Maelezo ya jumla
Ukomo wa hedhi (menopause) ni mabadiliko ya asili ya mwili yanayowatokea wanawake wenye umri kati ya miaka 45 mpaka 55, kwa sababu ya kupungua kwa kiwango cha homoni ya kike ‘’estrojeni’’. Mwanzoni, damu ya hedhi inaanza kuwa nyepesi, baadae inaanza kukosekana kabisa kwa baadhi ya miezi na hatimae inakoma kabisa kutoka. Mwanamke husemekana kuwa amefikia ukomo wa hedhi kama hajapata hedhi kwa angalau mwaka mmoja. Baadhi ya wanawake hawapati dalili zozote, lakini kuna wengine wanapata matatizo mbalimbali kwa sababu ya ukomo wa hedhi, hii ni pamoja na kupatwa na vipindi vya joto la mwili kupanda ghafla, kuvuja jasho jingi sana usiku na ukavu wa uke.
Kama una matatizo wakati wa ukomo wa hedhi mwone daktari kama
Ni vizuri kupanga kumwona daktari kama hauna uhakika kuwa dalili unazozipata zinatokana na ukomo wa hedhi, au kama unaona ni vyema kuanza kutumia tiba ya kuongeza homoni mwilini.
Unachoweza kufanya wewe mwenyewe wakati wa ukomo wa hedhi
Kuna mambo kadhaa unayoweza kufanya ili kudhibiti dalili zinazosababishwa na ukomo wa hedhi
- Kama unapatwa na matukio ya joto la mwili kupanda ghafla ‘’hot flushes’’, vaa nguo nyepesi ndani, ili iwe rahisi kuvua nguo nzito ya juu utakapoanza kuhisi joto. Lala kwenye chumba chenye joto la kawaida na shuka jepesi. Oga maji ya uvuguvugu. Epuka kula vyakula vya moto na vyakula vyenye pilipili, na punguza kiwango cha kahawa, chai na pombe.
- Kama unaona uke unakauka sana na unahisi maumivu wakati wa ngono, jaribu kutumia kilainishi ‘’lubricating jelly’’. Kilainishi kitasaidia kupunguza karaha wakati wa ngono. Unaweza kuweka kilainishi ukeni muda mfupi tu kabla ya ngono.
- Unaweza kujaribu kuongeza bidhaa za soya kwenye mlo. Soya ina ‘’phytoestogen’’ ambayo ni kemikali ya asili inayopatikana kwenye mimea aina ya soya, kemikali hii inafanya kazi sawa na estrojeni mwilini. Ukila vyakula vyenye soya inaweza kusaidia kupunguza ‘’hot flushes’’.
- Kunywa maji ya kutosha, angalau glass 6-8 kwa siku
- Kama unajihisi misuli imekaza, jaribu kutumia mbinu za kulegeza misuli ‘’muscle relaxing thechnique’’. BONYEZA HAPA KUJIFUZA MBINU ZA KULEGEZA MISULI
- Fanya mazoezi ya kuimarisha misuli, kama vile kubeba vitu vizito na kupunguza msongo. Ni sawa pia kutembea taratibu kwa angalau dakika 20 -30 kwa siku 5 za wiki.
- Epuka kuvuta sigara– kuvuta sigara kunasababisha dalili kuwa mbaya zaidi na kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo na kiharusi
Wakati wa ukomo wa hedhi mwone daktari kama
Panga kumwona daktari kama:
- Mbinu za kujisaidia mwenyewe nyumbani hazisaidii
- Ukiona dalili mpya, kwa mfano kuvuja damu ukeni tena, hasa kama umekuwa haupati hedhi kwa angalau mwaka mmoja