Kuungua kunasababishwa na nini?
Mtu yoyote anaweza kuungua. Kwa Watoto wadogo, majeraha mengi ya kuungua yanasababishwa na kukaa sana kwenye jua, kuoga maji ya moto sana, au kuvuta vitu vya moto kutoka jikoni au juu ya kabati. Watoto wakubwa mara nyingi wanaunguzwa na moto wanapokuwa wakichezea viberiti, milipuko au mafuta. Watu wazima mara nyingi wanaungua baada ya kushika vitu vya moto au ajali.
Uangalifu mkubwa unapaswa kuchukuliwa kuwalinda watoto na wazee kutokana na kuungua, kwa sababu majeraha mengi ya kuungua huwapata wao.
Unawezaje kuzuia kuungua?
Majeraha mengi yanayotokana na kuungua yanatokea kwa ajali, kwa hiyo ni muhimu kuwa makini katika hali ambazo zinaweza kukuweka wewe na watoto wako karibu na moto, vitu vya moto au maji ya moto.
- Kwa wale wenye ngozi nyepesi – vaa nguo za kukukinga ili usiungue na jua
- Kama unapaka dawa za kukukinga na jua (sunscreen), ongeza dawa kila baada ya masaa 2 au mapema zaidi kama unatokwa jasho, kuogelea au kujifuta maji kwa taulo.
- Kagua maji ya kuoga kabla ya kuanza kuoga – yasikuunguze
- Usimwache mtoto mwenyewe karibu na maji au bomba la maji
- Usimbembe mtoto unapokuwa unafanya kazi karibu au na vitu vya moto
- Weka kemikali na viberiti mbali na watoto au vifungie kwenye kabati
- Usimwache mtoto karibu na moto bila usimamizi wa mtu mzima
- Hakikisha kuwa nyaya za umeme, vifaa vya umeme na soketi zote ziko kwenye hali nzuri na salama
- Hakikisha kuwa kuna kizima moto ndani ya nyumba (kama inawezekana)
Ninawezaje kutibu jeraha dogo la kuungua?
Kama ukipata jeraha dogo baada ya kuungua – umeungua sehemu ya juu tu (sehemu ya jeraha ni nyekundu, inauma na haina malengelenge). Pooza sehemu ya jeraha kwa maji ya baridi kwa angalau dakika 20. Usitumie barafu.
Unaweza kupaka Aloe vera cream kama unayo au dawa ya kupaka ya antibiotiki kwenye jeraha. Dawa za kupunguza maumivu kama vile ibuprofen, paracetamol au aspirin zinaweza kusaidia. Kama sehemu ya jeraha itaanza kupata malengelenge, inaweza kumaanisha kuwa umeungua kwenda ndani zaidi ya ulivyodhani. Usitoboe malengelenge. Aina hii ya majeraha yanaweza kutibiwa kwa kupaka Aloe vera cream na kupaka dawa ya antibiotiki na kisha kufunga kwa gauze au bandeji.
Ni wakati gani napaswa kumwona daktari?
Unapaswa kumwona dakatari mapema kama umeungua kwa umeme au kama umeungua eneo kubwa la mwili au maeneo maalumu kama vile usoni, kwenye maungio ya miguu au mikono, au kwenye via vya uzazi. Onana na daktari mapema iwezekanavyo kama jeraha la kuungua limeingia ndani sana, limeanza kupata malengelenge, una kisukari na umepata jeraha la kuungua au kama una upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI), kama eneo la jeraha linauma sana au kama sehemu iliyoungua haijapona baada ya wiki 2.
Angalizo
Taarifa zilizotolewa katika ukurasa huu zimetoa muhtasari na zinaweza zimfae kila mtu. Ongea na daktari ili kung’amua kama taarifa hizi zinakufaa na wewe au jaribu kutafuta habari zaidi kuhusu shida hii.