Ni nini husababisha kutokwa damu katika hatua za mwanzo za ujauzito?
Karibu mwanamke mmoja kati ya wanne watapata tatizo la kutokwa damu katika hatua za mwanzo za ujauzito/ mimba. Hasa katika miezi michache ya mwanzo. Sababu zinaweza kuwa nyingi. Baadhi ya sababu zilizozoeleka kusababisha shida hii ni hali ya kutishia kutoka kwa mimba, mimba iliyotungwa nje ya mji wa mimba na kutoka kwa mimba.
- Hali ya kutishia kutoka kwa mimba (threatened abortion) ni hali ya kutokwa damu kutoka kwenye mji wa mimba lakini ujauzito unabakia kuwa sawa. Kwa mara chache mabonge ya damu yanaweza kutengenezeka ndani ya mji wa mimba, na kuongeza uwezekano wa kupoteza ujauzito. Hata hivyo, wanawake wengi wanaopatwa na hali ya kutishia kutoka kwa mimba wanajifungua salama mtoto mwenye afya.
- Mimba iliyotungwa nje ya mji wa mimba (ectopic pregnancy) ni hali ya mtoto kujipandikiza na kukua nje ya mji wa mimba (Uterasi), mara nyingi anajipandikiza kwenye mirija ya uzazi. Kama hali hii ikitokea, eneo hilo hupasuka na kuvuja damu nyingi. Hali hii inaweza kutishia maisha ya mama.
- Kutoka kwa mimba (miscarriage) kunaamisha mimba imetoka kabisa. Hii inatokea kama ujauzito umeshindwa kukua na hakuna mabaki ya kijusi baada ya kutoka kwenye uterasi. Wakati mwingine mama atahitajika kutumia dawa au kufanyiwa utaratibu ili kuondoa mabaki ya tishu au kuzuia damu kuvuja.
Baadhi ya sababu nyingine zinazosababisha kutokwa damu katika hatua za mwanzo za ujauzito ni pamoja na maambukizi, bawasiri, saratani ya shingo ya mlango wa kizazi, na saratani nyingine za wakati wa ujauzito.
Nifanye nini kama natokwa damu katika hatua za mwanzo za ujauzito?
Mpigie daktari simu haraka sana kama unaweza au nenda kaonane nae. Kama unatokwa damu nyingi au unapata maumivu makali, ni vizuri kwenda katika chumba cha wagonjwa wa dharura.
Daktari anaweza kufanya vipimo mbalimbali kuangalia kwa nini unatokwa damu. Unweza kufanyiwa uchunguzi wa nyonga, kipimo cha ultrasound, vipimo vya damu au mkojo. Kwa mara nyingi, kipimo cha ultrasound kinatosha kabisa kukagua kama ujauzito uko sawa. Hata hivyo, kama ni hatua za mwanzo sana za ujauzito, unaweza kuhitaji vipimo zaidi ili kumsaidia daktari kutambua sababu ni nini.
Kutokwa damu katika hatua za mwanzo za ujauzito kunatibiwa vipi?
Matibabu yanategemea sababu ya kutokwa na damu. Hakuna njia nzuri ya kuzuia hali ya kutishia mimba kutoka kwa kutumia dawa, hasa kama damu imekwisha anza kutoka. Kama mimba yako itatoka, daktari atakuangalia kwa makini ili kuhakikisha tishu zote zinatoka zenyewe au kama utahitaji dawa au utaratibu mwingine kuzitoa, atasaidia. Tishu kutokana na ujauzito kujipandikiza nje ya mji wa mimba zinapaswa kutolewa kwa dawa au kwa upasuaji.
Nifanye nini ili kuzuia mimba kutoka?
Kuweka mwili katika hali ya afya ndio njia bora zaidi ya kupata ujauzito na mtoto mwenye afya. Usivute sigara, usiywe pombe, au kutumia dawa za kulevya. Tumia virutubisho wakati wa ujauzito, matumizi ya vidonge vya “folic acid” kabla haujapata ujauzito kunasaidia kupunguza uwezekano wa mtoto kupata tatizo la mgongo wazi.
Kama una matatizo ya kitabibu kama vile shinikizo la juu la damu au kisukari, ongea na daktari kuhusu uangalizi utakaohitaji katika kipindi kizima cha ujauzito. Ni vizuri kuongea na daktari kuhusu shida hizi kabla haujapata ujauzito kama inawezekana.
Hakuna njia ya kuzuia mimba kutoka baada ya damu kuanza kuvuja. Hakuna njia pia ya kutambua kwa hakika kwa nini mimba inatoka. Mara nyingi haitoki kwa sababu yoyote inayosababishwa na mama. Kina mama wengi wanaopoteza watoto wanaweza kupata watoto wenye afya baadae. Kama umepoteza mimba zaidi ya tatu, ongea na daktari ili akufanyie vipimo zaidi na matibabu.