Macho mekundu ni nini?
Macho mekundu ni hali inayotokana na kuvimba kwa utando mwepesi unaofunika jicho na sehemu ya ndani ya kope. Macho mekundu ni hali inayotambulika pia kama konjaktivaitisi. Kwa kawaida hali hii inasababishwa na maambukizi ya kawaida ambayo huwa sio tishio. Visa vingi vya macho mekundu vinasababishwa na virusi, lakini pia yanaweza kusababishwa na vimelea wengine (kama vile bakteria, au fangasi) au kizio (kama vile chamvua au vumbi).
Ni zipi dalili za macho mekundu?
Dalili zifuatazo ndizo zinazowapata zaidi watu wenye macho mekundu:
- Wekundu na kuhisi kama macho yanaungua
- Kutokwa na majimaji au uchafu wa njano unaosababisha kope kugandiana pamoja, hasa wakati wa kuamka
- Uoni hafifu / kushindwa kuona vizuri au kushindwa kuona au kuumizwa na mwanga
- Kuvimba kwa kope
- Maumivu kuzunguka macho
Unapaswa kumwona daktari kama dalili zitadumu kwa zaidi ya siku tatu au zaidi.
Macho mekundu yanatibiwa vipi?
Matibabu yanategemea sababu. Macho mekundu yaliyosababishwa na virusi yanapona yenyewe ndani ya wiki moja hata kama usipopata matibabu. Macho mekundu yanayosababishwa na bakteria yanaweza kupona yenyewe bila matibabu, lakini daktari anaweza pia kukuandikia dawa ya kuweka kwenye macho kama una dalili kali sana.
Kama inasababishwa na kizio /aleji, unapaswa kukaa mbali na vitu vinavyosababisha hali na dalili zako kuwa mbaya zaidi. Daktari anaweza kupendekeza utumie dawa ya kuweka kwenye macho ili kuyapooza na kupunguza kuwashwa.
Je, ugonjwa wa macho mekundu unaambukizwa?
Ugonjwa wa macho mekundu unaosababishwa na mzio hauambukizwi, lakini ugonjwa wa macho mekundu unaosababishwa na vimelea unaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja mpaka mwingine. Unaweza kuambukizwa kwa kugusana moja kwa moja na mtu mwenye ugonjwa.
Kwa mfano, unaweza kuupata kwa kufikicha macho kwa vidole vya mikono vilivyokuwa na vimelea, kwa kukohoa au kupiga chafya, au kwa kuogelea katika bwawa moja na mtu mwenye macho mekundu. Unaweza pia kuupata kwa kuchangia vitu binafsi kama vile taulo au vipodozi
Nifanye nini nisisambaze ugonjwa huu?
Ni muhimu kuwa unawe mikono vizuri na utumie karatasi za tishu kujifutia. Usichangie vitu binafsi. Kama una macho mekundu au kama yanatoa uchafu, usivae lenzi za macho “contact lens”. Hauna haja ya kukaa mbali na watu wengine, ila inaweza kuwa vizuri kuwazuia watoto wasiende shuleni kama macho yao ni mekundu ya yamesababishwa na vimelea.