Saratani ya ovari ni nini?

Saratani ya ovari ni kansa inayoanzia kwenye ovari. Ovari ni viungo vidogo vinavypatikana upande wa kulia na kushoto mwa mji wa mimba (uterasi). Ovari zinatunza mayai ya uzazi na kutengeneza homoni za kike. Saratani ya ovari ni ngumu kuitambua mapema kwa sababu wanawake wengi hawaisikii wakati inapokuwa inakua. Hata baada ya mwanamke anapoanza kuona dalili, bado inakuwa ngumu kujua kama shida imeanzia kwenye ovari. Na hii ndio sababu mara nyingi utakuta kansa hii imesambaa kwenda sehemu nyingine kabla ya kugunduliwa.

Nani anapata saratani ya ovari?

Inaweza kutokea katika umri wowote. Lakini visa vingi vinatokea baada ya damu ya hedhi kukata (ukomo wa hedhi). Inawapata zaidi wanawake ambao:

  • Wana mwanafamilia ambaye ana saratani ya ovari au saratani ya matiti
  • Wamekuwa wakitumia dawa za kuongeza homoni mwilini baada ya damu ya hedhi kukata kwa zaidi ya miaka mitano
  • Wana uzito mkubwa wa mwili

Nifanye nini kama nadhani kuwa saratani ya ovari inarithiwa katika familia yangu?

Kuna vipimo mbalimbali vinavyoweza kupima na kuangalia kama una jeni zinazokuweka kwenye hatari ya kupata saratani ya ovari. Ongea na daktari ili uweze kufanyiwa vipimo hivi kama:

  • Una mwanafamilia ambaye aligunduliwa na saratani ya matiti au saratani ya ovari kabla ya umri wa miaka 45
  • Una mwanafamilia ambaye amewahi kupata saratani ya matiti au saratani ya ovari zaidi ya mara moja
  • Una mwanaume kwenye familia yako aliyewahi kupata saratani ya matiti

Nitapunguza  vipi hatari ya kupata saratani ya ovari?

Ili kupunguza hatari ya kupata saratani ya ovari

  • Usitumie dawa kuongeza homoni mwilini kwa zaidi ya mika kadhaa baada ya damu kukata (menopause)
  • Usitumie talc powder kwenye via vya uzazi
  • Punguza uzito wa mwili kama ni mkubwa sana
  • Kama una mtoto, mnyonyeshe

Nitajuaje kama nina saratani ya ovari?

Ni vigumu kujua.

  • Unaweza kupata maumivu ya tumbo, kujaa kwa tumbo, au matatizo wakati wa kukojoa.
  • Unaweza kutokwa na damu ukeni isivyo kawaida

Kama mambo haya yakitokea haimaanishi kuwa una saratani ya ovari, kwa sababu yanaweza kutokea kwa sababu nyingine nyingi. Lakini unapaswa kumwona daktari ili atambue tatizo ni nini?

Kuna njia yoyote ya kutambua kansa ya ovari mapema kabla haijasababisha matatizo?

Hakuna njia nzuri ya kuangalia saratani ya ovari kama ilivyo kwa saratani nyingine, saratani ya njia ya haja kubwa tunaweza kufanya kipimo cha colonoscopy au saratani ya shingo ya mlango wa kizazi tunaweza kufanya Pap smear. Kwa saratani ya ovari, hatuna njia nzuri. Lakini kama saratani ya ovari inarithiwa kwenye familia yako, ni vizuri kufanya kipimo cha kuangalia jeni za mwili, ili kuona kama una umerithi jeni inayokuweka kwenye hatari.

Saratani ya ovari inatibiwaje?

Matibabu ya kawaida ni upasuaji. Tibakemikali inaweza pia kutumika kwa baadhi ya wagonjwa.

Angalizo

Taarifa zilizotolewa katika ukurasa huu zimetoa muhtasari na zinaweza zimfae kila mtu. Ongea na daktari ili kung’amua kama taarifa hizi zinakufaa na wewe au jaribu kutafuta habari zaidi kuhusu shida hii.

Vyanzo

https://medlineplus.gov/ovariancancer.html

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *