Kupima uzito na kulinganisha na umri
Kupima uzito na kulinganisha na umri – Kipimo hiki hutumika kutathmini hali ya lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Ni muhimu kumpima mtoto angalau mara moja kila mwezi ili kuweza kupata mwelekeo na kasi ya ukuaji wa mtoto, hivyo kujua hali yake ya lishe . Kipimo hiki hutumika kwenye kliniki za watoto.
Jinsi ya kutafsiri baada ya kupima uzito na kulinganisha na umri
Uzito wa mtoto hulinganishwa na umri wake kwa kutumia kadi ya mtoto ya kliniki ambayo ina rangi kuu nne zinazoashiria hali ya lishe ya mtoto.
- Rangi nyekundu huashiria hali duni ya lishe (utapiamlo mkali),
- Kijivu huashiria uzito pungufu kulingana na umri wake (utapiamlo wa kadiri) na
- Ile ya kijani huashiria hali nzuri ya lishe.
- Endapo mtoto yuko katika rangi nyeupe ina maana uzito wake umezidi.
Ni muhimu sana kuzingatia mwelekeo wa mstari wa ukuaji kwani watoto huongezeka uzito wanapokua; endapo uzito unapungua bila kujali mtoto yupo katika rangi ipi inaashiria kuna tatizo la kiafya au ulishaji duni. Fanya uchunguzi kulibaini mapema.
Iwapo mtoto ameongezeka hata kama yuko kwenye rangi nyekundi au kijivu, ni dalili nzuri hivyo mama/mlezi ampongezwe ili kumjengea kujiamini ili aendelee kufanya vizuri.
Hatua za kuchukua kufuatana na tafsiri ya vipimo
Rangi kwenye kadi | Tafsiri | Hatua za kuchukua |
Nyekundu |
Utapiamlo mkali |
Mzazi au mlezi apewe unasihi wa lishe wa jinsi ya kuboresha ulishaji wa mtoto wake. Afuatiliwe kwa karibu kuhusu matibabu na ulishaji |
Kijivu | Utapiamlo wa wastani | Mzazi au mlezi apewe unasihi wa lishe wa jinsi ya kuboresha ulishaji wa mtoto wake. Afuatiliwe kwa karibu kuhusu ulaji wake na kama ana maradhi atibiwe |
Kijani | Uzito unaofaa | Mama au mlezi apongezwe na kutiwa moyo. Mzazi au mlezi apewe unasihi wa lishe wa jinsi ya kuendelea kumlisha mtoto wake. |
Nyeupe | Uzito umezidi | Jadili na mama/mlezi kuhusu ulishaji wa mtoto kwani hali hii humwongezea mtoto uwezekano wa kuwa na uzito mkubwa hata atakapokuwa mtu mzima na hivyo kumuweka katika hatari zaidi ya kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza. Mtoto asinyimwe chakula bali kiasi na ubora viangaliwe. |
Angalizo: Zingatia mwelekeo wa mstari wa ukuaji wa mtoto
Kumbuka:
Uzito wa mwili hutegemea kiasi na aina ya chakula unachokula; pamoja na shughuli unazofanya. Mara nyingi unene hutokana na kula chakula kingi kuliko mahitaji ya mwili na kutokufanya mazoezi.