifungua na kusababisha matatizo wakati wa kujifungua.
Inaweza pia kuhitajika ili kuharakisha mchakato wa kujifungua kama kuna wasiwasi kuhusu mapigo ya moyo ya mtoto.
Nini cha kutarajia baada ya kuongeza njia wakati wa kujifungua?
Mkato unaotokana na kuongeza njia hupona bila matatizo na inaweza kuwa rahisi kutibu mkato wa aina hii kuliko mchaniko unaotokana na uzazi.
Unaweza kuendelea shughuli zako za kawaida muda mfupi tu baada ya kujifungua. Nyuzi zinazotumika ni maalumu na hazihitaji kutolewa baadae. Unaweza kupunguza maumivu kwa dawa na barafu kwa masaa 24 ya kwanza, ikifuatiwa na kuoga maji ya uvuguvugu.
Matatizo yanayoweza kutokea
Tafiti nyingi zimegundua kuwa utaratibu huu hauna faida yoyote ukifanyika kwa uzazi usio kuwa na matatizo yoyote. Na hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba utaratibu unaboresha tendo la ngono kwa mwanamke. Pia imegundulika kuwa wanawake walioongezewa njia wakati wa kujifungua hupata maumivu wakati wa kujamiiana na huchukua muda mrefu kidogo kuanza kufanya ngono tena baada ya kujifungua.
Kuna uwezekano mdogo kuwa, mkoto uliowekwa ili kuongeza njia wakati wa kujifungua, unaweza kuongezeka mpaka kuifikia misuli inayozunguka mkundu. Hili linaweza kusababisha matatizo baadaye, mgonjwa anaweza kushindwa kuzuia gesi au kinyesi.
Hatari nyingine ni pamoja na:
- Kuvuja damu
- Kuvia damu
- Kushindwa kuzuia kinyesi au gesi
- Maambukizi
- Kuvimba