Maelezo ya jumla
Kutokwa damu (bleeding) kunaweza kutokea nje au ndani ya mwili:
- Ndani ya mwili, damu huvuja kutoka kwenye mishipa ya damu au viungo
- Nje ya mwili, damu hutoka kupitia kwenye matundu ya asili (kama vile uke, mdomo, au njia ya haja kubwa) au damu inapotoka kupitia kwenye ngozi
Daima tafuta msaada wa dharura kama unatokwa na damu nyingi, au kama unahisi unavuja damu ndani ya mwili. Kuvuja damu ndani ya mwili kunaweza kuwa hatari sana na hata kutishia maisha. Majeraha makubwa yanaweza yasivuje damu nyingi sana, na baadhi ya majeraha madogo (kwa mfano, majeraha ya kichwani) yanaweza kuvuja damu nyingi sana. Watu wanaotumia dawa za kuzuia damu kuganda au watu walio na ugonjwa kama vile hemophilia unaozuia damu kuganda, wanaweza kuvuja damu kupita kiasi. Matibabu ya haraka yanahitajika wanapovuja damu.
Kubana au kuweka shinikizo moja kwa moja kwenye eneo linalovuja damu hupunguza damu kuvuja. Daima, osha mikono yako kabla (kama inawezekana) na baada ya kutoa huduma ya kwanza kwa mtu anayevuja damu, ili kuepuka maambukizi. Jaribu kutumia glavu (gloves) wakati wa kumtibu mtu anayevuja damu. Unaweza kupata virusi vinavyosababisha homa ya ini (hepatitis ) ukigusa damu ya mtu aliyeambukizwa. Unaweza pia kupata VVU kama damu ya mtu aliyeambukizwa itaingia kwenye jeraha lililowazi – hata dogo.
Japo majeraha yanayosababishwa na kuchomwa na vitu vyenye ncha kali hayavuji damu sana, ni rahisi sana kupata maambukizi. Tafuta matibabu ili kuzuia tetanasi au maambukizi mengine. Majeraha ya tumbo na kifua yanaweza kuwa hatari sana kwa sababu ya kuwepo uwezekano wa kuvuja damu ndani kwa ndani. Tafuta matibabu ya haraka kwa jeraha lolote la tumbo au kifua. Ikiwa viungo vya ndani vimetokeza kupitia kwenye jeraha, usijaribu kuvisukumiza ndani. Funika jeraha kwa bandage/kitambaa kilicholowekwa kwenye maji na kisha bana kidogo ili kupunguza kuvuja kwa damu.
Kuvuja damu kunaweza kusababisha damu kuvia chini ya ngozi baada ya kupigwa au kuanguka. Weka kitambaa au kifuko cha barafu kwenye eneo uliloumia ili kupunguza uvimbe. Usiweke barafu moja kwa moja kwenye ngozi.
Je! Nini dalili za kutokwa damu?
- Damu huvuja kutoka kwenye jeraha la wazi
- Kuvia kwa damu chini y ngozi
- Mshtuko (shock), ambao unaweza kusababisha mojawapo au zaidi ya dalili zifuatazo:
- Kuchanganyikiwa au kupungua kwa fahamu
- Ngozi kuwa baridi na yenye kunata
- Kizunguzungu kinachotokea baada ya kuumia
- Kiwango cha chini cha shinikizo la damu
- Kuongezeka kwa kiwango cha mapigo ya moyo
- Kupumua kwa shida
- Uchovu
Dalili za kuvuja damu ndani ya mwili:
- Maumivu ya tumbo na kuvimba kwa tumbo
- Maumivu ya kifua
- Kuvuja damu kupitia kwenye matundu ya asili (masikio, mdomo, pua, mk*ndu, uke au uume)
- Damu kwenye kinyesi (kinaonekana cheusi, kahawia, au chekundu)
- Damu kwenye mkojo (unaonekana mwekundu, waridi, au rangi ya chai)
- Kutapika matapishi yenye damu (yanaonekana mekundu, au kahawia kama kahawa)
- Kutokwa na damu ukeni (nzito kuliko kawaida au baada ya damu kukatika(menopause))
Mabadiliko ya rangi ya ngozi hutokea siku kadhaa baada ya kuumia (ngozi inaweza kuwa nyeusi, bluu, zambarau, kijani)
Kutokwa damu husababishwa na nini?
Kuvuja damu kunaweza kusababishwa na majeraha au kutokea bila sababu yoyote. Kuvuja damu bila sababu yoyote mara nyingi husababishwa na matatizo ya viungo, mfumo wa kumeng’enya chakula na mfumo wa mkojo.
Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
Tafuta msaada wa haraka kama:
- Unashindwa kuzuia damu kutoka
- Inahitajika kufunga mguu kwa kamba ”tourniquet” ili kuizuia damu kutoka
- Kutokwa damu kumesababishwa na jeraha baya
- Jeraha linahitaji kushonwa
- Mchanga au uchafu kwenye jeraha hauwezi kuondolewa kwa urahisi/ kwa kusafisha polepole
- Unafikiri kuna damu inavuja ndani kwa ndani au kama unaona hali yako inaendelea kuwa mbaya kwa sababu ya kupoteza damu nyingi.
- Ishara za maambukizi zimeanza kujitokeza, hii ni pamoja na kuongezeka kwa maumivu, wekundu, uvimbe, kutokwa na majimaji ya rangi ya njano au samawi kwenye kidonda, kuvimba kwa tezi za limfu, homa, au michirizi myekundu inayotoka kwenye kidonda kuelekea kwenye moyo.
- Jeraha limetokana na kuumwa na mnyama au binadamu
- Mgonjwa hajapata sindano ya tetanasi ndani ya miaka 5-10 iliyopita
Uchaguzi wa matibabu
Huduma ya kwanza ni muhimu kwa mtu anaetokwa na damu. Kama mtu anatokwa damu nyingi sana au ana mshtuko au anavuja damu ndani ya mwili, apate msaada wa dharura mara moja.
- Kuwa mtulivu na mhakikishie mtu huyo kuwa unatoaa msaada.
- Kama jeraha liko juu juu, lisafishe kwa sabuni na maji kisha likaushe kwa kitambaa safi.
- Mlaze mtu huyo chini. Hii huongeza mtiririko wa damu kwenye ubongo na kupunguza uwezekano wa kupoteza fahamu.
- Ondoa uchafu wowote unaoonekana kwenye jeraha. Kitu kama kisu, fimbo, au mshale kikiwa kimebakia mwilini Kufanya hivyo kunaweza kusababisha uharibifu zaidi na kusababisha damu kutoka zaidi. Weka bendeji kukizunguka na kama ikiwezekana kifunge mahala pake kisitoke.
- Bana jeraha la nje kwa bendeji, kitambaa safi au hata nguo. Kama hakuna chochote bana hata kwa kiganja cha mkono. Kubana jeraha ni njia bora sana ya kupunguza damu kuvuja, lakini si kwa jeraha la jicho
- Endelea kubana mpaka damu itakapoacha kutoka. Ikiacha kutoka funga kwa kitambaa safi au bendeji. Weka kifuko cha barafu juu ya jeraha lililofungwa vyema ili kupunguza uvimbe. Usichungulie kuona kama damu imeacha kutoka.
- Kama damu itajaa kwenye kitambaa cha kwanza ulichokiweka , usikitoe, weka tu kingine juu yake mpaka itakapoacha kutoka. Hakikisha unapata matibabu mapema.
- Kama damu inatoka nyingi sana, pata msaada wa tabibu. Tuliza sehemu ya mwili iliyojeruhiwa. Mlaze chali mtu aliyeumia, nyanyua miguu yake juu kama sentimita 30, na mfunike kwa shuka au blanketi.
- USIMHAMISHE mtu aliyeumia kichwa, shingo, mgongo, au kuumia mguu, kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kumuumiza zaidi. Tafuta msaada wa matibabu haraka iwezekanavyo.
USIFANYE HAYA
- Kama kuna njia nyingine, usitumie tourniquet kudhibiti damu, na kama ikikulazimu kufanya hivyo uwe na uhakika kuwa hakuna njia nyingine inayoweza kutumika kuzuia damu, hii ni kwa sababu kufanya hivyo kunaweza kusababisha madhara zaidi kuliko mema. Tourniquet inapaswa kutumiwa katika hali inayotishia maisha pekee na inapaswa kuwekwa na mtaalamu.
- Kama kubana jeraha kunashindwa kupunguza damu kuvuja, na damu inavuja sana, tourniquet inaweza kusaidia mpaka utakapofika hospitalini.
- Inapaswa kufungwa na kukazwa kwenye mguu kati ya eneo linalotoka damu na moyo.
- Angalia tourniquet kila baada ya dakika 10 hadi 15. Ikiwa damu itaacha kutoka, unaweza kuitoa.
- USICHUNGULIE jeraha ili kuona kama damu inaendelea kutoka. Usilisumbue jeraha.
- USIONDOE vitu vilivyokwama kwenye jeraha, kufanya hivi kunaweza kusababisha damu kuvuja zaidi.
- USIONDOE Kitambaa kilichokwisha lowa damu kwenye jeraha, badala yake weka kingine juu yake.
- USIJARIBU kusafisha jeraha kubwa. Hii inaweza kusababisha kutokwa damu zaidi
- USIJARIBU kusafisha jeraha baada ya kudhibiti damu kuvuja. Pata msaada wa kitabibu
Dawa za kuepuka
Wagonjwa wanaonatokwa damu wanapaswa kuepuka kutumia dawa zifuatazo:
- Enoxaparin
- Fondaparinux
Kama unatokwa na damu, ongea na daktari kabla ya kuanza au kuacha dawa yoyote.
Kuzuia kutokwa damu
Fanya maamuzi ya hekima, weka visu na vitu vikali mbali na watoto wadogo.
Chomwa chanjo zote, hasa chanjo ya tetanasi.