Ugonjwa wa hashimoto ni nini?
Ugonjwa wa hashimoto ni tatizo la tezi dundumio. Tezi dundumio ni tezi iliyopo kwenye sehemu ya mbele ya shingo na inasaidia kudhibiti matumizi ya nguvu mwilini. Kama una ugonjwa wa hashimoto, tezi dundumio haifanyi kazi vizuri ya kutengeneza homoni na matumizi ya nguvu mwilini yanatatizika.
Ni zipi dalili za ugonjwa wa hashimoto?
Watu wengi wenye ugonjwa huu hawana dalili. Kipimo cha kawaida cha homoni kinaweza kuonesha kiwango kisichosawa cha homoni zinazotolewa na tezi dundumio.
Kwa sababu tezi dundumio inaweza kukua kubwa, unaweza kujisikia sehemu ya mbele ya shingo imekaza au imejaa.
- Unaweza kupata shida kumeza chakula au kunywa vinywaji.
- Unaweza kuwa na uvimbe unaoitwa rovu sehemu ya mbele ya shingo.
Baadhi ya watu wenye ugonjwa wa hashimoto wana dalili kama vile;
- Uchovu
- Kusahausahau
- Sonona
- Ngozi iliyokauka
- Moyo unaopiga polepole,
- Kuongezeka uzito
- Kufunga choo na
- Kuogopa baridi au kushindwa kukaa eneo lenye baridi ya kawaida.
Kipimo cha damu kinaweza kueleza kama tezi dundumio inafanya kazi au la. Vipimo vingine vinaweza kutumika.
Ni nani anapatwa na ugonjwa wa hashimoto?
Japo ugonjwa wa hashimoto unaweza kuwapata watu wa rika zote, lakini unawapata zaidi wanawake walio katika miaka ya 30 na 40. Kama kuna mtu kwenye familia yako ana ugonjwa wa hashimoto, uko kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu pia. Hakuna mtu anayejua kwa uhakika kwa nini ugonjwa huu unatokea.
Ugonjwa wa hashimoto unatibiwa vipi?
Ugonjwa wa hashimoto hauna tiba ya kuutibu ukapona kabisa. Hata hivyo, daktari anaweza kukupatia matibabu ili kuhakikisha kuwa homoni zilizopungua mwilini kwa sababu ya tezi dundumio kuharibiwa zinawekwa sawa kwa kutumia dawa.
Dawa za tezi dundumio zinaweza kufanya kazi kama mbadala wa homoni zilizokuwa zinatolewa na tezi dundumio. Muda utakaohitajika kutumia dawa hizi unategemea matokeo ya vipimo vya damu. Dawa za kuongeza homoni zinazotengenezwa na tezi dundumio hazisababishi madhara yoyote kwa watu wengi.
Kutumia dawa za kuongeza homoni za tezi dundumio na kufanya vipimo vya damu mara kwa mara kuangalia namna tezi dundumio inavyofanya kazi kutasaidia kuzuia dalili kama vile uchovu, kuongezeka uzito na kufunga choo.
Levothyroxine ndiyo ni moja ya dawa inayopendelewa zaidi kutibu upungufu wa homoni za tezi dundumio
Angalizo
Taarifa zilizotolewa katika ukurasa huu zimetoa muhtasari na zinaweza zimfae kila mtu. Ongea na daktari ili kung’amua kama taarifa hizi zinakufaa na wewe au jaribu kutafuta habari zaii kuhusu shida hii.
Vyanzo
https://medlineplus.gov/genetics/condition/hashimoto-thyroiditis/