Kwa nini uzazi wa mpango ni muhimu?

Kipindi cha ujauzito kinaweza kikawa ni hatari kwa mama na mtoto hususani kinamama wakipata ujauzito katika umri mdogo sana/mkubwa, muda mfupi baada ya kujifungua au wakizaa watoto wengi. Asilimia kumi na saba ya vifo vyote vya kinamama wa kitanzania kuanzia umri wa miaka 15-49 hutokea wakati wa ujauzito, wakati wanajifungua, ndani ya kipindi cha miezi miwili  baada ya kujifungua au kutoka kwa mimba. Vilevile mtoto mmoja kati ya watoto ishirini wa kitanzania hufariki dunia kabla ya kutimiza umri mwaka moja baada ya kuzaliwa. Njia mojawapo bora ya kuzuia vifo vya kinamama na watoto vitokanavyo na uzazi ni kuzuia mimba zisizopangwa/zisizotarajiwa na njia nzuri ya kujikinga na hili ni kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Nini hali halisi ya uzazi wa mpango Tanzania?

Ingawa kuna ongezeko la watu wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango lakini pia kuna ongezeko la watoto 5.4 wanaozaliwa kwa kila mwanamke mmoja.  Utafiti unaonyesha wanawake wengi huzaa mapema ambapo asilimia ishirini na nane 28% huzaa katika umri wa miaka 18, asilimia hamsini na tano 55% umri wa miaka 20 na asilimia themanini na nane 88% umri wa miaka 25. Tafiti hii inaonyesha kuna umuhimu wa kutoa elimu juu ya uzazi wa mpango kwa vijana, kwa watu ambao hawajaoa au kuolewa. Vilevile kuna ulazima wa kuwalenga pia wenza (wanaume).

Pia asilimia sabini 70% ya wanawake walioolewa wanatamani kuchelewa kupata watoto au kupanga idadi ya watoto watakaowazaa lakini ni asilimia ishirini na saba 27% ya wanawake hao hutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango. Ambapo  asilimia tano 5%  hutumia njia za muda mrefu na njia za kudumu za uzazi wa mpango.

Uzazi wa mpango una faida gani?

Pamoja na kumuwezesha mama na mtoto kuwa na afya njema, uzazi wa mpango una faida nyingi kwa wanawake, wanaume, watoto, familia na jamii kwa ujumla:

  • Unamsaidia mama kurudi katika hali yake ya zamani ambayo ilisumbuliwa na hali ya ujauzito, uchungu na kujifungua, mama atakuwa mwenye nguvu, afya nzuri na mchangamfu. Na pia atakuwa na muda mzuri wa kurudisha afya yake kabla ya kupata ujauzito mwingine.
  • Unamuwezesha kuhudumia familia yake vizuri na kuwa na maisha bora. Utakuwa na muda, fedha na mahitaji muhimu kwa familia yako kama chakula, mavazi, elimu, mapenzi na huduma zote muhimu.
  • Mama anapata muda wa kutosha wakujishughulisha na mambo mengine ya kiuchumi na kimaendeleo kwa ajili ya familia na jamii kwa ujumla.
  • Mama na baba wanapata muda mzuri wa kujishughulisha zaidi na mambo na mahitaji yao binafsi.
  • Unasaidia kukuza uchumi na maendeleo ya nchi

Nani anapaswa kutumia uzazi wa mpango?

Yoyote mwenye umri wa kuzaa au anatarajia kufikia umri huo anapaswa kufikiria kuhusu uzazi wa mpango. Uzazi wa mpango ni muhimu kwa:

  • Wanawake na wanaume
  • Watu walioa na kuolewa au ambao hawajaoa wala kuolewa
  • Watu wenye watoto au bado hawajapata watoto.

Ni wakati gani mtu atumie uzazi wa mpango? 

Umri sahihi wa kuanza kutumia uzazi wa mpango ni kuanzia miaka ishirini (20) na thelathini na tano (35). Ujauzito ni hatari kwa mama na mtoto endapo mama atajifungua chini ya umri wa miaka ishirini (20) au zaidi ya miaka thelathini na tano (35) vilevile ni hatari kwa mama atakaejifungua zaidi ya watoto wane au hasipowapishanisha watoto. Wenza wanatakiwa kusubiri angalau miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine pia wafikirie kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango wakati wote ambao hawajapanga kupata mtoto.

Njia za uzazi wa mpango ni zipi?

Kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinaweza kutumiwa na mtu au wenza waweze kusubiri, kuchelewesha, au kupunguza idadi ya watoto watakaowazaa. Zipo njia za mda mfupi, mda mrefu na za kudumu.

Njia za muda mfupi:

Hizi ni njia za kisasa za uzazi wa mpango ambazo unaweza kuzibadilisha. Unaweza kupata ujauzito pindi utakapoacha kuzitumia. Njia hizi ni nzuri kwa mama anayetaka kupata ujauzito baada ya miaka miwili baada ya kujifungua. Nazo ni:

  • Njia ya vichecheo – Njia hizi zina vichocheo ni sawa na vichocheo vya kawaida vilivyomo kwenye mwili wa mwanamke.
  • Njia za Kizuizi – Kondomu za kike na kondomu za kiume. Ni muhimu kutumia ipasavyo kila unapofanya ngono. Hii ni njia ya pekee ambayo pia inazuia maambukizi ya VVU na magonjwa ya zinaa.
  • Njia za asili
    • Kukosa hedhi kwa kunyonyesha mfululizo – Hii ni njia ya asili ambayo inatokea kwa mwanamke anayenyonyesha na ni ya kuaminika zaidi wakati mama huyo bado hajaanza kuona siku zake za hedhi na ili hayo yote yatokee ni lazima mama awe anamnyonyesha mwanae mara kwa mara usiku na mchana na Mtoto awe na umri chini ya miezi sita (6).
    • Elimu ya kujua siku za hatari uzazi – Hii inawezekana ikiwa mama anaufahamu mzunguko wake mzima wa siku zake za hedhi na kujua ni zipi siku za hatari za kushika mimba. Yeye na mwenza wanatakiwa kuacha kabisa kufanya ngono siku hizo za hatari.
    • Kukojoa nje Hii inafanywa na mwanamume wakati wa tendo la ndoa ambapo humwaga shahawa zake nje ya uke.

Njia za muda mrefu:

Hizi ni njia ambazo pia zinaweza kurudishwa. Unaweza kupata ujauzito mara utakapoacha kuzitumia. Hizi ni nzuri ikiwa unataka kusubiri zaidi ya miaka miwili kabla ya kupata mtoto mwingine.

  • Njia ya vipandikizi Hiki ni kijiti cha plastiki anachowekewa mwanamke chini ya ngozi kwenye mkono wake kinaweza kuwa kimoja au viwili. Hivi huzuia mwanamke asipate ujauzito kwa muda kati ya miaka 3 hadi 5 kutegemea na aina ya vipandikizi alivyotumia.
  • Njia ya kitanzi Ni kifaa kidogo chenye shaba na plastiki ambacho huwekwa kwenye mji wa mimba. Hichi hukuzuia usipate mimba mpaka miaka kumi na mbili (12), unaweza kukitoa wakati wowote utakapoamua au kuhitajia kupata mtoto.

Njia ya kudumu:

Hizi ni njia huwezi kuzirudia na ukitumia huwezi kupata mtoto tena. Na hutumiwa na watu ambao hawataki kupata mtoto tena. Nazo ni:

  • Kufunga kizazi kwa mwanaume Njia hii inahusisha upasuaji mdogo ambapo mirija ya uzazi ya mwanaume ukatwa au kufungwa hivyo kuzuia yai kusafiri na kukutana na shahawa. Mwanaume anaendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kutoa mbegu lakini mbegu zake hazitaweza kutunga mimba
  • Kufunga kizazi kwa mwanamkeNjia hii inahusisha upasuaji mdogo inafanyika kwa kuziba au kukata mirija ya kizazi kuzuia yai kukutana na mbegu. Mwanaumke ataendelea kuwa na hamu ya kujamiiana na kuona siku zake za hedhi.

Utafahamu vipi kuwa njia gani ya uzazi wa mpango ni sahihi kwako?

Inategemea na mtu mwenyewe au wenza kuamua njia gani ni sahihi kwao. Tembelea kituo cha afya kilicho karibu nawe uonane na wahudumu wa afya wataweza kukufahamisha njia sahihi kwako.

Ni nini Madhara ya njia za uzazi wa mpango?

Njia za kisasa za uzazi wa mpango hazina madhara na zinafanya kazi vizuri zikitumiwa kwa ufasaha. Yafuatazo ni maudhi madogo madogo ya njia za uzazi wa mpango ambayo ni ya kawaida na hayana madhara. Pia sio dalili ya maradhi. Mama wengine wanaweza kuona:

Madhara mengi yanapungua au kuisha ndani ya miezi michache baada ya kuanza kutumia njia za uzazi wa mpango. Ni wanawake wachache hupata matatizo baada ya kutumia njia za uzazi wa mpango. Ukipata matatizo yoyote nenda kituo cha Afya kilicho karibu nawe.

Vipi njia za uzazi wa mpango unaathiri uwezo wa kupata mtoto

Njia za kisasa za uzazi wa mpango hazimfanyi mtu kuwa tasa. Njia kama kondomu, vidonge, kitanzi na vipandikizi unapoviacha tu mwanamke anaweza kupata ujauzito. Inawezekana mwanamke kuchukua miezi michache kupata ujauzito kwa yule aliyetumia sindano. Hii ni hali ya kawaida na mwanamke hana haja ya kuwa na wasiwasi.

Kuna njia mbili za kudumu za kufunga kizazi kwa mwanamke na kufunga kizazi kwa mwanaume ambazo hawataweza kupata mtoto tena. Hizi ni kwa wale ambao wameamua kutopata mtoto tena katika maisha yao. Ni vizuri ifahamike kuwa uzazi unapungua kadiri mwanamke anapoongezeka umri. Unaweza kwenda kwenye kituo cha afya kilichopo karibu nawe wakati wowote ikiwa una tatizo lolote, maswali au ikiwa unataka kubadilisha njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Nani wa kufanya maamuzi kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango?njia za uzazi wa mpango

Ingawa wanawake ndio wanafanya maamuzi kutumia njia za uzazi wa mpango, ni vema wanawake na wanaume kwa pamoja kuwa na jukumu la kuchagua njia za uzazi wa mpango inayowafaa.

Wanaume wawasaidie vipi wanawake kutumia njia za uzazi wa mpango?

Kuna njia nyingi mwanaume anaweza kufanya kumsaidia mwanamke katika kutumia njia za uzazi wa mpango. Nazo ni:

  • Kuamua pamoja wakati muafaka wa kupata mtoto, idadi yao na muda wa kusubiri kati ya mtoto mmoja na mwingine.
  • Jifunze zaidi kuhusu njia za uzazi wa mpango.
  • Tembelea kituo cha afya kilicho karibu nawe ili upate ushauri juu ya njia za uzazi wa mpango kutoka kwa wahudumu wa afya.
  • Chagueni pamoja njia za uzazi wa mpango.
  • Wanaume wasaidie fedha za usafiri kwenda kliniki pamoja na kulipia njia za uzazi wa mpango.
  • Mshiriki kwa pamoja kutumia njia za uzazi wa mpango
  • Mkubaliane kutumia kondomu.
  • Tumieni njia mbadala kwa pamoja iwapo mama atasahau kutumia njia za uzazi wa mpango.

Vyanzo

National Bureau of Statistics (NBS) [Tanzania] and ICF Macro. 2011. Tanzania Demographic and Health Survey 2010. Dar es Salaam, Tanzania: NBS and ICF Macro.

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *