Ugonjwa wa glaukoma (presha ya macho) ni nini?

Ugonjwa wa glaukoma (presha ya macho) – Ni ugonjwa wa macho ambao huharibu mshipa mkuu wa neva ya kuona, na mara nyingi husababishwa na kuongezeka kwa mbanano/shinikizo ndani ya jicho. Mbanano huu mara nyingi husababishwa na kushindwa kupenya kwa maji yanayokaa mbele ya mboni ya jicho kwenye njia yake ya kawaida.

Ugonjwa huu ni hatari sana kwani mara nyingi huja bila maumivu ya jicho na kuharibu taratibu mshipa wa fahamu wa kuona, pia unaweza kuharibu jicho kidougokidogo kwa miaka mingi, kabla uwezo wa kuona haujapungua au kwisha kabisa na kuleta upofu wa kudumu

Sababu ya kutokea mbanano/shinikizo ndani ya jicho (presha ya macho)

  • Maji yanayotengenezwa na jicho kushindwa kufuata sehemu yake ya kutokea.
  • Kuziba kwa mboni ya jicho kwa kushikana na kioo cha jicho au lensi yenyewe kuwa kubwa sana kuziba mboni yote.
  • Kuharibika kwa mfunuo wa njia ya kutokea hayo maji kuelekea kwenye mishipa ya damu inayozunguka jicho

Chanzo/asili ya ugonjwa wa glaukoma (presha ya macho)

  • Kwa kurithii kutoka kwa wazazi ambao wana asili ya shida hii
  • Kupata jeraha la jicho
  • Matatizo ya magonjwa mengine
  • Ugonjwa huu huonekana zaidi kwa watu wenye umri wa miaka 40 na zaidi

Dalili za mbanano/shinikizo ndani ya jicho

Ni vigumu kuugundua huu ugonjwa pindi unapoanza kwa sababu mara nyingi mwanzo wake hauna dalili zozote za wazi. Mara nyingi watu hufika kumwona mtaalamu wa macho wakati ugonjwa umeshaleta madhara makubwa ambayo hayawezi kutibiwa wala kurudisha uwezo wa kuona kama ulivyokuwa awali

  • Uwezo wa kuona unapungua hasa sehemu za upande, na baadaye hauwezi kuona vizuri sehemu zote.
  • Mara nyingi hugundulika kwenye upimaji wa kawaida wa macho au wakati wanapochunguzwa magonjwa mengine ya macho

Matibabu ya ugonjwa wa glaukoma (presha ya macho)

Upasuaji mdogo hufanyika (tundu dogo linatengenezwa) kuwezesha maji hayo kuzunguka sawasawa ili kupunguza mbanano ndani ya jicho.

Kawaida upasuaji huu hufanyika kwenye hospitali kubwa za macho zenye vyombo vya kufaa na wataalam wa kutosha.

Dokezo muhimu kuhusu ugonjwa wa glaukoma

Uharibifu wa mishipa wa neva ya kuona ni tatizo la kudumu. Hakuna matibabu yanayoweza kurudisha uweza wa kuona kama hapo awali. Matibabu yanalenga kuzuia kuharibika zaidi kwa mshipa wa neva ya kuona. Mtu yeyote afikapo umri wa miaka 49 au zaidi ni vizuri aende kwa mtaalam wa macho akachunguzwe ili kugundua mapema shida yeyote ya macho

Vyanzo

Kipeperushi: Kilimanjaro Centre for Community Ophthalmology (KCCO)

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *