Maelezo ya jumla
Maambukizi kwenye kibofu (cystitis) yanasababisha utando unaofunika sehemu ya ndani ya kibofu kuvimba, na mara nyingi tatizo hili linatokana na maambukizi. Kama ukiwa na maambukizi ya kibofu, unahisi maumivu kama unaungua unapokuwa unakojoa na unajihisi kukojoa mara kwa mara, hata kama hakuna mkojo kwenye kibofu. Mkojo uaweza kuwa wenye ukungu na unaonuka vibaya, na unaweza kuwa na maumivu sehemu ya chini ya kitovu. Wakati mwingine tatizo hili huanza mara tu baada ya kushiriki ngono. Maambukizi ya kibofu ni tatizo linalowapata wanawake wengi, lakini linawapata wanaume na watoto kwa mara chache.
Mwone daktari kama una maambukizi kwenye kibofu
Kama wewe ni mwanamke, panga kumwona daktari kama:
- Una ujauzito
- Kuna damu kwenye mkojo
- Una maumivu ya mgongo au kwenye sehemu za pembeni, chini kidogo ya mbavu; una homa kali; au kama unatetemeka
- Dalili hazijapungua baada ya masaa 48 ya kufuata njia zifuatazo
Wanaume na watoto wenye dalili zozote za maambukizi kwenye kibofu, wanapaswa kumwona daktari bila kukosa, ili atambue sababu ni nini na kutoa tiba
Unachoweza kufanya mwenyewe ukiwa na maambukizi kwenye kibofu
Ukifuata utaratibu ufuatao inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa kabisa maambukizi ya kawaida kwenye kibofu. Hata hivyo, Dawa za antibiotiki zinaweza kuhitajika
- Kunywa maji ya kutosha ili ukojoe na kuosha vizuri kibofu na kuodoa bakteria.
- Epuka matunda ya jamii ya mlimau, nyanya, vyakula vya pilipili, kahawa, pombe na nikotini. Vyakula vyote hivi vinaweza kusumbua kibofu.
- Kama una maumivu ya tumbo, chukua chupa yenye maji ya moto ikiwa imefunga vizuri na uikumbatie kwenye tumbo ili kupata nafuu. Unaweza pia kutumia madawa ya kupunguza maumivu, madawa kama vile ‘’acetaminophen’’ yanawea kusaidia kupunguza maumivu
- Jaribu kukojoa kabla na baada tu ya kushiriki ngono, hii itasaidia kusafisha bakteria waliongia kwenye kibofu.
Kuzuia maambukizi kwenye kibofu
Ili kuzuia usiapate maambukizi kwenye kibofu mara kwa mara, fanya mambo yafuatayo:
- Kunywa maji glass 8 kwa siku, unaweza pia kunywa vinywaji vingine kama vile juisi
- Kojoa mara kwa mara na hakikisha unakojoa mkojo wote
- Baada ya kujisaidia haja kubwa, jifute au tawadha kutoka mbele kwenda nyuma ili kuzuia kuingiza bakteria
- Kojoa kabla na baada ya kushiriki tendo la ngono
- Vaa kufuli/chupi iliyotengenezwa kwa pamba na epuka kuvaa suruali zinazobana
- Usitumie au kupiga marashi ukeni