Maelezo ya jumla
Ugonjwa wa matende ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea ambao hauwezi kuwaona kwa macho pekee, unahitaji darubini, vimelea hawa wanafanana na minyoo. Vimelea hawa kama minyoo, wanapokuwa wakubwa wanaishi katika mfumo wa limfu. Mfumo wa limfu ni mfumo unaodhibiti kiwango cha maji yaliyo kwenye damu na unabeba kingamwili zinazopambana na maambukizi.
Ugonjwa wa matende unawaathiri takribani watu milioni 120 katika nchi 73 za ukanda wa kitropiki, Asia, Afrika, mashariki mwa bahari ya pasifiki, na sehemu za visiwa vya karibea na kusini mwa Amerika.
Ni zipi dalili za ugonjwa wa matende?
- Unaweza kuwa hauna dalili yoyote katika hatua za mwanzo za ugonjwa
- Kuwa na matende (hasa miguuni – miguu inaongezeka ukubwa na kuvimba – mguu wa tembo)
- Kuvimba kwa pumbu – pumbu zinaongezeka ukubwa
- Kukohoa
- Homa
- uchovu
- Maumivu ya kichwa
- Kuhisi baridi
- Kuwashwa
- Kuvimba kwa mfumo wa limfu
Ni nini husababisha ugonjwa wa matende? 
Ugonjwa wa matende unasababishwa na vimelea wanaoitwa nematodi au minyoo mviringo. minyoo hawa huongezeka ukubwa na wingi na hatimaye kusababisha mishipa ya limfu kuvimba na hatimaye kuziba kabisa. Kwa sababu ya kuziba kwa mishipa ya limfu, maji na kiwango kidogo cha protini hujikusanya kwenye tishu za sehemu za miguu au korodani taratibu na kwa miaka mingi na hatimamye kusababisha matende. Minyoo hawa ni pamoja na:
- Brugia malayi
- Brugia timori
- Loa loa
- Mansonella ozzardi
- Mansonella perstans
- Mansonella streptocerca
- Onchocerca volvulus
- Wuchereria bancrofti
Nani yuko kwenye hatari zaidi?
- Ili kupata ugonjwa wa matende mtu atahitajika kuumwa na mbu mara nyingi na mara kwa mara
- Watu wanaoishi maeneo ya kitropiki yenye ugonjwa huu wako kwenye hatari
Ni wakati gani utafute matibabu ya ugonjwa wa matende?
Ni vizuri kuomba msaada wa kitabibu kama una dalili zozote za ugonjwa wa matende, dalili kama vile:
- Homa inayotokana na minyoo kuwepo mwilini
- Matende kwenye miguu – kuongezeka ukubwa wa mguu
- Kuvimba pumbu
- Kuwa na vivimbe chini ya Ngozi
Utambuzi wa ugonjwa wa matende
Njia nzuri ya kuutambua ugonjwa huu ni kwa kuwachunguza minyoo hawa kwenye damu kwa kutumia darubini. Uchunguzi huu unaweza kuwa mgumu kwa sababu minyoo hawa mara nyingi hujitokeza kwenye damu wakati wa usiku pekee. Na kwa sababu hii, damu kwa ajili ya kipimo inapaswa kuchukuliwa wakati wa usiku minyoo anapotoka mafichoni na kuingia kwenye damu.
Kuna njia nyingine ya kupima kwa kutumia serolojia – vipimo vya serolojia vinafaa kwa sababu, baadhi ya watu wanaweza kuwa wamekwisha kuwa na matende na inaweza kuwa ngumu kuwapata minyoo.
Uchaguzi wa matibabu ya ugonjwa wa matende
Watu wenye minyoo wakubwa wanapaswa kumeza dozi ya dawa inayoitwa diethylcarbamazine kila mwaka, ili kuua minyoo wadogo wanaozunguka kwenye damu. Japo dawa hii haiui minyoo wakubwa, inasaidia kupunguza uwezekano wa kuwaambukizwa wengine.
Kuwa na matende kwenye miguu au kuvimba kwa pumbu, sio sababu ya kupewa dawa ya diethylcarbamzine – kwa sababu watu wengi wenye matende na kuvimba kwa pumbu hawana maambukizi ya ugonjwa matende kwa wakati huo – unakuta minyoo wamekwisha kufa.
Daktari anapaswa kufanya kipimo kujihakikishia kuwa bado mgonjwa ana minyoo na kisha ndio aagize dawa baada ya utambuzi.
Matende yanaweza kutokea hata baada ya minyoo yote kufa. Fuata mapendekezo yafuatayo ili kupunguza shida zinazoletwa na matende kutokea:
- Nawa vizuri sehemu ziliozovimba kwa kutumia sabuni na maji kila siku
- Nyanyua na fanyisha mazoezi mkono au mguu uliovimba / wenye matende ili kuboresha mzunguko wa mfumo wa limfu
- Kama kuna kidonda kihudumie. Tumia dawa za kudhibiti maambukizi ya bakteria au fangasi kama zinahitajika.
Matarajio
- Visa vinavyotambulika mapema vina matarajio mazuri
- Kama ugonjwa utaendelea unaweza kumwacha mtu katika hali mbaya ya ulemavu – ugonjwa wa matende unaweza kuharibu kabisa via vya uzazi au miguu
Mtatizo yanayoweza kutokea
- Matende kwenye miguu – kuvimba kwa miguu
- Ngiri maji
- Kuharibika kwa figo
Kuzuia ugonjwa wa matende
Kuepuka kuumwa na mbu ndio njia bora zaidi ya kujikinga. Mbu wanaoeneza maambukizi ya ugonjwa wa matende wanauma watu nyakati za jioni. Kama unaishi au kama unasafiri kwenda eneo lenye ugonjwa wa matende:
- Lala chini ya chandarua
- Vaa nguo zenye mikono mirefu na suruali
- Tumia dawa za kufukuza mbu kwney maeneo ambayo hayajafunikwa, hasa jioni
MAELEZO ZAIDI KUHUSU UGONJWA WA MATENDE
Maelezo ya jumla
Ni ugonjwa unaosababishwa na mwili kuitikia ili kupambana na uwepo wa minyoo kwenye mfumo wa limfu wa mwili
Sababu
- Wucheriria bancrofti (wanasambazwa na mbu aina ya culex, Anopheles au Aedes)
- Brugia malayi and (wanasambwa na mbu aina ya mansonia)
- Brugia timori (wanasambazwa na mbu aina ya Anopheles)
Epidemiolojia
Unapatikana sana maeneo ya kitropiki ya Afrika, eneo la bahari ya pasifiki, kati na kusini mwa Maerika.
Uambukizo
UNasambazwa kwa kuumwa na mbu aliyeambukizwa mabuu/larvae wanaosababisha ugonjwa
Muda kabla ya dalili kuanza
Mwezi mmoja, mzio unaosababishwa na kuvimba kunaweza kuonekana – allergic inflammatory
Muda wa uambukizo
Wanadamu wanawaambukiza mbu kunapokuwepo na mabuu (microfilariae) kwenye damu. Mabuu haya yanaweza kubakia mwilini kwa mika 5 -10 au zaidi. Mbu anakuwa tayari kuambukiza watu masaa 12-14 baada ya kunyonya damu yenye mabuu.
Nani yuko kwenye hatari
Watu wote wako kwenye hatari
- Muundo wa uambukizo -life cycle
-
- Buu (larvae) anatoboa ngozi na kuingia ndani wakati mbu anapokuwa akinywa damu
- Ndani ya mwili wa mwanadamu, buu anakua na kuwa mnyoo kwenye mishipa ya limfu
- Mnyoo wa kike unaanza kuzaa mabuu wengienwanaoitwa microfilariae ambao wanaogelea kwenda kwenye mfumo wa damu
- Mbu anaponyonya damu, anabeba na mabuu hawa wanaitwa microfilariae
- Microfilariae wanajiva gamba kuwa buu anayeitwa larvae tayari kwa kuambukiza
- Larvae anasafiri kwenda kwenye sehemu za mdomo tayari kuambukiza
Dalili
Uwepo wa minyoo kwenye mfumo wa limfu unaonekana kama kitu kigeni na mwili unajaribu kupandana nao na hivyo kuasababisha muitikio mbaya na kuvimba. Na baada ya minyoo kufa, protini kadhaa zinatolewa ambazo pia zinazongeza tatizo. Kuna hatua 3 za ugonjwa huu wa matende.
- Kipindi cha awali
- Huanza miezi michache baada ya maambukizi
- Kuvimba tezi za mwili
- Homa
- Kwa kipindi hiki mabuu aina ya microfilariae yanakuwa hayaonekani kwenye damu kwa sababu minyoo inakuwa haijakomaa. Dalili za wakati huu zinatokana na mwili kupambana na mnyoo kwa sababu ni kitu kigeni/mvamizi
- Hatua ya kati
- Hii inaanza mwaka mmoja baada ya hatua ya mwanzo. katika hatua hii minyoo inakuwa imekua na imeanza kutotoa microfilariae kwenda kwenye damu
- Kwa sababu kinga ya mwili unajaribu kuwaua minyoo inasababisha homa na kuvimba kwa mfumo wa limfu, korodani na mapumbu. Kama hali hii ya muitikio mbaya itanedelea mwishowe mgonjwa anapata mabusha.
- Hatua ya mwisho
- Baada ya miaka mingi ya miitikio mbaya kuwepo kwa minyoo, tezi na mishipa ya limfu inaziba na kusababisha maji kuanza kujaa mwilini. Kujaa kwa maji kunashuhudiwa zaidi kwenye miguu na pumbu, lakini pia unaweza kuonekana kwenye uke, matiti na mikono
- Kwa sababu kwa wakati huu unakuta minyoo wakubwa unakuta wameshakufa, microfilariae pia hautawaona.
Utambuzi
- Dalili na epidemiolojia
- Kuna dalili zinazoonesha kuziba kwa mishipa ya limfu na historia ya kusafiri kwenda maeneo yenye ugonjwa huu
- Kwa kuangalia mabuu (microfilarie) kwenye damu ya mgonjwa wa darubini
- Ukitaka kuchukua damu kwa ajili ya kipimo inabidi ujue kuwa katika maeneo mengi ya dunia microfilariae wanajitokeza kwenye damu wakati wa usiku pekee (nocturnal) na kisha mchana hujificha wasionekane, isipokuwa kwa wale wanaoishi kwenye maeneo ya kusini mwa pasifiki (diurnal)
Matibabu
- Diethyl carbamazin Citrate (DEC) inaweza kuondoa haraka mabuu (microfilariae) kutoka kwenye damu lakini inaweza kushindwa kuua minyoo wakubwa. kwa sababu hii, utapaswa kurudia kutumia dawa hii ya DEC kila mwakwa kwa miaka kadhaa.
- Upasuaji kwa mgonjwa mwenye mabusha
Kuzuia
- Dhibiti mbu
- Toa tiba kinga kwa watu wanaoishi maeneo hatarishi
- Jikingine binafsi na mbu