Ugonjwa wa sonona (huzuni) baada ya kujifungua ni nini?
Ugonjwa wa sonona (huzuni) baada ya kujifungua ni aina ya sonona kali inayotokea baada ya kujifungua. Karibu wanawake wanne kati ya watano wanaojifungua wanapata mabadiliko ya kihisia ndani ya siku 10 za mwanzo baada ya kujifungua. Kama dalili hizi ni kali sana na zinadumu zaidi ya siku 10, tunasema kuwa mama huyo ana ugonjwa wa sonona (huzuni) baada ya kujifungua.
Baadhi ya wanawake wanaanza kujisikia vizuri baada ya wiki kadhaa. Baadhi wanaendelea kujisikia wenye huzuni kwa miezi kadhaa. Wanawake wenye dalili kali zaidi au ambao waliwahi kupatwa na ugonjwa wa sonona wanaweza kuchukua muda mrefu zaidi kujisikia vizuri.
Ni zipi dalili za ugonjwa sonona (huzuni) baada ya kujifungua?
Dalili zinaweza kujumuisha kujisikia mwenye huzuni, mwoga na kulialia. Baadhi ya wanawake wanakuwa na wasiwasi uliozidi kuhusu mtoto wao, au wanaogopa sana kufanya makosa yoyote wanapokuwa wakimuhudumia mtoto. Wanaweza pia kupata shida kulala au kuona ugumu kuwa makini wanapofanya kitu fulani. Baadhi ya wanawake wanaweza kupoteza hamu ya kufanya mambo waliyokuwa wanayapenda.
Ni hali ya kawaida kuwa na wasiwasi kiasi baada ya kujifungua. Lakini, kama wasiwasi au woga huo unakufanya ushindwe kujihudumia au kuhuduma familia yako, kuna tatizo.
Baadhi ya wanawake wenye ugonjwa wa sonona (huzuni) baada ya kujifungua wanakuwa na mawazo kichwani ya kutaka kumuumiza au kumuua mtoto. Aina hii ya mawazo inaweza kukukera na hata kukuogofya, lakini haimaanishi kuwa wanawake hawa wanaweza kweli kumuumiza mtoto. Hii ni dalili ya kawaida inayowapata wanawake wengi wenye ugonjwa wa sonona (huzuni) baada ya kujifungua na yataisha baada ya kupata matibabu. Ongea na daktari kama unaona dalili hizi.
Baadhi ya wanawake wenye aina kali ya ugonjwa wa sonona (huzuni) baada ya kujifungua wanaweza kujihisi kama hawana sababu ya kuendelea kuishi na kwamba maisha yao hayana thamani kabisa, au wanaweza kujihisi kuwa mtoto au wanafamilia wataishi maisha bora zaidi kama yeye ataondoka/kufa. Ongea na daktari haraka sana kama una mawazo haya.
Ni nini kinasababisha ugonjwa sonona (huzuni) baada ya kujifungua?
Sababu za tatizo hili hazijulikani vizuri bado. Baadhi ya wanawake wanaitikia zaidi mabadiliko ya homoni yanayosababisha mabadiliko makubwa kwenye miili yao baada ya kujifungua, na hii inaweza kusababisha sonona. Kujisikia huzuni haimaanishi kuwa wewe ni mtu mbaya.
Nani anapata ugonjwa sonona (huzuni) baada ya kujifungua?
Mwanamke yoyote anaweza kupata tatizo hili, lakini baadhi ya mambo yanaweza kuongeza uwezekano / hatari ya kuupata. Hizi ni pamoja na:
- Kama umewahi kuwa na ugonjwa wa sonona, hasa wakati wa ujauzito au baada ya kujifungua
- Baada ya matatizo ya mahusiano
- Wanafamilia au marafiki wachache wa kuongea nao
- Matatizo mengine yanayoongeza msongo kwenye kipindi cha ujauzito au baada ya kujifungua
Tatizo la sonona (huzuni) baada ya kujifungua linatibiwa vipi?
Daktari anaweza kukuandikia dawa za kudhibiti msongo (anti-depressants). Anaweza pia kupendekeza uongee na daktari wa tiba maongezi au ujiunge kwenye kikundi cha kutegemezana cha kina mama wenye tatizo kama lako.
Je, ninaweza kutumia dawa za kudhibiti ugonjwa wa sonona (huzuni) baada ya kujifungua nikiwa nanyonyesha?
Ndiyo. Kiwango cha dawa kinachoingia kwenye maziwa ni kidogo sana na sio rahisi kumdhuru mwanao. Kutokutibu ugonjwa wako, ni hatari zaidi kwa mwanao. Kama usipotibiwa ugonjwa wa sonona (huzuni) baada ya kujifungua itasababisha uwe na uhusiano mbaya na mtoto wako, itasababisha asikue impasavyo, na itaongeza uwezekano wa mtoto kuwa na sonona atakapokuwa mtu mzima.
Nifanye nini kingine ili kujihisi vizuri?
Unapaswa kukumbuka kuwa wanawake wengi wanapata hisia na mawazo haya unayopata. Ongea na daktari ili akusadie kupanga mpango na mambo unayoweza kufanya ili kujisikia vizuri.