Maelezo ya jumla

Saratani ya mapafu ni kansa inayowapata watu wengi duniani kote. Ni kansa inayoongoza kwa kusababisha vifo kwa wanaume na wanawake duniani. Uvutaji wa sigara ni sababu kuu ya kutokea kwa kansa nyingi za mapafu. Mambo mengine yanayoongeza hatari ya kupata saratani ya mapafu ni pamoja na kiwango kikubwa cha uchafuzi wa mazingira, mionzi na athari za asbesto.

Kulingana na patholojia, kansa ya mapafu hugawanywa katika makundi mawili, ”small cell lung carcinoma” na ”non-small cell lung carcinoma”. Kansa ya mapafu husababisha kikohozi kisichopoa, maumivu ya kifua yasiyoisha, kukohoa damu, kupumua kwa shida, kukorota, kukwaruza kwa sauti, matatizo ya mara kwa mara kama nimonia (nyumonia) au mkamba , kuvimba kwa shingo na uso, kupoteza hamu ya kula, kupungua uzito na uchovu. Matibabu hujumuisha upasuaji, tiba ya mionzi, tiba kemikali au mchanganyiko wa hayo. Matarajio baada ya matibabu hutofautiana sana. Matarajio hutegemea hasa hatua ya kansa wakati wa utambuzi, na ikiwa uvimbe unaweza kuondolewa kwa upasuaji.

Je, nini dalili za saratani ya mapafu?

Mara nyingi katika hatua ya mwanzo kansa ya mapafu haina dalili. Lakini kansa inavyozidi kukua, dalili huanza kujitokeza ,kama zifuatazo:    

Katika hali ya kawaida, sio mara zote dalili hizi zinatokana na kansa. Matatizo mengine ya kiafya yanaweza kusababisha baadhi ya dalili hizi. Mtu yeyote mwenye dalili hizi anapaswa kumuona daktari atambuliwe na kutibiwa mapema iwezekanavyo.

Nini husababisha saratani ya mapafu?

Saratani ya mapafu husababisha vifo vingi kwa wanaume na wanawake. Kila mwaka, watu wengi zaidi hufa kwa kansa ya mapafu kuliko saratani ya matiti, koloni, na saratani ya tezi dume (prostate) kwa pamoja. Saratani ya mapafu huwapata watu wazima. Ni nadra kuwapta watu chini ya umri wa miaka 45. Uvutaji wa sigara ndiyo sababu kuu inayoongoza kwa kusababisha saratani ya mapafu. Kadri unavyovyuta sigara nyingi zaidi kwa siku na kadri unavyoanza kuvuta sigara katika umri mdogo zaidi, ndivyo hatari ya kupata saratani ya mapafu inavyoongezeka.

Hata hivyo, saratani ya mapafu imetokea kwa watu ambao hawajawahi kuvuta sigara. Kuvuta moshi wa sigara unaotoka kwa watu wengine wanaovuta huongeza hatari ya kupata kansa ya mapafu. Kulingana na Shirikisho la Kansa la Marekani, wastani wa watu wazima 3,000 wasiovuta sigara watakufa kila mwaka kutokana na saratani ya mapafu kwa sababu ya kupumua moshi wa sigara kutoka kwa wengine wanaovuta.

Yafuatayo yanaweza pia kuongeza hatari ya kupata kansa ya mapafu:   

  • Uchafuzi wa hewa uliokithiri    
  • Viwango vya juu vya arsenic kwenye maji ya kunywa    
  • Gesi ya radon   
  • Asbesto    
  • Historia ya kuwepo kansa ya mapafu kwenye familia    
  • Tiba ya mionzi kwenye mapafu    
  • Kukutana na kemikali zinazosababisha saratani kama vile Urani (uranium), beryllium, vinyl chloride, nickel chromates, bidhaa zitokanazo na makaa ya mawe (coal products), haradali (mustard gas), chloromethyl ethers, petrol (gasoline), na moshi wa dizeli.

Nani yuko kwenye hatari zaidi?

Tafiti zimegundua sababu zifuatazo huongeza hatari ya kupata saratani ya mapafu:    

  • Uvutaji wa tumbaku: moshi wa tumbaku husababisha saratani ya mapafu. Ndio sababu muhimu zaidi inayopelekea kutokea kwa saratani ya mapafu. Kemikali hatari zilizo kwenye moshi wa tumbaku huharibu seli za mapafu. Hii ndiyo sababu uvutaji wa sigara, kiko, au biri (cigar) husababisha saratani ya mapafu, na ndio sababu moshi kutoka kwa watu wengine unaweza kusababisha saratani kwa watu wasiovuta. Kadri mtu anapovuta moshi huu wa sigara ndivyo hatari yake ya kupata saratani inavyoongezeka.    
  • Radoni: Radoni ni gesi yenye miali nunurishi (radioactive) ambayo huwezi kuiona, haina harufu, au ladha. Inaundwa kwenye udongo na miamba. Watu wanaofanya kazi katika migodi wanaweza kuvuta gesi hii hatari ya radon bila kujua. Katika maeneo mengine ya nchi, radon inapatikana kwenye nyumba. Radon huharibu seli za mapafu, na watu wanaovuta radon huwa katika hatari kubwa ya kupata saratani ya mapafu.
  • Asbesto na vitu vingine: Watu wanaofanya kazi katika viwanda vya ujenzi na kemikali wako kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya mapafu. Kukutana na asbesto, aseniki, kromium, nickel, masizi, lami, na vitu vingine vinaweza kusababisha saratani ya mapafu. Hatari ni kubwa zaidi kwa wale waliokutana na kemikali hizi kwa muda mrefu zaidi.  Hatari ya kupata saratani ya mapafu ni maradufu kwa watu wanaovuta sigara.
  • Uchafuzi wa hewa: Uchafuzi wa hewa unaweza kuongeza hatari ya kupata kansa ya mapafu. Watu wanaovuta sigara na wanaoishi katika maeneo yenye uchafuzi mkubwa wa hewa ,wako kwenye hatari maradufu ya kupata saratani ya mapafu.
  • Historia ya kansa ya mapafu kwenye familia: Watu wenye baba, mama, kaka, au dada aliye na kansa ya mapafu wanaweza kuwa katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu, hata kama hawavuti sigara .    
  • Historia binafsi ya saratani ya mapafu: Watu ambao wameshawahi kuwa na kansa ya mapafu wako katika hatari zaidi ya kupata saratani nyingine.
  • Umri zaidi ya miaka 65: Watu wengi huwa na umri zaidi ya miaka 65 wakati wanapogunduliwa kuwa na kansa ya mapafu.

Utambuzi wa saratani ya mapafu

Ikiwa una dalili zinazofanana na za kansa ya mapafu, daktari ni lazima achunguze na kugundua kama dalili hizo zinatokana na kansa kweli au sababu nyingine. Daktari anaweza kukuliza kuhusu historia binafsi na historia ya kimatibabu ya familia yako. Daktari anaweza kuagiza vipimo vya damu, na anaweza pia kufanya vipimo vifuatavyo:

  • Uchunguzi wa kimwili: Daktari atachunguza mwili, atasikiliza jinsi unavyopumua, na kuchunguza kama kuna maji kwenye mapafu. Daktari anaweza kuchunguza kama tezi zako za limfu zimevimba na kama ini limevimba.
  • X-ray ya kifua: Picha za eksirei ya kifua zinaweza kuonesha uvimbe au maji kifuani.    
  • CT scan: Madaktari mara nyingi hutumia CT scans kupiga picha ya kifua. Mashine ya eksirei iliyounganishwa na kompyuta hupiga picha kadhaa,picha hizi zinaweza kuonesha uvimbe, maji , au tezi za limfu zilizovimba.

Jinsi ya kukusanya sampuli ya kipimo

Njia pekee ya uhakika ya kujua kama kuna kansa kwenye mapafu ni kwa daktari kuchunguza sampuli za seli au tishu. Mwanapatholojia huchunguza sampuli kwa darubini na hufanya vipimo vingine. Kuna njia nyingi za kukusanya sampuli.

Daktari anaweza kuamuru ufanye moja au zaidi ya vipimo vifuatavyo ili kukusanya sampuli:    

  • Sputum cytology (sitolojia ya kohozi): makohozi kutoka kwenye mapafu. Maabara huchunguza sampuli za makohozi kuangalia seli za kansa.    
  • Thoracentesis: Daktari hutumia sindano ndefu kutoa maji kifuani. Maabara huchunguza maji hayo kama kuna seli za saratani.    
  • Bronchoscopy: Daktari huingiza tube nyembamba yenye kamera (bronchoscope) mapafuni kupitia puani au mdomoni. Hii humpa furusa daktari kuchunguza njia ya hewa na mapafu. Daktari anaweza pia kuchukua sampuli ya seli kutoka katika sehemu ya mapafu anayoishuku kwa ajili ya kuipima.
  • Fine-needle aspiration: Daktari hutumia sindano nyembamba ili kuchukua tishu au maji kutoka kwenye mapafu au tezi za limfu.
  • Thoracoscopy: Daktari wa upasuaji atatoboa matundu kadhaa kifuani ili kuruhusu tube yenye kamera kuingia ndani ya kifua kwa ajili ya uchunguzi. Kipimo hiki humpatia fursa daktari kuyakagua mapafu bila kufungua kifua chote na kama ataona eneo lisilo la kawaida anaweza kuchukua nyama ndogo (biopsy) kwa ajili ya uchunguzi.
  • Thoracotomy: Huu ni upasuaji mkubwa,daktari wa upasuaji hufungua kifua ili kuyakagua vyema mapafu na ikiwezekana kuiondoa kabisa sehemu ya mapafu yenye kansa. Tezi za limfu na tishu nyingine zinaweza kuondolewa pia.    

Wakati gani utafute matibabu ya haraka?

Mtu yeyote aliye na dalili zinazofanana na zilizoorodheshwa hapo juu anapaswa kumuona daktari atambuliwe na kutibiwa mapema iwezekanavyo.

Uchaguzi wa matibabu

Wagonjwa wenye kansa ya mapafu wana chaguzi nyingi za matibabu. Uchaguzi wa matibabu hutegemea hatua ya saratani. Chaguzi za matibabu ni pamoja na,upasuaji, tiba ya mionzi, tibakemikali, au mchanganyiko wa njia hizi. Kabla ya kuanza kwa matibabu, uliza kuhusu madhara yatokanayo na matibabu kwa sababu mara nyingi matibabu ya saratani huharibu seli na tishu zenye afya pia. Athari za matibabu hazifanani kwa watu wote na zinaweza kubadilika kulingana na aina ya tiba.

  • Upasuaji: Kama hatua ya kansa na afya ya mgonjwa kwa jumla inaruhusu, upasuaji ni tiba kuu ya saratani ya mapafu. Uvimbe wote na sehemu ya seli zenye afya zinazouzunguka huondolewa.
  • Tiba ya mionzi: Hii ni tiba ya kansa inayoua seli za saratani au kuzizuia kukua kwa kutumia mionzi ya yenye nguvu sana.    
  • Tibakemikali: Tiba hii hutumia madawa kuua seli za saratani au kuzizuia zisikue au kuongezeka.    
  • Matibabu ya kulenga (targeted therapies): aina hii ya tiba hutumia dawa zinazolenga  kupunguza ukuaji wa mishipa ya damu kwenye uvimbe na madawa yanayolenga kuzuia epidermal growth factor receptor ambayo huchochea ukuaji wa uvimbe wa kansa.

Magonjwa yenye dalili zinazofanana na kansa ya mapafu    

Nini cha kutarajia?

Matarajio kwa kansa ya mapafu ni mabaya na hutegemea mambo yafuatayo:    

  • Kama uvimbe unaweza kuondolewa kwa upasuaji au la.   
  • Hatua (stage) ya kansa: ukubwa wa uvimbe na  kama kansa imeenea hadi nje ya  mapafu
  • Afya ya mgonjwa kwa ujumla    
  • Kama kansa ndio imegunduliwa sasa au imejirudia baada ya kutibiwa.

Jinsi ya kuzuia saratani ya mapafu

Takwimu za epidemiolojia zinaonesha kufanya mambo yafuatayo kunapunguza maradufu hatari ya kupata kansa ya mapafu.

  • Epuka uvutaji wa sigara au kupumua moshi wa watu wengine wanaovuta.    
  • Punguza au epuka kabisa kukutana gesi ya radon.    
  • Epuka kukutana na kemikali zinazosababisha kansa ya mapafu unapokua mahali pa kazi au mahali pengine.    
  • Kula chakula bora ,matunda na mboga nyingi.    
  • Kwa wavutaji wa sigara wa sasa au wa zamani, watumie dozi kubwa ya vitamini au madawa yenye vitamin nyingi.

Vyanzo

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *