Magonjwa ya ngono ni nini?
Magonjwa ya ngono – ni maambukizi ya magonjwa yanayoenezwa kwa kufanya ngono isiyo salama. Endapo utafanya ngono ya ukeni, mk*nduni, au kwa kulamba sehemu za uke bila ya kutumia kinga (kondomu) uko hatarini kuambukizwa magonjwa yatokanayo na ngono. Magonjwa ambayo ni ya kawaida ni pamoja na UKIMWI, kisonono, malengelenge na kaswende.
Mtu yeyote anaweza kupata magonjwa ya ngono hata kama umefanya ngono mara moja. Haihitajiki uwe na washirika wengi ili upate magonjwa hayo.
Nitatambuaje kuwa nina magonjwa ya ngono?
Ni muhimu kujua viashiria vya magonjwa ya kawaida yatokanayo na ngono. Ukitambua moja ya viashiria vifuatavyo, ni vyema kwenda kituo cha afya ukapimwe, na utibiwe:
- Kutokwa na majimaji yasiyo ya kawaida, yenye rangi njano, au kijani mpauko, ukeni, au kwenye uume (yaweza yakawa yanawasha, au kutoa harufu)
- Maumivu au kuwaka wakati wa kutoa mkojo
- Kujisikia kukojoa mara kwa mara
- Maumivu chini ya kitovu (kinena)
- Vidonda, vipele, malengelenge, uvimbe, kusunguka mboo, uke, au mk*ndu
- Kuwashwa, malengelenge, na maumivu katika sehemu za siri
- Uvimbe unaouma, kwenye uke, mapumbu au uume
- Maumivu wakati wa kufanya ngono
- Kutokwa damu wakati au baada ya kitendo cha ngono
- Hedhi zisizo na mpangilio
- Kwa wanawake, homa kali na viashiria vilivyotajwa na hasa maumivu makali chini ya kitovu, ni jambo baya sana
Huwezi kumtambua mtu mwenye magonjwa yatokanayo na ngono kwa kumtazama tu, kwa vile magonjwa mengine yatokanayo na ngono kama vile Chlamydia hayana viashiria vya wazi. Kwa hiyo, wewe na mwenzi wako mnaweza mkawa na magonjwa yatokanayo na ngono bila kujitambua. Ndio maana ni muhimu kupimwa mara kwa mara ikiwa unafanya ngono bila ya kutumia kinga kondomu.
Ninawezaje kujikinga na magonjwa ya ngono
- Tumia kondomu kwa usahihi kila mara ufanyapo ngono. Hi inakupunguzia hatari ya kupata, au kusambaza magonjwa yatokanayo na ngono. Lakini endapo mwenza wako ana malengelenge, vipele au vidonda katika sehemu zake za siri ambavyo havijafunikwa na kondomu, basi utakuwa huna kinga.
- Nenda ukapime mara kwa mara. Hata kama umekuwa na mwenza wako kwa muda mrefu, ni vyema kwenda kupima, ili mradi muwe salama.
- Usitegemee mitishamba au waganga wa kienyeji. Hawatibu magonjwa yatokanayo na ngono. Na endapo unaishi na Virusi vya UKIMWI, itasababisha tiba yako kushindwa kufanya kazi.
Kwanini nipime ?
Usipopima, huwezi ukapatiwa tiba ya haraka. Magojwa mengine ya Ngono yasipopatiwa tiba kwa muda mrefu, yanaweza kupelekea kutoweza kupata mtoto tena. Kuishi na magojwa ya ngono kunakuweka katika hatari zaidi ya kupata VVU.
Habari njema ni kuwa magonjwa ya ngono mengi yanatibika kwa urahisi. Magonjwa mengine ya ngono kama vile vidonda sehemu za siri na VVU,hayatibiki, lakini dalili zinaweza kupunguzwa. Ukipima na kugundulika una maambukizi ya VVU, Ukafata tiba ipasavyo, inamaana una maisha marefu yenye afya mbele yako.
Niende wapi kupata matibabu ya magonjwa ya ngono?
Ni kawaida kujisikia woga kupima lakina hakuja haja ya kuona aibu. Unaweza kwenda kwenye kituo chochote cha afya kilicho karibu ukapimwa, ambako una haki, heshima na usiri wa tiba. Pia una haki ya kutohukumiwa.
Endapo una mwenza wako wa kila mara, unaweza kwenda naye kliniki, maana huenda wote mkahitaji kutibiwa. Endapo wewe pekee ndio umetibiwa, halafu wewe na mwenzi wako mnafanya ngono bila kinga, kuna uwezekano mkubwa wewe kupata tena maambukizi. Bali kama huna mwenza wa kila mara, ni vyema mshirika huyu wa sasa akapimwa pia.
- Unafanya jambo jema: Kuwajibika juu ya afya yako, na afya ya wengine