Maelezo ya jumla
Wanawake wengi wana tatizo la kushindwa kuzuia mkojo, yaani wanajikojolea /kuvuja mkojo kwa sababu ya kushindwa kudhibiti kibofu. Tatizo hili linazidi zaidi kunapoongezeka mgandamizo kwenye kibofu, kwa mfano unaweza kujikojolea/ kushindwa kuzuia mkojo unapokohoa, kupiga chafya, kufanya mazoezi, au kuinua kitu kizito. Hali hii inaweza kusababishwa na kulegea kwa misuli ya nyonga, misuli hii inategemeza kibofu, mji wa mimba (uterasi) na puru/rektamu. Ni kawaida kulegea kwa misuli ya nyonga kwa wanawake waliojifungua watoto. Sababu nyingine za kushindwa kuzuia mkojo ni pamoja na kufunga choo, maambukizi kwenye kibofu, mabadiliko ya homoni baada ya ukomo wa hedhi, na baadhi ya dawa kama vile ‘’diuretics’’ (dawa hizi zinatumika kudhibiti shinikizo la juu la damu). Baadhi ya wanawake wanatatizo la kushindwa kuusubirisha mkojo, akihisi kukojoa inabidi akakojoe haraka, la sivyo anaweza kujikojolea au wengine mkojo unapita bila hata kujijua. Tatizo hili wakati mwingine linaweza kutokana na matatizo kwenye neva zinazodhibiti kibofu.
Mwone daktari kama
Panga kumwona daktari kama:
- Unavuja mkojo mwingi sana
- Unahisi kiu kikali na unakunywa maji au vinywaji kwa wingi sana
- Unavuja mkojo bila habari au kama unajikojolea au unashindwa kushikilia mkojo mpaka kufika chooni
- Unatumia dawa ambazo zinasababisha ushindwe kudhibiti mkojo
Unachoweza kufanya wewe mwenyewe
Kuna hatua kadhaa unazoweza kuzichukua ili kuboresha udhibiti wa kibofu kama unavuja mkojo baada ya kucheka au kupiga chafya, au unaweza kuzitumia pamoja na matibabu uliyopewa na daktari
- Kunywa maji angalau glass 6-8 kwa siku ili mkojo usiwe mzito sana. Lakini usinywe maji mengi sana kwa wakati mmoja, ukifanya hivi inaweza kusababisha ukavuja mkojo
- Jaribu kuongeza muda kati ya wakati ulioenda kukojoa na mwingine ili kujengea kibofu uwezo wa kuhimili mkojo. Usiwe na haraka, kojoa taratibu mpaka mkojo utakapoisha wote. Kojoa kabla haujaenda kulala
- Punguza kunywa chai, kahawa, cola na pombe; Zinaweza kusababisha ukaanza kuhisi hamu ya kukojoa au inaweza kusababisha ukajikojolea bila kujua. Epuka kunywa vinywaji vya viwandani vyenye kaboni, vinywaji vya juisi ya jamii ya mlimao na vyakula vyenye pilipili; Hivi vyote vinaweza kusumbua kibofu
- Fanya mazoezi ya Kegel ‘’Kegel exercise’’
- Mazoezi ya kegel yanaweza kufanyika mahali popote, ukiwa umesimama au ukiwa umekaa. Inaweza kuchukua kama wiki 12 kabla ya kuanza kuona faida zake, na unapswa kuendelea kuyafanya ili dalili zisijirudie tena
- Jaribu kukaza na kulegeza misuli ya nyonga, hii ni ile misuli unayotumia kuzuia mkojo katikati kabla ya kumaliza kukojoa. Kama hauijui, jaribu kama unazuia mkojo usitoke; misuli uliyoikaza ndiyo inayoizungumzia ‘’pelvic floor muscles’’
- Kaza misuli hiyo na ishikilie kwa sekunde kadhaa na kisha achia taratibu. Rudia hivi mara kadhaa. Anza taratibu mpaka uweze kukaza mara 10, na kwa kila mkazo ukiishikilia kwa sekunde 10, huku ukipumzika kwa sekunde 4 baada ya kukaza.
- Fanya zoezi hili mara kwa mara mpaka litakapokuwa sehemu ya maisha yako
- Kama unavuja mkojo wakati wa shughuli kama vile kukimbia, ingiza ‘’tampon’’ kabla haujaanza kukimbia ili kutegemeza kibofu. Iondoe baada tu ya kumaliza kukimbia. Tumia njia hii pale tu inapohitajika.
Kuzuia
Ukifanya mambo haya, yanaweza kupunguza mgandamizo na harara kwenye kibofu
- Jaribu kupunguza uzito
- Kula vyakula vyenye nyuzi nyuzi kwa wingi ili kuzia kufunga choo
- Acha kuvuta sigara. Nikotini inasumbua kibofu, na moshi unasababisha kukohoa na kusababisha misuli kukaza
Omba msaada wa kitabibu
Panga kumwona daktari kama:
- Unaona tatizo linaongezeka au kiasi cha mkojo unaovuja kinaongezeka
- Haujaona mabadiliko au kuboreka kwa hali ya kudhibiti mkojo baada ya wiki 4-6
- Ukiona unaanza kuwa dalili nyingine