Magonjwa sugu ya njia ya hewa

Aina za magonjwa sugu ya njia ya hewa ni pamoja na ugonjwa wa pumu, saratani ya mapafu, na mengine yanasababishwa na kemikali zinazotoka katika viwanda vinavyochafua mazingira kwa mfano kiwanda cha saruji, pamba na sigara.

Mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa sugu ya mfumo wa hewa

Magonjwa sugu ya njia ya hewa mara nyingi husababishwa na kuharibika kwa njia za hewa katika mapafu kunakoweza kutokana na: ­

  • Kuvuta sigara, au kukaa karibu na mtu anayevuta sigara; ­
  • Uchafuzi wa hewa ya ndani na nje, kutokana na aina ya vumbi au chavua ya maua; ­
  • Hewa za sumu na vumbi toka viwandani; ­
  • Unene uliokithiri ­ Mara nyingine magonjwa sugu ya njia ya hewa huweza kurithiwa mfano pumu.

Ushauri wa lishe na ulaji kwa mgonjwa mwenye magonjwa sugu ya njia ya hewa ­

Endapo una ugonjwa sugu wa njia ya hewa ni vyema kuzingatia ushauri wa mtaalam wa afya, matibabu na kufuata kanuni za mtindo bora wa maisha; ­

  • Unashauriwa kula mlo kamili na vyakula vya aina mbalimbali ili upate virutubishi vyote vinavyohitajika kwa afya yako; ­
  • Kula matunda freshi, mbogamboga zenye rangi ya kijani, mbogamboga na matunda yenye rangi ya njano ili kuimarisha kinga ya mwili wako; ­
  • Unashauriwa pia kula vyakula vyenye makapi mlo kwa wingi ili kusaidia mfumo wa kusaga chakula kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa uchafu tumboni kwa urahisi. Hali hii husaidia kuweza kupumua kwa urahisi; ­
  • Ni vizuri kula milo midogo midogo mara kwa mara; ­
  • Punguza matumizi ya chumvi ili kuepuka maji kujikusanya mwilini na kusababisha kupumua kwa shida; ­
  • Ni muhimu pia kuepuka uzito uliozidi au unene kwani huongeza tatizo la kupumua; ­
  • Zingatia kuwa na uzito unaofaa kwa kula chakula cha kutosha. Mara nyingi mtu mwenye magonjwa sugu ya njia ya hewa huweza kupungua uzito kwa sababu inamlazimu kutumia nguvu (nishati–lishe) kwa kiasi kikubwa wakati wa kupumua. Matumizi makubwa ya nguvu husababisha asiwe na nishatilishe ya akiba ambayo huhifadhiwa mwilini na kufanya mtu huyo kuwa mwembamba.
  • Mgonjwa huyo anashauriwa: ­
    • Kuepuka visababishi na vichochezi kama vile vumbi, kuvuta sigara, chavua, hasira, pombe na harufu; ­
    • Kuhakikisha mazingira na nyumba yake ni safi na pia iwe na madirisha yanayoruhusu mzunguko wa hewa.

Jinsi ya kuzuia magonjwa sugu ya mfumo wahewa ­magonjwa sugu ya njia ya hewa

  • Epuka kuvuta sigara ­
  • Epuka kukaa na mtu anayevuta sigara kwa kuzuia mtu kuvuta sigara nyumbani na ofisini. Inapaswa pia kuzuia uvutaji sigara kwenye maeneo ya watu kama hoteli, vituo vya usafiri, kwenye vyombo vya usafiri, hospitali, shuleni, vyuoni, ofisini, sokoni nk. Weka vibao vya ” usivute sigara” katika sehemu zenye mikusanyiko ya watu wengi viwekwe. ­
  • Epuka kuchafua mazingira hasa hewa tunayovuta. Uchafuzi wa hewa ndani na nje ya nyumba hudhibitiwa kwa kufanya yafuatayo:

Nje ya nyumba: –

  • Usiwashe gari na kuiacha kwa muda mrefu bila kuizima kama haitumiki
  • Epuka kutumia dawa ya kuuwa wadudu shambani na kemikali nyingine kuwepo karibu na nyumba yako hasa sehemu za bustani na zile za kukaa watu

Ndani ya nyumba: –

  • Dhibiti hali ya unyevunyevu hasa jikoni, chooni na bafuni. Hakikisha sakafu, sinki na meza ni safi na kavu;
  • Hakikisha vifaa kama kiyoyozi, feni, heater vinasafishwa mara kwa mara;
  • Dhibiti vumbi na manyoya ya wanyama kama paka kwa kusafisha kikamilifu sehemu kama sakafu, kabati, magodoro, makochi, mito. Utitiri na viroboto hukua na kuzaliana kwenye magodoro, makochi, mito na matandiko ambayo hayapitishi hewa ya kutosha. Shuka na blangeti zifuliwe na maji ya moto na mazulia yasafishwe mara kwa mara na yawe makavu ili kuua wadudu.
  • Hakikisha madirisha ni mapana kuweza kupitisha hewa ya kutosha na yafunguliwe kila siku kupitisha hewa; na
  • Hakikisha nyumba ipo wazi (milango na madirisha) wakati wa kufanya usafi, kupaka rangi au shughuli nyingine kubwa.

Jikinge na kuvuta hewa zenye kemikali. Watu wanaofanya kazi ya kujenga, migodini na viwandani wako katika hatari zaidi ya kupata magonjwa sugu ya njia ya hewa kama saratani ya mapafu, pumu na mengineyo. Watu hawa wanashauriwa kuvaa vifaa rasmi vya kuzuia kuvuta hewa chafu kama kitambaa au kichuja hewa

Vyanzo

https://www.tfnc.go.tz/publications/9

 

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *