Maelezo ya jumla

Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea wanaoambukizwa na mbu aina ya anofelesi. Dalili za awali za ugonjwa huu ni pamoja na: uchovu, homa, kuhisi baridi, kutokwa jasho, maumivu ya kichwa, kichefuchefu na kutapika. Dalili zinazofuta zinaweza kuwa mbaya na hata kutishia maisha ya mgonjwa. Mgonjwa huanza kupata shida kupumua, kuchanganyikiwa, na hatimaye koma. Kuna aina tano za vimelea wanaoweza kusababisha ugonjwa huu, Plasmodium falciparum, P. vivax, P. oval, P. malariae, na P. knowlesi. Mtu yeyote anaweza kuambukizwa ugonjwa wa maleria.
Hata hivyo, watu fulani wako kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa, hii ni pamoja na wanaoishi katika nchi zenye malaria kwa wingi mf: nchi zilizo katika ukanda wa kitropiki kama Tanzania, Kenya na Uganda. Ugonjwa huu unaweza kutambuliwa kwa kuangalia dalili na vipimo vya maabara, kama vile darubini au vipimo vya kutambua antijeni. Malaaria inaweza kutibiwa kwa muunganiko wa madawa kadhaa (kila nchi inao muunganiko maalumu unaokubalika na kuaminika). Watu wanaosafiri kwenda katika nchi zenye kiwango kikubwa cha malaria wanapaswa kutumia dawa za kujikinga na kuchukua hatua kujikinga dhidi ya mbu. Mfano; kwa kutumia dawa za kufukuza mbu (mosquito repellents) na kuvaa nguo za kufunika mikono na miguu. Kesi nyingi za malaria hupona vyema bila matatizo baada ya kutibiwa vyema.

Nini dalili za Malaria?

Dalili za kawaida za ugonjwa huu ni pamoja na:

Baada ya kuumwa na mbu aina ya anofelesi mwenye vimelea vya malaria, muda kidogo hupita kabla ya dalili za kwanza kuonekana. Kwa kesi nyingi dalili za kwanza huonekana siku 7 hadi 30 baada ya kuumwa na mbu.

Ni nini kinachosababisha Malaria?

Ugonjwa huu husababishwa na vimelea wanaoenezwa na aina fulani ya mbu wanaokunywa damu ya mwanadamu. Ugonjwa huu huenezwa toka kwa mtu mmoja mpaka mwingine kwa kuumwa na mbu aina ya anofelesi.
Kuna aina nne za vimelea vinavyoweza kusababisha malaria kwa mawanasamu:

  • Plasmodium falciparum
  • vivax
  • ovale
  • malariae
  • knowlesi – hii ni aina ya vimelea wa malaria iliyogunduliwa hivi karibuni, inayosababisha maambukizi kwa nyani (macaque) na wandamu huko Asia kusini. Aina hii ya malaria inaweza kuhama toka kwa wanyama na kuwaambukiza wanadamu (zoonotic malaria).

Malaria inayotokana na ”falciparum” huwa inaathiri kiasi kikubwa cha chembe nyekundu za damu kuliko aina nyingine, na kwa sababu hii inaifanya aina hii ya malaria kuwa na matokeo mabaya na inaweza kusababisha kifo masaa machache tu baada ya kuanza kwa dalili za awali.
Malaria inaweza pia kuambukizwa kwa njia zifuatazo

  • Mtoto aliye tumboni kwa mama anaweza kuambukizwa vimelea vya malaria akiwa tumboni
  • Utaambukizwa malaria ukiongezewa damu yenye vimelea vya maleria.

Nani aliye kwenye hatari zaidi ya kupata malaria?

  • Mtu yeyote anaweza kuambukizwa ugonjwa huu.
  • Matukio mengi ya ugonjwa huu hutokea kwa watu wanaoishi katika nchi zenye kiwango kikubwa cha uambukizo wa malaria
  • Watu wasioishi kwenye nchi zenye uambukizo mkubwa wa ugonjwa huu wanaweza kuambukizwa wakisafiri kwenda kwenye nchi zenye uambukizo mkubwa au kwa kuongezewa damu.
  • Mtoto anaweza kuambukizwa malaria toka kwa mama kabla au wakati wa kujifungua.

Ni nani aliye katika hatari zaidi ya Kufa kwa Malaria?

  • Watu wanaoumwa na mbu wengi ambao wameambukizwa vimelea vya falciparum (vimelea hawa husababisha ugonjwa mkali na hatari) wako katika hatari kubwa ya kufa.
  • Watu wanaoishi katika nchi Afrika zilizo kusini mwa jangwa la sahara – vimelea aina ya falciparum ni kawaida
  • Watu wasio na kingamwili ya kutosha kupambana na malaria, kama vile watoto wadogo, wanawake wajawazito, na wasafiri wanaotoka katika maeneo yasio na uambukizo mkubwa wa maleria.
  • Watu masikini, wanaoishi vijijini na wasio na uwezo wa kuzifikia huduma za afya

Wakati gani utafute matibabu unapokuwa na malaria?

Unapaswa kutafuta huduma ya matibabu haraka kama:

  • Kama unaanza kuona dalili na unaishi katika maeneo yenye uambukizo mkubwa mf; Tanzania, Kenya, Uganda.
  • Unaona dalili za malaria ukiwa safarini katika nchi yenye uambukizo mkubwa.
  • Unaona dalili za malaria baada ya kutembelea eneo lenye uambukizo mkubwa malaria (hata baada ya mwaka mzima baada ya kurejea nyumbani)

Utambuzi wa ugonjwa wa malaria

Uchunguzi hutegemea dalili za mgonjwa na matokeo ya uchunguzi wa mwili. Dalili za awali za malaria zinafanana na magonjwa mengine (mfano: “mafua” na maambukizi mengine ya virusi).
Kwa malaria kali, Ishara zake huwa kali na kusababisha utambuzi kuwa rahisi. Ishara hizi ni pamoja na:

Ishara hizi zinapaswa kuthibitishwa kwa kufanya kipimo. Vipimo vya malaria ni pamoja na:

  • Uchunguzi kwa kutumia darubini
  • Kugundua antijeni
  • Serolojia

Mbali na vipimo vilivyotajwa hapo juu, daktari anaweza kuagiza vipimo vifuatavyo ili kuangalia hali ya mwili wako.

  • Complete blood count
  • Routine chemistry panel

Kama umepimwa na kugundulika kuwa una malaria, daktari anaweza kuagiza vipimo vya ziada ili kutambua kama ugonjwa wako ni mkali au la?. Vipimo hivi huchunguza kama kuna:

  • Upungufu mkubwa wa damu
  • Kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu
  • Kushindwa kwa figo kufanya kazi
  • Kiwango kikubwa cha ”bilirubin” kwenye damu- hii huashiria kuwa malaria inavunja na kuziharibu seli nyekundu za damu kwa wingi na kwa kasi sana

Uchaguzi wa matibabu ya malaria

Malaria ni ugonjwa mkali na unaweza kuua (hasa kama umesababishwa na Plasmodium falciparum). Matibabu yake yanapaswa kuanzishwa haraka iwezekanavyo.
Matibabu ya ugonjwa huu yanategemea mambo mengi ikiwa ni pamoja na:

  • Ukali wa ugonjwa
  • Aina ya vimelea vya malaria vilivyosababisha ugonjwa

Wagonjwa ambao wana malaria kali ya P. falciparum, au ambao hawawezi kumeza dawa, wanapaswa kutibiwa kwa sindano.
Kuna dawa nyingi zinazotumika kutibu malaria katika pembe zote za dunia

  • Chloroquine
  • Atovaquone-proguanil
  • Artemether-lumefantrine– ALU
  • Mefloquine
  • Quinine
  • Quinidine
  • Doxycycline (hutumiwa pamoja na quinine)
  • Clindamycin (hutumiwa pamoja na quinine)

Uchaguzi wa dawa utakayotumia unategemea mahali ulipo. Daktari wako atakuchagulia dawa inatakayokufaa kwa kufuata miongozo ya kutibu malaria iliyotolewa na wizara husika.
Pamoja na kutumia dawa mgonjwa atapaswa kupewa huduma nyingine za kitabibu ili kupata nafuu. Atahitaji kuongezewa damu kama imepungua, ataongezewa maji mwilini kama amepungukiwa maji baada ya kutapika sana, anaweza pia kuhutaji kuwekwa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua kama anapata shida kupumua n.k.

Kuzuia

  • Watu wengi wanaoishi katika maeneo yenye uambukizo mkubwa wa malaria kama vile Tanzania hutengeneza kingamwili (usugu) dhidhi ya ugonjwa huu  na kwa sababu hiyo hawaugui mara kwa mara.
  • Wageni, wasio na kinga yoyote, wanapaswa kutumia dawa za kujikinga wakitembelea eneo lenye uambukizo mkubwa. Ni muhimu kumwona mtoa huduma ya afya mapema kabla ya kusafiri, matibabu yanaweza kuanza wiki 2 kabla ya safari na kuendelea mpaka mwezi mmoja baada ya kurejea kutoka katika eneo hilo.
  • Dawa zinazotumiwa na wasafiri wanaoelekea Marekani ya kusini, Afrika, Asia, India, na Pasifiki ya Kusini ili kujikinga ni pamoja na:
    • Mefloquine
    • Doxycycline
    • Chloroquine
    • Hydroxychloroquine
    • Malarone- Atovaquone / Proguanil
  • Wanawake wajawazito wanapaswa kutumia dawa za kujikinga dhidi ya malaria – hii hupunguza uwezekano wa mtoto kuambukizwa akiwa tumboni
  • Watu wanaotumia dawa za kutibu malaria wanaweza kuambukizwa tena malaria. Jikinge dhidi ya mbu kwa kuvaa nguo zinazofunika miguu na mikono, tumia dawa za kufukuza mbu, lala chini ya chandarua, weka skrini kwenye madirisha yako na tumia dawa ya mbu.
  • Kwa miaka mingi Chloroquine imekuwa ikitumiwa kama dawa ya kujikinga dhidi ya malaria. Lakini kwa sababu ya kuongezeka usugu dhidi ya dawa hii , kwa sasa inashauriwa kutumika kukinga malaria katika maeneo yenye ugonjwa unaosababishwa na Plasmodium vivax, P. oval, na malariae pekee.
  • Kwa wasafiri (wageni) wanaosafiri kwenda maeneo yenye malaria inayosababishwa na falciparum, wanaweza kutumia moja ya zifuatazo ili kujikinga:
    • Mefloquine
    • Atovaquone / Proguanil -malarone
    • Doxycycline

malariaNini cha kutarajia?

Mara nyingi, Ugonjwa malaria hupona kama matibabu sahihi yatatolewa haraka na kwa wakati.
Matarajio huwa si mazuri sana kwa malaria kali inayosababishwa na falciparum.

Matatizo yanayoweza kutokea

Matatizo mbalimbali yanaweza kusababishwa na ugonjwa mkali. Malaria kali husababisha baadhi ya viungo mwilini kushindwa kufanya kazi, husababisha uharibifu wa damu ya mgonjwa na kuvuruga  mfumo wa kimetaboliki. Ishara za ugonjwa mkali wa malaria ni pamoja na;

  • Malaria kupanda kichwani
  • uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo- meningitis
  • Upungufu mkubwa wa damu 
  • Kushindwa kupumua kunakotokana na mapafu kujaa maji
  • Kuvuja damu ovyo kunakotokana na damu kushindwa kuganda
  • Kushindwa kwa moyo kufanya kazi
  • Kushindwa kwa figo kufanya kazi
  • Kushindwa kwa ini kufanya
  • Kupasuka kwa wengu kunakosabaisha damu kuvujia ndani ya mwili

MAELEZO YA ZIADA KUHUSU UGONJWA WA MALARIA

Maelezo ya jumla

Ni maambukizi ya damu yanayosababishwa na protozoa anayeitwa plasmodium

Sababu

  • Plasmodium falciparum – Inavamia seli nyekundu za umri wote
  • Plasmodium vivax – inavamia seli nyekundu kabla hazijakomaa – reticulocytes
  • Plasmodium ovale – inavamia seli nyekundu kabla hazijakomaa – reticulocytes
  • Plasmodium ovale – Inavamia seli nyekundu Kabla hazijakomm – reticulocytes

Epidemiolojia

Unapatikana zaidi katika maeneo ya kitropiki duniani. Unaathiri 40% ya watu wote duniani. Watoto walio chini ya mika 5, wajawazito na wasafiri wako kwenye hatari zaidi. Plasmodium falciparum 60% na vivax 40% hupatikana Tanzania.

Uambukizo

  • Kwa kuumwa na mbu wa kike aina ya anopheles mwenye maambukizi, amabaye ananyonya damu ya mwandamu ili kukuza mayai yake.
  • Kuongezewa damu, kuwekewa kiungo na kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto akiwa tumboni

Muda kabla dalili kuanza

Inategemea umeambukizwa aina gani ya plasmodium

  • Plasmodium falciparum siku 7-14
  • Plasmodium virvax siku 8-14
  • Plasmodium ovale siku 8-14
  • Plasmodium malariae siku 7-30

Muda wa uambukizo

Mbu wanaendelea kuwa na uwezo wa kuambukiza kama bado watanyonya damu ya wagonjwa wenye mayai ya vimelea vya kwenye damu. Mbu wakishambukizwa vimelea vya malaria, wanabakia na uwezo wa kuambukiza katika kipindi chote cha maisha yao.

Nani yuko kwenye hatari

kila mtu yuko kwenye hatari ya kuambukizwa isipokuwa kwa baadhi ya watu wenye hali maalumu

  1. Hali maalumu zisizoeleweka vizuri
    • Watu wenye tabia ya selimundu (sickle cell traits)
    • Kwa sababu ya kinga inayotoka kwa mama watoto wachanga wanakingwa siku za mwanzo za maisha yao
    • Kuwa na joto kali sana la mwili – husemekana kuwa linauwa vimelea vimwilini
    • Uwezo wa wengu kuondoa seli zenye maambukizi haraka – splenic clearance reaction
  1. Hali maalumu zinazoeleweka
    • Kupata kinga ya mwili, baada ya kupata maambukizi ya ina fulani ya plasmodium mara nyingi

Namna ya uambukizo – life cycle

  1. Buu wanaitwa sprozoites wanainguzwa kwenye mshipa ya mtu anapokuwa ananyonya damu
  2. Buu hawa wanavamia seli za ini kama mbegu zinazoota na kuongezeka ukubwa kutengeneza schizonts
  3. Schizonts baada ya muda zinapasuka na kutoa mabuu wengine wengi kwa jina merozoites ambao wanasambaa na kuvamia seli nyekundu za damu
  4. Baadhi ya hizi meroziotes zinakuwa na kutengeneza mayai yanayoitwa gametocytes
  5. Mayi ya gametocytes yanaendela kuzunguka mwilini mpaka mbu anapkuja kunya damu na kuyachukua
  6. Kwenye tumbo la mbu, yai la kiume na kike yanaungana kutengeneza kijusi ambacho kinakuwa kutengeneza oocyst ambayo ikipasuka inatoa mabuu – sporotoites
  7. Mabuu wa sporozoites wanasafiri mpaka mdomoni mwa mbu tayari kuambukiza watu

Dalili

Homa, kutetemeka, maumivu ya kichwa, kuharisha, kuona vitu au kusikia sauti ambazo hazipo, maumivu ya tumbo, maumivu ya mwili, dalili za mfumo wa mkojo au dalili za mfumo wa upumuaji, manjano kwenye macho n.k

Utambuzi

  • Dalili au ishara na epidemiolojia
  • Kuchunguza kwa darubini kama kuna vimelea
  • Kuangalia kiwangu cha chembe nyeupe za damu – WBC
  • Kupandikiza damu ili kuhakikisha kuwa hakuna maambukizi mengine – blood cultre
  • Eksirei ya kifua ili kuhakikisha kuwa si nimoni

Matibabu

Malaria isiyokali

  • Artemether+Lumefantrine (FDC) (PO) 20mg+120mg (Watu wazima)
  • Fixed formulation Artemether 20mg, Lumefantrine120mg; 6, 12, 18 and 24 tablets blister
  • Fixed formulation Artemether 80mg, Lumefantrine 480mg; 6 tablets blister
  • Dihydroartemisinin+piperaquine (FDC) (PO).

Malaria kali

  • Parenteral artesunate – 2.4 mg/kg (IV) or (IM) given on admission (time = 0 hour), then at 12 hours and 24 hours for a minimum of 3 injections in 24 hours

Kuzuia

  1. Kutumia dawa za kukinga malaria – hasa kwa wageni wanaosafiri kwenda kwenye maeneo yenye malaria, kwa watoto chini ya miaka 5 na wajawazito kwa sababu hawajajenga kinga ya kutosha
  2. Kudhibiti mbu
  • Funika madimbwi, kata nyasi kuzunguka nyumba, funika maji yaliyo kwenye ndoo na makopo, nyunyiza dawa kwenye mabwawa ili kupunguza mazalia ya mbu
  • Vaa nguo zinazofunika, paka dawa za kufukuza mbu, lala chini ya neti, weka wavu kwenye madirisha, piga dawa ya kuua mbu
  1. Tibu wagonjwa wa malaria mapema

Vyanzo

http://www.nlm.nih.gov/medlineplus/ency/article/000621.htm

Shares:
2 Comments
  • Benjamin Najimu Mohamed
    Benjamin Najimu Mohamed
    March 4, 2025 at 8:50 am

    Hongera sana daktari. Unafanya kazi nzuri sana ya kuielimisha jamii kuhusu masuala ya afya.

    Reply
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *