Maelezo ya jumla
UKIMWI – Upungufu wa kinga mwilini- ni ugonjwa unaopata mtu baada virusi vya VVU kuharibu mfumo wa kinga yako ya mwili. Kwa kawaida, mfumo wako wa kinga husaidia kupambana na magonjwa. Mfumo wako wa kinga unaposhindwa kufanya kazi yake vyema unaweza kuugua sana na hata kufa. VVU – Virusi vya Ukimwi – ni virusi vinavyoua “seli za mwili zinazoitwa CD4 “. Seli za CD4 ambazo pia huitwa T-helper seli, husaidia mwili wako kupambana na magonjwa. UKIMWI ni ugonjwa unaotokana na kuharibiwa kwa seli za T-helper. VVU husababisha UKIMWI.
Je, nini dalili za UKIMWI?
Dalili za UKIMWI ni matokeo ya maambukizi ambayo kwa kawaida hayawapati watu wenye kinga imara ya mwili. Aina hii ya magonjwa yanayowapata watu wenye kinga dhaifu ya mwili huitwa magonjwa nyemelezi. Mfumo wa kinga wa watu wenye UKIMWI umedhoofishwa sana na VVU na wako kwenye hatari ya kushambuliwa na magonjwa nyemelezi. Watu wengine wenye maambukizi ya VVU hubakia bila dalili yoyote kwa miaka mingi. Mwanzoni baada tu ya mtu kuambukiwa VVU (wiki 2 baada) anaweza kupata dalili kama za mafua.
- Homa
- Kutokwa jasho (hasa usiku),
- Kuvimba kwa tezi, kuhisi baridi, uchovu
- Kupungua uzito
- Maumivu kwenye koo
- Kuhara
- Vidonda mdomoni, hii ni pamoja na fangasi a mdomoni.
UKIMWI husababishwa na nini?
Mtu yeyote anaweza kupata VVU. Ni jambo la muhimu sana kujua ni kwa jinsi gani unaweza kupata virusi.
Unaweza kupata VVU:
- Kwa kufanya ngono isiyo salama – kujamiiana bila kondomu – na mtu mwenye VVU. Virusi vinaweza kuwa kwenye damu, shahawa, au majimaji ya uke ya mtu aliyeambukizwa na vinaweza kuingia mwili mwako kupitia kwenye kidonda ukeni, kwenye uume, mkunduni au mdomoni.
- Kwa kuchangia sindano au kuchangia vifaa vinavyotumika kuandaa madawa ya kulevya na mtu aliye na VVU.
- Kwa kuongezewa damu yenye maambukizi ya VVU (Lakini si rahisi siku hizi kuambukizwa kwa njia hii kwa sababu damu hupimwa kabla ya mtu kuongezewa)
- Watoto waliozaliwa na wanawake wenye VVU wanaweza kuambukizwa wakati wa ujauzito, kuzaliwa, au kunyonyesha.
Huwezi kupata VVU:
- Kwa kufanya kazi au kuwa karibu na mtu mwenye VVU.
- Kutoka kwenye jasho, mate, machozi, nguo, simu, viti vya choo, au vitu vya kila siku kama kuchangia chakula.
- Kwa kuumwa na wadudu
- Kwa kutoa damu.
- Kwa busu la kinywa hasa kikiwa kimefungwa (lakini kuna nafasi ndogo sana ya kupata virusi kutokana na busu la mdomo ukiwa wazi- French kiss – Kula denda).
Nani yuko kwenye hatari zaidi ya kupata UKIMWI?
- Watu ambao hufanya ngono isiyo salama (bila kinga), watu wenye uraibu wa madawa ya kulevya.
- Wapenzi wa watu wenye tabia zinazoongeza hatari ya maambukizi, mf; watu wanaofanya ngono kinyume na maumbile, wanaochangia sindano wakati wa kuchoma madawa ya kulevya.
- Watoto waliozaliwa na kina mama wenye VVU wako kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu
Utambuzi wa UKIMWI
Unaweza kuwa na VVU na bado ukajihisi una afya nzuri. Njia pekee ya kujua kwa uhakika kama umeambukizwa au la ni kupimwa. Ongea na mtoa huduma ya afya au mshauri wa afya kabla na baada ya kupimwa. Unaweza kwenda kwa daktari wako au idara yoyote ya afya kwa ajili ya kupima. Daktari wako au mtoa huduma ya afya atakupima na majibu ya kipimo chako yatabaki kuwa siri baina yenu kama ilivyo kwa taarifa zako zingine za kitabibu. Hii inamaanisha taarifa hizo zinaweza kuonwa na watu wenye mamlaka ya kuziona pekee na si vinginevyo. Unaweza kumuuliza daktari wako, mtoa huduma ya afya, au mshauri wa VVU wa mahali unapopimwa, ni nani anayeweza kuziona taarifa zako. Kwa mfano, unaweza kuuliza kama kampuni yako ya bima inaruhusiwa kujua hali yako ya VVU kama unadai madai ya bima ya afya au kuomba bima ya maisha au bima ya ulemavu. Shirika la afya duniani linashauri kila mtu kujua hali yake. Ni kwa mara ngapi unapaswa kupimwa hutegemea mazingira yako. Ikiwa haujawahi kupimwa VVU, unapaswa kupimwa. Ikiwa una tabia zinazoongeza hatari ya kupata VVU, basi unapaswa kupimwa mara kwa mara.
Wakati gani utafute matibabu ya haraka?
Kwa kuwa VVU hudhoofisha mfumo wa kinga, watu wenye UKIMWI wanapaswa kumwona daktari na kupimwa ikiwa wanaamini wameambukizwa. Kama umegunduliwa kuwa umeambukizwa unapaswa kuwasiliana na daktari wako mara kwa mara. Watu wenye UKIMWI, wako kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi, kansa na magonjwa mengine nyemelezi ambayo kwa kawaida hayawezi kuwapata watu wenye kinga thabiti ya mwili. Kwa hiyo wanapaswa kuwa makini na kutoa taarifa ya ugonjwa wowote mpya kwa daktari pindi unapojitokeza.
Uchaguzi wa matibabu ya UKIMWI
Hakuna tiba ya VVU. Ni hali utakayoishi nayo maisha yako yote. Japo kuambukizwa VVU ni jambo la kuogofya, siku hizi watu wengi wenye VVU na UKIMWI huishi miaka mingi ya afya kwa sababu ya matibabu ya kudhibiti virusi yenye ufanisi mkubwa. Ni muhimu sana kuhakikisha unaonana na daktari ili kuanza tiba ya VVU. Kama una ujauzito au unapanga kubeba mimba, ni muhimu sana kuongea na mtaalamu. Kuna mambo kadhaa unayopaswa kuyafanya wewe mwenyewe ili kudumisha afya njema. Yafuatayo ni chache lakini muhimu:
- Fuata maelekezo ya daktari. Fika hosipitalini kila unapohitajika. Daktari anaweza kuagiza utumie dawa. Tumia dawa kama ulivyoagizwa, ukiacha kutumia dawa unatoa nafasi ya virusi vya VVU kuongezeka.
- Kama unavuta sigara au kutumia madawa yoyote ambayo haujaagizwa na daktari, ACHA.
- Kula mlo wenye afya. Hii itasaidia kuupa nguvu mwili, kuongeza uzito wako, na kusaidia mwili kupambana na magonjwa.
- Fanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuuimarisha mwili
- Pata usingizi na mapumziko ya kutosha.
Kuzuia UKIMWI
- Usichangie sindano wakati wa kuchoma madawa ya kulevya, vitamini, au hata wakati wa kuweka tatoo au kutoga masikio. Pia, usichangie vifaa vinavyotumika kutayarisha madawa ya kulevya kabla ya kujichoma. Watu wengi wameambukizwa VVU, homa ya ini (hepatitis), na vijidudu wengine kwa njia hii.
- Njia ya uhakika ya kuepuka maambukizi ya magonjwa ya zinaa ni kujiepusha na ngono, au kuwa na uhusiano wa muda mrefu na mwenzi mmoja mwaminifu ambaye amepimwa na ambaye anafanya ngono salama kama vile kutumia kondomu.
- Kwa watu ambao tabia za ngono zinawaweka katika hatari ya kupata VVU, matumizi sahihi na thabiti ya kondomu za kiume yanaweza kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa. Hata hivyo, hakuna njia ya kinga ambayo hutoa kinga asilimia 100, na matumizi ya kondomu hayawezi kuhakikisha ulinzi kamili dhidi ya magonjwa ya zinaa na UKIMWI. Kadri unavyokuwa na washirika wengi wa ngono ndivyo hatari ya kuambukizwa inavyoongezeka.
- Kondomu lazima zitumimiwe kwa usahihi kila mara tendo la ngono linapofanyika ili kuwa na ufanisi na kinga. Matumizi yasiyofaa yanaweza kusababisha kondomu kuteleza au kupasuka, na hivyo kupunguza uwezo wa kukukinga. Matumizi yasiyofaa, k.m., kushindwa kutumia kondomu kwa kila tendo la ngono, inaweza kusababisha uambukizo wa magonjwa ya zinaa kwa sababu maambukizi yanaweza kutokea kwa kitendo kimoja cha ngono.
- Usichangie nyembe au mswaki, kwa sababu zinaweza kuwa na damu ya mtu mwingine.
- Kama una ujauzito au unadhani unaweza kubeba mimba hivi karibuni, wasiliana na daktari au idara yoyote ya afya katika eneo lako ili kupima VVU. Kama umeambukizwa VVU, matibabu yapo yatakayopunguza uwezekano wa kumwambukiza mtoto wako VVU.
Nini cha kutarajia?
- Kwa sasa, hakuna tiba ya UKIMWI. Daima UKIMWI husababisha kifo kama matibabu hayatatolewa. Wagonjwa wengi wanaishi miaka mingi baada ya utambuzi kwa sababu ya upatikanaji wa madawa ya kupunguza makali ya VVU (ARV=Antretroviral). ARV na madawa mengine kama hayo yameongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya watu ambao wanaishi kwa muda mrefu na VVU.
Utafiti unaendelea katika kutafuta tiba, madawa na chanjo ya UKIMWI. Kwa bahati mbaya, dawa za VVU si mara zote zinazopatikana katika nchi zinazoendelea.
Matatizo yanayoweza kutokea
Wagonjwa wa UKIMWI huwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi, kansa na matatizo ya mfumo wa neva- Maambukizi kama-
- Kifua kikuu (TB)
- Ugonjwa wa kuhara unasababishwa na salmonela (Salmonellosis)
- Cytomegalovirus (CMV)– virusi hivi huharibu mfumo wa neva kwa watu wenye upungufu wa kinga
- Cryptococcal meningitis– Fangasi aina ya cryptococcal husababisha kuvimba kwa utando unaofunika ubongo na uti wa mgongo, hali hii ni hatari na inaweza kutishia maisha
- Ugonjwa wa toxoplasmosis– Vimelea wa ugonjwa huu huenezwa kwa kula nyama isiyoiva vyema au kwa kula kinyesi cha paka, vimelea hawa hushambulia ubongo na wanaweza kusababisha kifo kama matibabu hayatafanyika mapema- mara nyingi watu wenye kinga thabiti ya mwili hawapati ugonjwa huu
- Cryptosporidiosis- Huu ni ugonjwa unaosababishwa na kimelea anayeitwa cryptosporidium, kimelea huyu husababisha mtu mwenye UKIMWI kuhara sana
Saratani kama-
- Sarcoma ya Kaposi
- Lymphomas
Matatizo mengine-
- Kupungua kwa uzito
- Matatizo ya mfumo wa neva kama vile kuchanganyikiwa, kusahausahau, sonona, wasiwasi mwingi na matatizo ya kutembea
MAELEZO YA ZIADA KUHUSU UKIMWI
Maelezo ya jumla
Ugonjwa mbaya unaotishia maisha uliotambuliwa mara ya kwanza mkoani Kagera mwaka 1983. Ugonjwa wa UKIMWI inatokana na kuwa na maambukizi ya muda mrefu ya VVU, ambao mara nyingi kadri muda unavyoenda yanasababisha uharibifu wa mfumo wa kinga ya mwili na viungo vya mwili, pamoja mfumo wa fahamu.
Sababu
Virusi vya ukimwi (VVU) (VV-1 na VVU-2)
Epidemiolojia
Ugonjwa huu ni janga la dunia nzima. VVU-1 ni maambukzi yaliyosambaa dunia nzima, lani yanapatikana zaidi Afrika kusini mwa jangwa la sahara, Amerika, Kusini mwa ulaya na kusini-mashariki mwa bara Asia. VVU-2 inapatikana zaidi Afrika magharibi.
Ripoti ya wizara ya afya 2020 imeandika baadhi ya mambo yafuatao kuhusu hali ya VVU/UKIMWI Tanzania
- Kiwango cha maambukizi ya VVU kama nchi kwa ujumla inakadiriwa kuwa ni 4.6 %
- Kiwango cha maambukizi mapya 58,000 kila mwaka (15 -49)
- Kiwango cha maambukizi mapya kwa watoto chini miaka 15 ni 6,500
- Karibia 50% ya maambukizi yote mapya yanawapata vijana umri wa 15-29
Takwimu hizi zinaogopesha kwa sababu “ni maambukizi mapya”. Kati ya magonjwa 10 yanayosababisha ulemavu na vifo vingi nchini, UKIMWI ni ya nne.
Uambukizo
Kuna njia kadhaa
- Ngono ni njia kuu na kukutana na damu au tishu za mwili zenye maambukizi
- Kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
Muda kabla dalili kuanza
Hii inategemea. Japo muda kuanzia wakati wa kuambukizwa mpka wakati ambao mtu atakuwa ametengeneza kinga zinazoweza kusababisha kujua kuwa mtu ana UKIMWI ni miezi 1-3, muda unaochukua maambukizi ya VVU kuanza kuonesha dalili za UKIMWI inachukua muda kati ya mwaka 1 mpaka 10 au zaidi. Karibia nusu ya watu wote wenye maambukizi watakuwa wamepata UKIMWI ndani ya miaka 10.
Muda wa uambukizi
Haifahamiki vyema. Ila inadhaniwa kuwa mtu aliyeambukizwa anaweza kuambukiza wengine muda mfupi baada ya maambukizi na maisha yake yote
Nani yuko kwenye hatari
Watu wote wako kwenye hatari. Hatari ya kuambukizwa inaongezeka zaidi kama una magonjwa mengine ya ngono, hasa yanayosababisha vidonda.
Dalili
Dalili za ugonjwa wa UKIMWI zimegawanyika katika makundi mawili
- Dalili za awali
-
- Zinatokea wiki 3-6 baada ya maambukizi
- Dalili hizi ni: homa, maumivu ya koo, kuvimba mtoki, maumivu ya kichwa, maumivu nyuma ya jicho, maumivu ya viungo, maumivu ya misuli, uchovu, kichefuchefu, kupungua uzito, kutapika na kuhara
- Kuvimba kwa utando unaofunika ubongo na uti wa mgono (meningitis), kuvimba kwa ubongo, matatizo ya mishipa ya fahamu, matatizo ya misuli, upele mwekundu, vidonda mdomoni/ukeni/ndani ya pua n.k.
- Dalili zinazotokea baadae
-
- Hizi zinatokea kwa sababya magonjwa nyemelezi kama zile nimonia (hasa inayosababishwa na fangasi aina ya pneumocystis carinii pneumonia), Kifua kikuu, kuvimba kwa utando unaofunika ubongo na uti wa mgongo (hasa husababishwa na fangasi cryptococcal)
Utambuzi
- Kwa kuangalia dalili, hasa katika hatua za baadae za ugonjwa
- Kwa kutumia vipimo vya damu, hasa katika hatua za awali za ugonjwa
Matibabu
- Tumia dawa za kupunguza makali ya VVU
- Tibu magonjwa nyemelezi
- Tumia dawa za kupunguza makali ili kupunguza uwezekano wa kumwambukiza mtoto aliyetumboni mwa mama
Kuzuia
- Acha kushiriki ngono
- Kuwa mwaminifu kwa mwenzi mliyekwisha pima na kukuta mko salama
- Tumia kondomu kwa usahihi
- Tambua visa na toa matibabu mapema iwezekanavyo