Kutetemeka ni nini?

Kutetemeka ni hali ya kutikisika, kushtuka au mpapatiko inayotokea kwenye sehemu ya mwili bila hiari yako mwenyewe. Mara nyingi viganja vya mikono ndio hupatwa na hali hii ya kutetemeka, lakini mikono, kichwa, miguu na hata sauti vinaweza kutetemeka. Kutetemeka ni hali inayowapata zaidi watu wa umri wa kati na wazee, lakini kunaweza kumtokea mtu wa umri wowote. Baadhi ya hali za kutetemeka inaweza kuwa ngumu kuziona, na baadhi hali inaweza kuwa mbaya kiasi kwamba mtu anashindwa kuandika au kushika vitu.

Kuna aina mbalimbali za hali ya kutetemeka. Kuna mitetemo inayotokea mtu akiwa ametulia (resting tremors). Mitetemo inayotokea unapokuwa unajongesha sehemu ya mwili (action tremors). Mitetemo inayotokea unapouweka mwili au sehemu ya mwili katika mkao fulani – kwa mfano ukinyoosha mkono au mguu (postural tremor). Mitetemo inayotokea ukiwa unafanya kazi au shughuli fulani – kwa mfano, kuchora au kumimina kinywaji (kinetic tremor). Ni muhimu kutambua ni aina gani ya hali ya kutetemeka uliyonayo.

Kutetemeka kunasababishwa na nini?

Mtu yeyote anaweza kutetemeka katika hali fulani. Kwa mfano, unaweza kutetemeka kama umechoka sana, una woga mkubwa, umekunywa kahawa nyingi sana, au kama unafanya baadhi ya kazi (kwa mfano, kuingiza uzi kwenye tundu la sindano). Matukio mengi ya kutetemeka yanawapata zaidi watu walio ana afya njema kabisa, lakini kutetemeka pia kunaweza kuwa moja ya ishara kuwa unaumwa.

Baadhi ya dawa, hii ni pamoja na corticosteroids, amphetamines, na dawa za kutibu magonjwa ya akili, zinaweza kusababisha hali ya kutetemeka. Woga uliopitiliza na matatizo ya kisaikolojia, matatizo ya tezi dundumio, matumizi mabaya ya pombe au kuacha kutumia pombe, kiharusi au majeraha ya kichwa, na ugonjwa wa Wilson (wilsons disease – ugonjwa adimu wa ini) unaweza pia kusababisha kutetemeka. Ugonjwa wa Parkinson unaweza kusababisha mitetemo mtu akiwa ametulia, na unawapata zaidi wazee. Baadhi ya hali za kutetemeka zinatokea kwenye familia, na baadhi hazina sababu inayojulikana.

Nitajuaje ni nini kinasababisha hali yangu ya kutetemeka?

Daktari atakuuliza kuhusu hali yako ya kutetemeka, matumizi ya pombe na dawa, na kuhusu historia ya kiafya ya familia yako. Anaweza kuchunguza uwezo wako, nguvu, mfumo wa fahamu (kwa mfano uoni, uwezo wa kunusa, uwezo wa kuhisi), mjongeo wako na balance – ulinganifu. Daktari mara nyingi anaweza kutambua ni nini kinasababisha mitetemo kwa kuuliza maswali na kukufanyia uchunguzi wa mwili. Wakati mwingine, vipimo vya kiwango cha sukari kwenye damu, vipimo vya kuangalia uwezo wa figo kufanya kazi au vipimo vya kuangalia uwezo wa ini kufanya kazi vinaweza kuhitajika. Kwa mara chache, unaweza kuhitaji kupigwa picha ya eksirei ya kichwa.

Tiba ya tatizo la kutetemeka ni ipi?

Hali nyingi za kutetemeka haziwezi kutibiwa na kupona kabisa, lakini zinaweza kudhibitiwa kwa tiba ili zisikusumbue sana. Aina ya matibabu inategemea sana sababu ya mitetemo. Dawa zinaweza kusaidia kwa mtu mwenye mitetemo ambayo sababu yake haijulikani, ambazo mara nyingi hutokea kati ya wanafamilia na huzidi kuongezeka unapoanza kujongea au kufanya kazi.

Dawa pia zinaweza kusaidia kudhibiti hali ya kutetemeka kwa wagonjwa wa Parkinson, ugonjwa wa Wilson na matatizo ya tezi dundumio. Daktari anaweza pia kupendekeza uache kutumia aina kadhaa za dawa au kuacha kutumia baadhi ya bidhaa zinazosababisha mitetemo (kwa mfano, pombe, kahawa). Upasuaji ni moja ya njia zinazoweza kutumika kutibu hali kali sana za mitetemo zinazoshindwa kudhibitiwa kwa dawa.

Baadhi ya matibabu yanayoboresha maisha ya wagonjwa wote wenye mitetemo ni pamoja na mazoezi ya viungo na mwili au mazoezi ya kufanya kazi, kutumia vifaa vya kujisaidia (kwa mfano, kutumia vyombo va kula vyenye mikono mikubwa, vifungo vya shati vya kupachika, kutumia mrija kunywea vinywaji badala ya kushika kwa mkono kikombe).

Angalizo

Taarifa zilizotolewa katika ukurasa huu zimetoa muhtasari na zinaweza zimsifae kila mtu. Ongea na daktari ili kung’amua kama taarifa hizi zinakufaa na wewe au jaribu kutafuta habari zaidi kuhusu shida hii.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ency/article/000762.htm

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *