Ugonjwa wa ndui ni nini?

Ugonjwa wa ndui (smallpox) ni ugonjwa hatari, unaasambaa haraka sana na wakati mwingine unaweza kusababisha vifo. Ndui inasababishwa na virusi wanaitwa variola. Milipuko ya ugonjwa huu ilitokea mara kwa mara kwa miaka elfu, lakini ugonjwa huu ulitokomezwa kabisa duniani kwa sababu ya kampeni za chanjo. Watu waliougua ndui walipatwa na homa na mapele makubwa. Japo watu wengi waliougua ugonjwa huu walipona, watu watatu kati ya kumi waliougua walikufa.

Nani anapata ugonjwa wa ndui

Kisa cha mwisho cha ugonjwa wa ndui kilitokea mwaka 1949 nchini Marekani. Kisa cha mwisho kilichotokea kwa asili kilikuwa huko nchini Somalia mwaka 1977. Mpango wa chanjo iliyotolewa kwa watu wote duniani iliwezesha kutokomeza kabisa virusi hivi. Isipokuwa mabaki ya virusi yaliyobakizwa katika maabara kadhaa duniani kwa ajili ya matumizi ya kiutafiti. Kwa sababu ya hofu iliyopo ya virusi hivi kutumiwa kama silaha, hata kisa kimoja tu cha ugonjwa huu, kinaweza kuzua kadhia kubwa duniani.

Ugonjwa wa ndui unasambazwaje?

Virusi vya variola vinasambaa kutoka kwa mtu mmoja mpaka mwingine kwa kugusa maji maji yanayoruka hewani baada ya kukohoa au kupiga chafya, majimaji ya mwili au vidonda kwenye ngozi ya mtu aliyeambukizwa. Unaweza pia kuambukizwa kwa kugusa nguo au matandiko yaliyotumiwa na mgonjwa. Virusi vya variola havisambazwi na wanyama au wadudu. Mtu mwenye ndui anaweza kuambukiza wengine punde tu  dalili ya mwanzo za upele zinapoonekana (vidoti vyekundu kwenye ulimi na mdomo). Mgonjwa wa ndui anaweza kuambukiza wengine mpaka upele utakapopasuka na kukauka kabisa.

Ni zipi dalili za ugonjwa huu?Ugonjwa wa ndui

Dalili za mwanzo ni pamoja na homa kali, uchovu, kujisikia vibaya, maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili na wakati mwingine kutapika. Dalili zinapoanza, mtu huwa mgonjwa sana, na hawezi kuendelea na kazi zake za kila siku.

Siku 2 mpaka 4 baada ya dalili kuanza, upele huanza kutokea. Upele unapoanza kutokea, homa inapungua na mtu anaanza kujisikia vizuri angalau. Huu upele unaanzia kwenye ulimi na ndani ya mdomo, unasambaa kwenye uso, mikono na miguu (hii ni pamoja na viganja vya mikono na nyayo za miguu, na baadae mwili mzima ndani ya masaa 24.

Upele mwanzoni unaonekana kama viuvimbe vidogo au malengelenge yaliyo jaaa ndani majimaji mazito na huwa na mdumbukio mdogo katikati. Ndani ya siku 5 mpaka 10 malengelenge yanakua makubwa, mviringo, magumu na yaliyojaa usaha. Katika wiki 2, majipu yanapasuka na kukauka. Ndani ya wiki ya 3 ya upele, upele uliopasuka una kauka na kuacha kovu.

Dalili zinaanza baada ya muda gani baada ya kuambukizwa?

Dalili zinaweza kutokea siku 7 – 19 baada ya kuambukizwa, lakini kwa kawaida inachukua siku 10 – 14 baada ya kuambukizwa.

Ugonjwa huu unatambuliwaje?

Ndui inatambuliwa kwa kuangalia dalili na ishara. Ugonjwa unaweza pia kutambuliwa kwa uhakika kwa kupeleka sampuli ya damu au tishu maabara. Utambuzi wa ndui unafanyika katika maabara maalumu, zenye vifaa na ulinzi wa kutosha kuwalinda wafanyakazi na mazingira.

Ni yapi matibabu ya ugonjwa wa ndui?

Ugonjwa wa huu unatibiwa kwa kutumia dawa za kudhibiti virusi (antivirals) na dawa nyingine za kutegemeza mwili kadri unavyozihitaji. Hakuna matibabu ya moja kwa moja yenye ufanisi mzuri kutibu ugonjwa huu, lakini dawa za kudhibiti virusi zinaweza kutibu/kuzuia ugonjwa kuwa mbaya zaidi.

Ugonjwa wa ndui unaweza kuzuiwa vipi?

Kupata chanjo ndani ya siku tatu baada ya kuambukiwa kunaweza kuzuia au kupunguza ukali wa ugonjwa wa ndui kwa watu wengi. Ukipewa chanjo ndani ya siku 4 mpaka 7 baada ya kuambukizwa inaweza kuwalinda baadhi ya watu na hata kupunguza athari zake. Kupata chanjo hakuwezi kukukinga na athari za ugonjwa wa ndui kama tayari umeanza kupata upele. Kwa sasa chanjo hii haipatikani kwa ajili ya matumizi ya umma.

Je, ugonjwa wa ndui unaweza kutumiwa kama silaha- ugaidi

Japo sio jambo linalotarajiwa kutokea, kuna uwezekano kuwa virusi vya variola vinaweza kusababisha ugonjwa wa ndui kama vikitumika kama silaha ya ugaidi. Mwaka 1980, wataalamu walitangaza kuwa ugonjwa wa ndui umetokomezwa kabisa duniani. Lakini ukweli ni kwamba, kuna maabara 2 duniani zinazohifadhi virusi hawa, moja iko nchini Marekani na moja nchini Urusi. Zinatunzwa huko, kwa matumizi ya kiutafiti pekee.

Vyanzo

https://www.cdc.gov/smallpox/index.html

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *