Ugonjwa wa Kawasaki ni nini?
Ugonjwa wa Kawasaki ni ugonjwa ambao ni nadra sana unaowapata watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano. Ugonjwa huu unasababisha kuvimba kwa mishipa ya damu, hasa mishipa inayosambaza damu kwenye misuli ya moyo (ateri za koronari). Inaweza kusababisha dalili kama:
- Homa
- Upele
- Wekundu kwenye sehemu nyeupe ya jicho
- Kuvimba kwa mikono na miguu
- Harara kwenye midomo (midomo ianonekana imechanikachanika au kupasukapasuka), mdomo na koo.
- Kuvimba kwa shingo
Ugonjwa wa huu unasababishwa na nini?
Hakuna anayejua kwa hakika nini kinasababisha ugonjwa huu. Kama mtoto ana dalili za ugonjwa huu, daktari atahitajika kupima na kujihakikishia kuwa hakuna magonjwa mengine yanayoweza kusababisha dalili hizi kabla ya kufanya utambuzi. Baadhi ya watoto wenye ugonjwa huu hawana dalili kabisa. Uchunguzi wa mwili wa mtoto na vipimo vya damu na mkojo vitasaidia kutambua kama mtoto ana ugonjwa huu.
Ugonjwa wa kawasaki unatibiwa vipi?
Ugonjwa wa kawasaki unatibiwa kwa dawa inayoitwa IVIG (immunoglobulin) inayotengenezwa kutokana na damu na dozi kubwa sana ya dawa ya aspirin. Mtoto atahitaji kubakia hospitalini kwa uangalizi na matibabu. Watoto wanaotibiwa mapema, wanapunguza uwezekano wa kupata matatizo ya moyo yanayoletwa na ugonjwa huu. Watoto wengi huanza kujisikia vizuri ndani ya siku moja au mbili baada ya kuanza matibabu.
Ngozi ya vidole vya mikono na miguu inaweza kuanza kuchunika/kukwanguka baada ya wiki kadhaa za kuugua. Hali hii itaisha yenyewe baada ya siku kadhaa au wiki kadhaa hauhitaji matibabu.
Ni nini kinatokea baada ya matibabu ya ugonjwa wa kawasaki?
Watoto wengi wenye ugonjwa wa kawasaki wanaweza kurudi na kuendelea na shughuli za kila siku baada ya kurudi nyumbani kutoka hospitali. Inaweza kuchukua siku au wiki kadhaa kujisikia vizuri kama kawaida.
Mtoto atahitaji vipimo vya mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa hana matatizo ya moyo. Vipimo hivi vinafanyika wiki mbili na miezi miwili baada ya matibabu. Baadhi ya watoto wanaweza kuhitaji vipimo zaidi kama wana matatizo ya moyo. Kuna uwezekano kuwa mtoto hatapata tena ugonjwa wa kawasaki.
Baadhi ya chanjo za watoto kama vile chanjo ya tetekuwanga, surua, matubwitubwi na chanjo ya surua ya ujerumani “rubella”, hazipaswi kutolewa kwa watoto hawa kwa kipindi cha miezi 11 baada ya kuugua ugonjwa wa kawasaki. Daktari atakuambia wakati itakapokuwa sawa kupata chanjo hizi.
Kazi nzuri daktari
Karibu saana mtaalamu, endelea kujifunza nasi