Maelezo ya jumla kuhusu madhara ya tumbaku/sigara

Tumbaku/sigara inaua haijalishi inatumiwa kwa njia gani. Bidhaa za tumbaku/sigara zinazovutwa, huwa na kemikali 7000, zikiwemo angalau kemikali 250 ambazo zinajulikana kuwa sumu au kusababisha saratani.

Matumizi ya bidhaa za tumbaku/sigara zisizovutwa yanaweza kusababisha matatizo mabaya ya kiafya – na wakati mwingine yanayoweza kuua. Kupumua moshi kutoka kwa mvutaji kumedhihirishwa pia kusababisha hali hatari za kiafya, ikiwemo kifo. Bidhaa mpya zaidi za tumbaku/sigara zina kemikali sawia na bidhaa za zamani za tumbaku/sigara na zinadhuru afya.

Watu wanaovuta tumbaku/sigara kwa kipindi kirefu cha maisha yao hupoteza kwa wastani miaka isiyopungua 10 ya maisha. Ulimwenguni kote, zaidi ya watu 22000 hufa kila siku kutokana na matumizi ya tumbaku/sigara au kupumua moshi kutoka kwa wavutaji – mtu mmoja kila sekunde 4. Matumizi ya tumbaku/sigara huathiri takriban viungo vyote vya mwili wa binadamu. Baadhi ya athari za kiafya zimeonyeshwa hapa chini – kuanzia utosini hadi miguuni.

Magonjwa yanayosababishwa na aina zote za tumbaku/sigarakiharusi

Mshtuko wa moyo, kiharusi na magonjwa mengine yanayoathiri mfumo wa usambazaji wa damu na moyo

Takribani kifo kimoja kati ya vitatu hutokana na ugonjwa unaoathiri mfumo wa usambazaji wa damu na moyo. Matumizi ya tumbaku/sigara na kupumua moshi kutoka kwa wavutaji huchangia pakubwa, huku vikisababisha takriban vifo milioni 3 vinavyotokana na matatizo ya mfumo wa usambazaji wa damu na moyo kila mwaka.

Wavutaji tumbaku/sigara wana hatari mara mbili ya kiharusi na hatari iliyoongezeka mara nne ya ugonjwa wa moyo. Moshi wa tumbaku/sigara huharibu ateri za moyo, na kusababisha kukusanyika kwa ukoga na kuganda kwa damu, na hivyo kuzuia mtiririko wa damu na hatimaye kusababisha mishtuko ya moyo na kiharusi.

Kuzuiliwa kwa mtiririko wa damu, kukikosa kutibiwa, kunaweza kusababisha gangrini (kuoza kwa sehemu ya mwili) na kukatwa kwa sehemu zilizoathirika. Kiharusi, kama vile ugonjwa wa moyo, kina hatari kubwa ya kifo, na manusura wa kiharusi wanaweza kupatwa na hali mbaya za kulemaza, kama vile kupooza au kupoteza uwezo wa kuona au kuongea. Uvutaji sigara hudhuru, haijalishi unavuta mara ngapi.

Wale wanaovuta sigara moja tu kwa siku tayari wana nusu ya uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa moyo au kiharusi sawia na wale wanaovuta sigara 20 kwa siku. Hata hivyo, sio tu uvutaji wa tumbaku/sigara na kupumua moshi kutoka kwa wavutaji ndiko kunaweza kuongeza hatari ya ugonjwa unaoathiri mfumo wa usambazaji wa damu na moyo. Matumizi ya bidhaa za tumbaku/sigara zisizovutwa pia huongeza hatari ya kifo kutokana na mshtuko wa moyo au kiharusi.

Saratani ya mdomo na magonjwa mengine ya mdomo

Matumizi ya tumbaku/sigara (kwa kuvuta moshi au kutumia bila kuvuta) husababisha kiasi kikubwa cha magonjwa ya mdomo.  Aina zote mbili zinafahamika kwa kusababisha saratani ya mdomo. Katika nchi nyingi, uwezekano wa kuishi kwa zaidi ya miaka mitano baada ya kugunduliwa na saratani ya mdomo ni mdogo.

Wale wanaonusurika saratani ya mdomo aghalabu hupatwa na uharibifu mkubwa wa uso na hupoteza uwezo wa kuongea, kumeza au kutafuna. Matumizi ya tumbaku/sigara pia huongeza hatari ya ugonjwa wa ufizi, ambao ni ugonjwa wa kuvimba wa kudumu unaomaliza ufizi na kuharibu taya, na hatimaye kupelekea kung’oka kwa meno.

Kuvuta tumbaku/sigara na matumizi ya bidhaa za tumbaku/sigara zisizovutwa huvuruga kemikali za mdomo, huku kukisababisha kuzidi kwa ukoga na kubadilika kwa rangi ya meno kuwa ya manjano,  na kusababisha harufu mbaya.

Saratani ya koo

Saratani ya kooSaratani koo

Matumizi ya bidhaa za tumbaku/sigara zisizovutwa na uvutaji wa tumbaku/sigara huongeza hatari ya saratani ya kichwa na shingo, zikiwemo saratani za midomo, koo (koromeo na zoloto) na umio. Upasuaji wa kuondoa zoloto iliyoathiriwa na saratani unaweza kusababisha kuhitajika kwa upasuaji wa bomba la pumzi, kudungwa shimo kwenye shingo na bomba la pumzi ambalo humwezesha mgonjwa kupumua.

Mnunurisho na tibakemikali za saratani ya koo zina athari zinazodhuru na za kudhoofisha, ikiwemo kupoteza ladha, upungufu wa utoaji wa mate, na ongezeko la kamasi kwenye koo, ambalo humfanya mgonjwa kuhisi uchungu anapokula na wakati mwingine kushindwa kula kabisa.

Saratani nyingine

Matumizi ya tumbaku/sigara yanajulikana pia kusababisha zaidi ya aina 10 nyingine za saratani. Kwa kila mpumuo mmoja wa sigara, sumu na visababishi vya saratani huingizwa mwilini. Kati ya kemikali nyingi zinazopatikana kwenye moshi wa tumbaku/sigara, angalau 70 kati ya hizo zinajulikana kusababisha saratani.

Wavutaji sigara wana hatari kubwa zaidi ya kupatwa na saratani mbaya ya damu na uboho wa mifupa; saratani ya mianzi ya pua na mashimo yaliyojaa hewa yaliyo ndani ya pua; saratani ya rektamu na utumbo mpana, ya figo, ini, kongosho, tumbo au ovari; na saratani ya sehemu ya chini ya mrija wa mkojo (ikiwemo kibofu, mirija ya kusafirisha mkojo kutoka kwa figo hadi kwa kibofu na nyonga ya figo).

Kansa
Seli za kansa

Tafiti za hivi karibuni zimeonyesha pia kuna uhusiano kati ya uvutaji tumbaku/sigara na ongezeko la saratani ya matiti, hususan kwa wavutaji sugu na wanawake wanaoanza kuvuta sigara kabla ya mimba yao ya kwanza. Uvutaji sigara unajulikana pia kuongeza hatari ya saratani ya mlango wa uzazi kwa wanawake walioambukizwa ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na virusi vya human papillomavirus.

Hatari ya saratani hizi kwa kawaida huongezeka kadri uvutaji na mara ya kuvuta yanavyoongezeka, kwa sababu ya kuzidi kuingiza sumu na visababishi vya saratani mwilini. Tumbaku/sigara isiyovutwa ina visababishi 28 vya saratani ambavyo husababisha kansa ya mdomo, umio na kongosho.

Kuendelea kutumia tumbaku/sigara baada ya kugunduliwa kuwa na saratani hupunguza uwezekano wa kupona ugonjwa, kwa sababu toksini zilizoko kwenye moshi wa tumbaku/sigara zinaweza kubadilisha biolojia ya seli, jambo ambalo linaweza kusababisha kukua tena kwa uvimbe wa kansa; kuvuruga dawa za kutibu saratani; na kuongeza matatizo yanayohusiana na tiba.

Kifo cha kijusi

Matumizi ya tumbaku/sigara na kuhatarishwa na moshi wa tumbaku/sigara wakati wa ujauzito huongeza hatari ya kifo cha kijusi. Wanawake wanaovuta sigara au wanapumua moshi kutoka kwa wavutaji wanapokuwa wajawazito wana hatari kubwa ya mimba kutoka. K

uzaa watoto wakiwa tayari wamefariki (kuzaa vijusi waliofia ndani ya tumbo la uzazi) hutokea sana kwa sababu ya kijusi kukosa oksijeni na hitilafu za kondo zinazosababishwa na monoksaidi ya kaboni katika moshi wa tumbaku/sigara na nikotini iliyoko kwenye moshi wa tumbaku/sigara na tumbaku/sigara isiyovutwa.

Wavutaji sigara wana hatari kubwa zaidi ya kupata mimba isiyotungika ndani ya uterasi, hali mbaya sana inayoweza kusababisha kifo cha mama ambapo yai lililotungishwa mimba hujishikisha nje ya uterasi. Kwa hivyo, kuacha kuvuta sigara na kujikinga dhidi ya kupumua moshi kutoka kwa wavutaji hasa ni muhimu kwa wanawake wa umri wa kuzaa wanaopanga kuwa wajawazito na katika wakati wa ujauzito.

Kupungua kwa ukuaji wa kijusi, uzito mdogo wa mtoto wakati wa kuzaliwa na kuzaa mtoto kabla ya muda wa kuzaa kufika

Aina yoyote ya matumizi ya tumbaku/sigara au kuhatarishwa na moshi wa tumbaku/sigara wakati wa ujauzito kunaweza kudhuru ukuaji wa mtoto. Watoto wachanga wanaozaliwa na wanawake ambao huvuta sigara, hutumia tumbaku/sigara isiyovutwa, au hupumua moshi kutoka kwa wavutaji wakiwa wajawazito wana hatari kubwa ya kuzaa watoto kabla ya muda wa kawaida wa kuzaa na kuzaa watoto wenye uzito mdogo. Watoto wanaozaliwa kabla ya muda wa kawaida na wakiwa na uzito mdogo wanaweza kupatwa na matatizo katika maisha yao yote, ikiwemo kupatwa na magonjwa sugu wakiwa watu wazima.

Magonjwa yanayosababishwa na moshi wa tumbaku/sigara

Saratani ya mapafu

Wavutaji sigara wana uwezekano wa hadi mara 22 zaidi wa kupatwa na saratani ya mapafu maishani mwao kuliko wale wasiovuta sigara.

Uvutaji tumbaku/sigara ndicho kisababishi kikuu cha saratani ya mapafu, na husababisha zaidi ya thuluthi mbili ya vifo vinavyotokana na saratani ya mapafu duniani kote na huua watu karibu milioni 1.2 kila mwaka. Watu wasiovuta sigara ambao hupumua moshi kutoka kwa wavutaji nyumbani au kazini pia wako katika hatari ya kupatwa na saratani ya mapafu

Pumu

Uvutaji sigara unajulikana kufanya pumu kuwa mbaya zaidi kwa watu wazima, kuwazuilia kufanya shughuli zao, na kuchangia kupatwa na ulemavu na ongezeko la hatari ya pumu sugu inayohitaji huduma ya afya ya dharura. Watoto wa wazazi ambao huvuta sigara waliofikisha umri wa kwenda shuleni wako kwa hatari ya athari zinazodhuru za kupumua moshi kutoka kwa mvutaji na wako kwa hatari ya kupatwa na pumu na kufanya hali yao kuwa mbaya zaidi kupitia kuvimba kwa njia za kupeleka hewa kwenye mapafu.

Ugonjwa sugu wa kuziba/kufungana kwa njia za hewa

Mmoja kati ya wavutaji watano wa tumbaku/sigara atapatwa na ugonjwa sugu wa kufungana kwa njia za hewa (COPD) maishani mwao, hususani watu ambao huanza kuvuta sigara katika miaka yao ya utotoni na ujana, kwa sababu moshi wa tumbaku/sigara hupunguza ukuaji na unenepaji wa mapafu kwa kiwango kikubwa. Wavutaji sigara wana uwezekano wa mara 34 zaidi wa kupatwa na ugonjwa wa COPD wakilinganishwa na wale wasiovuta sigara.

Uvutaji tumbaku/sigara husababisha kuvimba na kupasuka kwa mifuko ya hewa kwenye mapafu na hivyo kupunguza uwezo wa mapafu wa kuingiza oksijeni na kutoa dioksidi ya kaboni. Pia husababisha kukusanyika kwa kamasi lililojaa usaha, hivyo kusababisha kikohozi chenye uchungu na kusumbuliwa na matatizo ya kupumua. Watu wazima ambao hupumua moshi kutoka kwa wavutaji sigara wakiwa watoto, na hivyo kuwafanya wapatwe na maambukizi ya mara kwa mara ya sehemu ya chini ya mfumo wa upumuaji, pia wana hatari ya kuugua ugonjwa wa COPD.

Kifua kikuu

Takriban robo moja ya watu wote ulimwenguni wana kifua kikuu kisicho na dalili zozote, na hivyo kuwafanya wawe katika hatari ya kuugua ugonjwa huo wenye dalili. Uvutaji tumbaku/sigara huongeza kwa zaidi ya mara dufu hatari ya kubadilika kwa ugonjwa wa kifua kikuu kutoka kwa hali isiyo na dalili hadi hali yenye dalili, na unajulikana pia kufanya hali asili ya kuendelea kwa ugonjwa kuwa mbaya zaidi. Aidha, kupumua moshi kutoka kwa mvutaji sigara kunaweza kuongeza hatari ya kubadilika kwa maambukizi ya kifua kikuu yakawa ugonjwa wenye dalili. Kifua kikuu huharibu mapafu, na kuongeza kupunguzwa kwa utendakazi wa mapafu kunakosababishwa na uvutaji, na huongeza hatari ya kiwango kikubwa cha ulemavu na kifo kutokana na kufeli kwa mfumo wa upumuaji.

Magonjwa mengine yanayoathiri mfumo wa upumuaji na upungufu wa utendakazi wa mapafu

Uvutaji wa tumbaku/sigara unajulikana kusababisha nimonia na dalili zote kuu za mfumo wa upumuaji, ikiwemo kukohoa, kukoroma na kohozi. Ukuaji na utendakazi wa mapafu pia zina uwezekano zaidi wa kulemazwa miongoni mwa wavutaji tumbaku/sigara. Watoto wa wazazi ambao huvuta sigara pia hupatwa na dalili sawia za mfumo wa upumuaji na viwango vya chini zaidi vya utendaji wa mapafu utotoni mwao. Watoto wachanga wanaozaliwa na kina mama ambao huvuta sigara wakiwa wajawazito wana hatari zaidi hasa, kwa sababu walihatarishwa kwa kemikali zinazopatikana kwenye tumbaku/sigara wakiwa katika hatua muhimu sana za ukuaji wakiwa wangali kwenye uterasi

Kisukari cha aina ya 2

Hatari ya kuugua kisukari iko juu zaidi kwa wavutaji sigara, na hatari hiyo huongezeka kadri idadi ya sigara zinazovutwa kila siku inavyoongezeka. Kuhatarishwa kutokana na kupumua moshi kutoka kwa wavutaji sigara kunahusishwa pia na kisukari cha aina ya 2.

Ugonjwa wa akili

Uvutaji sigara ni jambo linalosababisha hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kiakili, ambalo ni kundi la matatizo ambayo hupelekea kuzorota kwa akili na kwa sasa hakuna dawa au tiba inayoweza kuuponya. Ugonjwa wa kuzorota kwa akili mara nyingi huendelea kuwa mbaya, na kuathiri uwezo wa kukumbuka, tabia na uwezo mwingine wa kiakili na kutatiza shughuli za kila siku.

Kando na kuchangia katika kiwango kikubwa cha ulemavu kwa mtu anayeugua ugonjwa wa kuzorota kwa akili, ugonjwa huu unaweza kuathiri pakubwa hisia za familia ya mgonjwa na wanaomtunza. Ugonjwa wa Alzheimer ndio aina ya ugonjwa wa kuzorota akili ambao watu wengi zaidi huugua, na inakadiriwa kuwa 14% ya visa vyote ulimwenguni vya ugonjwa wa Alzheimer husababishwa na uvutaji sigara.

Upungufu wa uwezo wa kuzalisha na kuzaa miongoni mwa wanaume na wanawake

Wavutaji sigara wana uwezekano mkubwa wa kuwa na utasa au ugumba. Wanawake wanaovuta sigara wana uwezekano zaidi wa kukumbwa na matatizo ya kupata mimba, kuongezeka kwa muda kabla ya kupata mimba na ongezeko la hatari ya mimba kutoka, wakilinganishwa na wale wasiovuta sigara.

Uvutaji sigara pia hupunguza idadi, uwezo wa kusonga na muundo (umbo la mbegu ya kiume) wa mbegu za kiume miongoni mwa wanaume. Wavutaji sigara wanaojaribu kupata mimba kwa kutumia teknolojia ya kusaidia kutungisha mimba huwa na viwango vya chini zaidi vya ufanisi, na wakati mwingine huhitaji mizunguko mara dufu ya kutungisha mimba nje ya mfuko wa uzazi ili kupata mimba.

Kupungua kwa uwezo wa kusimamisha uume

Uvutaji sigara huzuilia damu isisambae kwenye uume, jambo ambalo linaweza kusababisha uhanithi (kukosa uwezo wa kusimika uume). Ukosefu wa uwezo wa kusimika uume huwapata sana wavutaji sigara na uwezekano mkubwa wa kuendelea au kudumu isipokuwa iwapo mwanaume ataacha kuvuta sigara mapema maishani.

Ugonjwa wa kifo cha ghafla cha watoto wachanga

Ugonjwa wa kifo cha ghafla cha watoto wachanga (SIDS) ni kifo cha ghafla, bila sababu cha mtoto mwenye umri wa chini ya mwaka 1.  Uvutaji sigara wakati wa ujauzito unajulikana kuongeza hatari ya ugonjwa wa SIDS, na hatari hiyo huongezeka zaidi miongoni mwa uzao wa wazazi ambao huendelea kuvuta sigara baada ya kuzaliwa kwa mtoto.

Hedhi na kukoma kwa hedhi

Wanawake wanaovuta sigara wana uwezekano mkubwa wa kupatwa na hedhi yenye maumivu na dalili sugu za kipindi cha kukoma kwa hedhi. Kukoma kwa hedhi hutokea miaka 1-4 mapema kwa wanawake wanaovuta sigara kwa sababu uvutaji sigara hupunguza utoaji wa mayai kwenye ovari, na kupelekea kupotea kwa uwezo wa uzazi na baadaye viwango vidogo vya estrojeni.

Kasoro za watoto wanaozaliwa

Uvutaji sigara unaweza kubadilisha umbo la mbegu ya uume na kuharibu DNA yake, na hili huenda likasababisha kasoro za watoto wanaozaliwa. Baadhi ya tafiti zimepata kuwa wanaume ambao huvuta sigara wana hatari kubwa ya kuzalisha mtoto ambaye atapatwa na saratani. Mwanamke mjamzito anayevuta sigara wakati wa kipindi cha awali cha ujauzito huongeza uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na mdomo na/au kaakaa iliyopasuka. Imetambuliwa kuwa wanaume ambao kina mama wao walivuta sigara wakiwa wajawazito wana mbegu za kiume zenye uzito mdogo wakilinganishwa na kina mama ambao hawajawahi kuvuta sigara.

Kupotea kwa uwezo wa kuona

Uvutaji sigara husababisha magonjwa mengi ya macho ambao, yakiachwa bila kutibiwa, yanaweza kupelekea kupotea kwa kudumu kwa uwezo wa kuona. Wavutaji sigara wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupatwa na tatizo la kudhoofika kwa eneo la retina lenye uwezo wa kuona kwa uwazi, hali ambayo hupelekea kupotea kwa uwezo wa kuona kusikoweza kutibiwa.

Kuharibika kwa doa la retina huathiri uwezo wa kusoma, kuendesha gari, kutambua nyuso na rangi na kuona vitu kwa uwazi zaidi. Wavutaji sigara pia wana hatari ya juu ya kupatwa na ugonjwa unaothiri watoto wa jicho, ambao huziba lenzi za jicho na kuzuilia mwangaza. Kuzibwa kwa lenzi za macho husababisha ulemavu wa kuona, na upasuaji ndilo suluhu pekee la kurejesha uwezo wa kuona.

Ushahidi mpya unaonyesha kuwa uvutaji sigara pia husababisha glakoma, hali ambayo huongeza shinikizo kwenye jicho na kuharibu uwezo wa kuona kwa macho. Moshi wa tumbaku/sigara huwasha macho na hufanya tatizo la kukauka macho kuwa baya zaidi kwa wavutaji sigara na wale walio karibu ambao hupumua moshi kutoka kwa mvutaji, hususan wale wanaovaa lenzi kwa macho.

Kupoteza uwezo wa kusikia

Kuvuta sigara miongoni mwa wazazi kunajulikana kusababisha ugonjwa wa sikio la kati miongoni mwa watoto walio na umri chini ya miaka 2 ambao hupumua moshi kutoka kwa mvutaji nyumbani. Kutoboka kwa kiwambo cha sikio (ugonjwa wa sikio la kati) miongoni mwa watoto ni kisababishi kikuu cha kupotea kwa uwezo wa kusikia na uziwi.

Wavutaji sigara ambao ni watu wazima wana uwezekano mkubwa wa kupoteza uwezo wa kusikia kwa sababu ya athari za kuvuta sigara kwa muda mrefu kwa usambazaji wa damu kwenye komboli. Kupoteza uwezo wa kusikia na uziwi ambao haujatibiwa unaweza kuleta madhara makubwa ya kijamii, kihisia na kiuchumi.

Magonjwa ya tumbo

Wavutaji sigara wana uwezekano wa kupatwa na matatizo ya tumbo, kama vile vidonda vya tumbo, ugonjwa wa kuvimba kwa mfumo wa mmeng’enyo, kama vile ugonjwa wa Crohn, na saratani za tumbo. Ugonjwa wa kuvimba kwa mfumo wa mmeng’enyo aghalabu huhusishwa na maumivu ya tumbo, kuhara kusikoisha, homa na kuvuja damu kwa rektamu

Kudhoofika kwa mfumo wa kinga

Chembe za moshi wa tumbaku/sigara hudhoofisha mfumo wa kinga, na kuwafanya wavutaji sigara wawe katika hatari ya maambukizo ya mfumo wa upumuaji. Aidha, wavutaji sigara wenye hali ya kijeni inayowafanya wawe rahisi kupatwa na matatizo ya mfumo wa kinga unaoufanya ushambulie mwili wa mwathiriwa, wako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa kadhaa, ikiwemo ugonjwa wa baridi-yabisi, ugonjwa wa Crohn, homa ya uti wa mgongo inayosababishwa na maambukizo ya bakteria, maambukizo baada ya upasuaji, na saratani.

Uvutaji sigara pia huongeza hatari ya kuugua magojwa yanayohusiana na ugonjwa mkuu anaougua mtu na kifo cha mapema kwa watu ambao wana mfumo wa kinga ulio hatarini, kama vile watu wanaougua ugonjwa unaofanya viungo vikuu kuzibwa na kamasi, ugonjwa wa mfumo wa neva au saratani.

Athari za tumbaku/sigara za kudhoofisha mfumo wa kinga huwaweka watu wanaougua VVU katika hatari kubwa ya kupatwa na Ukimwi. Miongoni mwa wavutaji sigara walio na VVU, wastani ya kiasi cha maisha yanayopotezwa ni miaka 12.3, zaidi ya mara dufu ya idadi ya miaka ambayo watu wenye VVU na wasiovuta sigara hupoteza.

Mifupa dhaifu

Monoksaidi ya kaboni, gesi kuu yenye sumu ambayo huwa kwenye moshi unaotolewa na magari na moshi wa tumbaku/sigara, hujiunganisha kwa hemoglobini ya damu kwa urahisi kuliko oksijeni, hivyo kupunguza kiasi cha oksijeni kinachopelekwa kwa viungo vya mwili. Wavutaji sigara wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupoteza uzito wa mfupa, huvunjika mifupa kwa urahisi na hupatwa na matatizo mabaya, kama vile kuchukua muda mrefu kabla ya kupona au kukosa kupona kabisa.

Uharibifu wa ngozi

Uvutaji tumbaku/sigara huongeza hatari ya kuugua ugonjwa wa kubambuka ngozi , ugonjwa wa kuvimba kwa ngazi usioambukizwa ambao huacha madoa mekundu yanayowasha mwilini kote. Uvutaji sigara huifanya ngozi kuzeeka kwa haraka kwa kuzeesha proteni zinazoifanya ngozi iumbuke kwa urahisi, kuzinyima vitamini A na kuzuilia kutiririka kwa damu. Wavutaji sigara wana uwezekano mkubwa wa kupata ngozi kavu, ngumu na yenye mikunjo , hususan kwenye midomo na macho.

Hitimisho

Aina zote za tumbaku/sigara hudhuru, na hakuna kiwango salama cha matumizi ya tumbaku/sigara. Uvutaji tumbaku/sigara ndio aina kuu ya matumizi ya tumbaku/sigara ulimwenguni kote. Bidhaa nyingine za tumbaku/sigara ni pamoja na bidis, sigara za karafuu, biri, sigara inayokunjwa na matawi ya tumbaku/sigara, bidhaa tofauti za tumbaku/sigara zisizovutwa, tumbaku/sigara yakujikunjia mwenyewe, kiko, buruma na bidhaa nyingine mpya za tumbaku/sigara.

Muda wa kuacha kuvuta sigara haujaisha. Kuacha kuvuta sigara kuna uwezo wa kupunguza pakubwa hatari ya magonjwa haya mengi na, katika hali zingine, kupunguza hatari kwa mtu ambaye hajawahi kuvuta sigara.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/smoking.html#:~:text=Remember%2C%20there%20is%20no%20safe,quit%2C%20the%20greater%20the%20benefit.

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *