Maelezo ya jumla

Ugonjwa wa homa ya matumbo (typhoid fever) ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria anayeitwa salmonella typhi.

Ni zipi dalili za ugonjwa wa typhoid?

Zifuatazo ni dalili za ugonjwa wa homa ya matumbo:

Ni nini sababu ya ugonjwa wa homa ya matumbo?

Bakteria anayesababisha ugonjwa huu – salmonella typhi – husambaa kutokana na kula chakula, kunywa vinywaji au maji yaliyochafuliwa. Kama ukila au kunywa chochote kilichochafuliwa, bakteria huingia mwilini, na kuingia kwenye utumbo, na baadae kwenye damu, kisha husafiri na kufika kwenye tezi za mwili, mfuko wa nyongo, ini, bandama, na sehemu nyingine za mwili.

Kuna baadhi ya watu wachache wanaweza kubeba bakteria hawa wa salmonella typhi bila kuugua, lakini wanaendelea kutoa bakteria kwenye kinyesi kwa miaka mingi na kusambaza ugonjwa huu. Ugonjwa wa homa ya matumbo umekithiri sana katika nchi zenye uchumi unaokua.

Ni nani yuko kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa h0ma ya matumbo?

Mtu yeyote anayekutana na bakteria wa salmonella typhi yuko kwenye hatari.

Ni wakati gani unapaswa kuomba msaada wa kitabibu?

Ongea na daktari kama umekutana na mtu mwenye homa ya matumbo au kama una dalili za homa ya matumbo. Kama umewahi kuugua na kutibiwa ugonjwa wa homa ya matumbo, wakati mwingine ugonjwa unaweza kujirudia. Ongea na daktari pia kama unapata maumivu makali sana ya tumbo, unapata mkojo kidogo sana au haukojoi kabisa, au kama unaona kuna dalili mpya usizozielewa.

Utambuzi wa  homa ya matumboUgonjwa wa homa ya matumbo

Unapokuwa umegundulika kuwa una salmonella typhi kwa vipimo vya maabara; stool culture au ELISA daktari ataanzisha matibabu

Uchaguzi wa matibabu ya homa ya matumbo

Unaweza kuongezewa maji kupitia kwenye mishipa. Utapatiwa antibiotiki zinazofaa kuua bakteria. Kuna ongezeko kubwa la usugu wa vimelea kwa dawa ulimwenguni, kwa hiyo daktari ataangalia ni aina gani ya dawa inapendekezwa tumika na wizara ya afya.

Baadhi ya dawa zinazopendelewa zaidi ni pamoja na ampicillin, trimethoprim-sulfamethoxazole na ciprofloxacin. Wagonjwa wanapatiwa antibiotiki mara nyingi huanza kujisikia nafuu baada ya siku 2 au 3, ni kwa nadra sana kifo kutokea. Hata hivyo, watu wasiopata matibabu wanaweza kuendelea kupata homa kwa wiki au miezi kadhaa, na karibia 20% hufariki kutokana na matatizo yanayosababishwa na maambukzi haya

Matarajio

Dalili mara nyingi huboreka ndani ya wiki 2 mpaka 4 baada ya matibabu. Matokeo ni mazuri zaidi kama matibabu yatawahi, na yanweza yasiwe mazuri sana kama matatizo yanayosababishwa na maambuzki yatakuwa yameanza kutokea. Dalili zinaweza kujirudia kama mgonjwa hatatumia dawa zote na kupna kabisa maambukizi.

Matatizo yanayoweza kutokea

Yafuatayo ni matatizo yanayoweza kutokea kama ugonjwa wa homa ya matumbo hautatambuliwa na kutibiwa mapema:

  • Kuvuja damu kwenye utumbo
  • Kutoboka kwa utumbo
  • Kushindwa kwa figo kufanya kazi
  • Kusambaa kwa maambukizi kwenye tumbo na kusababisha uvimbe wa fumbatio – peritonitis

Kuzuia

Japo zipo chanjo kwa ajili ya kuzuia ugonjwa wa homa ya matumbo, hazifanyi kazi kila wakati, kwa hiyo ni vizuri kunywa maji yaliyochemshwa pekee au maji ya chupa na kula chakula kilichopikwa vyema.

Kuboresha mfumo wa kutibu maji ya bomba, maji taka, na kulinda chakula kisichafuliwe ni moja ya njia za kuilinda jamii dhidi ya homa ya matumbo.

Kama kuna mtu anayebeba ugonjwa huu lakini haugui na anaweza kuwaambukiza wengine “typhoid carriers” wasiruhusiwe kuwa wapishi au kushughulika na chakula.

MAELEZO ZAIDI YA ZIADA KWA UFUPI

Homa ya matumbo ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababisha homa, uchovu wa mwili na huzihusisha pia tishu za mfumo wa limfu.

Sababu ya homa ya matumbo

  • Salmonella typhi
  • Salmonella enteriditis (nadra sana)

Epidemiolojia ya homa ya matumbo

  • Inatokea duniani kote, hasa maeneo enye uchumi duni
  • Kwa mwaka kunakadiriwa kutokea visa milioni 17 na kusababisha vifo 128,000 – 160,000 duniani.
  • Ugonjwa huu unawapata zaidi watoto walio shuleni (miaka 5-19)

Njia ya kuambukizwa ugonjwa wa homa ya matumbo

  • Kwa maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi na mkojo wa mgonjwa au mtu anayebeba ugonjwa huu.
  • Nzi wanaweza kutua kwenye chakula na kisha vimelea kuongezeka mpaka kufikia kiwango kinachotosha kusababisha maambukizi

Muda mpaka dalili za ugonjwa homa ya matumbo kuonekana

Inachukua muda wa wiki 1-3 dalili kuonekana toka kuambukizwa

Muda wa uambukizo wa ugonjwa wa homa ya matumbo

  • Ilimradi mtu anatoa vimelea kwenye kinyesi anaweza kuambukiza wengine, na hii inaanza wiki 1 baada ya kuambukizwa.
  • Karibu 10% ya wagonjwa wasiopata matibabu wataendelea kutoa vimela kwa miezi 3 baada ya dalili kuanza na 2% – 5% wanakuwa wabebaji sugu wa ugonjwa huu

Watu walio kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa ugonjwa wa homa ya matumbo

  • Watu wote wako kwenye hatari, ila hatari ni kubwa zaiid kwa watu wenye VVU
  • Mtu hupata kinga ya muda mfupi baada ya kuugua au baada ya kupewa chanjo, lakini haitoshi kukukinga na kama utakula kiwango kikubwa cha vimelea

Dalili za ugonjwa wa homa ya matumbo

  • Wiki ya kwanza – Kujihisi kuumwa kiasi ukiwa na homa inayoendelea kupanda taratibu, kichefuchefu, uchovu wa mwili na maumivu ya mwili kiujumla. Maumivu yasiyomakali na yasiyoisha ya sehemu ya mbele ya kichwa. Kuvuja damu puani, maumivu yasiyomali ya tumbo na kufunga choo kwa 10% ya wagonjwa.
  • Wiki ya pili – Homa isiyopungua. Kujihisi kuumwa sana na mchovu, unashindwa kufikiri vizuri, kujisikia vibaya na kuvimba kwa tumbo. Kuhara kunaweza kutokea na kinyesi kinaweza kuwa na damu.
  • Wiki ya tatu – Mgonjwa anaendelea kuwa na homa kali na kujihisi mchovu sana. Kama hakutatokea matatizo mengine wakati huu, mgonjwa huanza kujihisi na homa kuanza kupungua taratibu.

Utambuzi wa homa ya matumbo

  • Unaweza kufanyika kwa kufuata dalili na ishara, lakini hii inaweza kuchanganywa na magonjwa mengine yenye dalili zinazofanana
  • Kwa kufanya kipimo cha Widal ili kuangalia uwepo wa vimelea
  • Kupandikiza – culture – damu, kinyes au mkojo

Matibabu ya ugonjwa wa homa ya matumbo

Kwa homa ya matumbo isiyokali sana

  • Ciprofloxacin (dawa ya kumeza) 500mg mara 2 kwa siku kwa jumla ya siku 10-14 AU
  • Azithromycin (dawa ya kumeza) 500mg mara 1 kwa siku kwa jumla ya siku 7 AU
  • Cefixime 400mg (dawa ya kumeza) mara 1 kwa siku kwa jumla ya siku 7-14

Kwa homa ya matumbo iliyo kali sana

  • Ciprofloxacin (dawa ya kuchoma kwenye mshipa) 400 mg mara 2 kwa siku kwa jumla ya siku 7 AU
  • Ceftriaxone (dawa ya kuchoma kwenye mshipa) 1-2gm mara 1 kwa siku kwa jumla ya siku 4-7

Kuzuia ugonjwa wa homa ya matumbo

  1. Tibu mapema wagonjwa na watu wanaobeba ugonjwa huu
  2. Elimu kuhusu kunawa mikono, hasa kwa wapishi, wagonjwa na walezi wa watoto
  3. Matumizi sahihi ya choo na kudhibiti nzi
  4. Kuwezesha upatikanaji na matumizi ya maji salama
  5. Utunzaji salama wa chakula
  6. Kuzuia wagonjwa au wanaobeba vimelea kupika chakula
  7. Kuwapatia chanjo watu walio kwenye hatari zaidi
  8. Kuwapima mara kwa mara watu wanaopika chakula na kushughulika na vinywaji – hotelini, cafeteria n.k

Vyanzo

https://medlineplus.gov/druginfo/meds/a607028.html

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *