Je, una wasiwasi kuwa una ujauzito?
Kwa kweli njia pekee kujua kama wewe ni mjamzito ni kupima ujauzito. Hata hivyo, zipo dalili za awali za ujauzito zinazoweza kukujulisha kuwa yawezekana ukawa mjauzito.
Je, wote wanapata dalili za awali za ujauzito za kufanana?
Ukweli ni kwamba wanawake hawapati dalili za kufanana, kila mwanamke yuko tofauti. Vivyo hivyo ndivyo zilivyo dalili za ujauzito. Pia ikumbukwe kwamba hata kwa mwanamke huyo huyo aliyewahi kuwa mjamzito, dalili za kila ujauzito zinaweza zisifanane.
Tahadhari nyingine muhimu ni kuwa inawezekana kabisa dalili za awali za ujauzito zikashabihiana na dalili za kuingia au ukiwa kwenye hedhi, hivyo unaweza usitambue kwa urahisi kwamba umepata ujauzito.
Kumbuka dalili hizi pia zinaweza kusababishwa na sababu zingine ambazo hazitokani na ujauzito. Hivyo kuona tu dalili hizi haimaanishi kwamba wewe ni mjamzito, njia pekee ya wewe kujua kwa uhakika ni kupitia kipimo cha ujauzito.
Zifuatazo ni dalili za awali za ujauzito
Maumivu ya tumbo na kutokwa matone ya damu
Baada ya upevushaji wa yai, yai lililorutubishwa hujipandikiza kwenye mji wa mimba. Hii inaweza kusababisha dalili za awali za ujauzito ambazo ni kama kutokwa na matone ya damu na wakati mwingine maumivu ya tumbo la chini ya kitovu.
Matone hutokana na kujipandikiza kwa yai lililorutubishwa kwenye mji wa mimba. Hutokea wakati wowote ndani ya ya siku 12 baada ya yai kurutubishwa.
Maumivu ya tumbo la uzazi (chini ya kitovu), huwa yanashabihiana na maumivu ya hedhi, hivyo baadhi ya wanawake huyachukulia kama maumivu ya hedhi. Pamoja na kutokwa damu ukeni unaweza kuona ute mweupe mwepesi kama maziwa kutoka ukeni.
Ute huu huwa hauna madhara wa harufu na hauambatani na kuwasha. Pale unapokuwa na wasiwasi kuhusu ute huu unaweza kumwona daktari naye atakufanyia vipimo kuona kama una fangasi, bakteria au klamidia.
Mabadiliko katika matiti
Mababdiliko katika matiti ni dalili nyingine ya awali ya ujauzito. Kiwango cha vichocheo (homoni) huwa kinapanda kwa kasi baada ya upevushaji. Mabadiliko hayo yanaweza kufanya matiti kujaa, kuwa na vitu vinavyochoma choma. Unaweza kuhisi uzito kwenye matiti au matiti kuuma yanaposhikwa. Sehemu nyeusi ya chuchu huwa nyeusi zaidi.
Kuna sababu zingine zinazoweza kusababisha mabadiliko katika matiti. Ikiwa mabadiliko haya yanatokana na ujauzito basi kuwa na hakika kwamba itachukuwa muda kwa homoni kuzoeleka na zitakapozoeleka mwilini, maumivu yanapungua.
Uchovu
Uchovu wa kupindukia katika kipindi cha ujauzito ni jambo la kawaida na ambalo huwa linaanza mapema tu katika wiki za awali za ujauzito. Unaweza kujihisi mchovu mara tu baada ya kutungiwa mimba. Uchovu unatokana na kiwango kikubwa cha kichocheo cha ”progesterone” kinachokuwa kwenye damu wakati wa ujauzito.
Ifahamike kuwa uchovu pia unaweza kusababishwa na sababu zingine kama vile kushuka kwa shinikizo la damu, kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu au pia ongezeko kwenye uzalishaji wa damu. Kama uchovu wa kupindukia unatokana na ujauzito ni vema upange kupata mapumziko ya kutosha. Ulaji wa vyakula vyenye ukwasi mwingi wa protini na madini ya chuma unaweza kusaidia kuondoa au kupunguza tatizo hili.
Kichefuchefu.
Hii ni dalilil maarufu na iliyozoeleka ya ujauzito. Hata hivyo si kweli kwamba kila mjamzito hupata kichefuchefu. Kichefuchefu katika kipindi cha ujauzito kinaweza kutokea wakati wowote ule ila mara nyingi hutokea wakati wa asubuhi.
Mbona wajawazito huchagua sana chakula?
Ni kweli kabisa, baadhi ya wajawazito hupenda baadhi ya vyakula na huchukia vingine. Hii ni kwa sababu ya mabadiliko ya vichocheo mwilini. Hali hii ya kichefuchefu inaweza kuwa kubwa kiasi kwamba hata vyakula pendwa navyo havikai tumboni. Hali hii inaweza kuwa mbaya kwa baadhi ya wanawake kiasi cha kuhitjai huduma ya matibabu ya kulazwa hospitalini.
Mara nyingi kichefuchefu, kutamani baadhi ya vyakula au kuchukia baadhi ya vyakula kunaanza kupungua kuanzia wiki 13 ya ujauzito kwa wajawazito wengi. Hali hii kwa baadhi ya wajawazito inaweza kuendelea katika kipindi chote cha ujauzito. Katika kipindi hiki kumbuka kula lishe yenye uwiano mzuri ili wewe na mwanao muweze kupata virutubisho vinavyotakiwa. Unaweza kuwasiliana na daktari kwa ushauri zaidi kuhusu chakula unachohitajika kula.
Kukosa kuona siku za hedhi
Kutokuona hedhi ni dalili ya awali iliyozoeleka ya ujauzito. Tafiti zinaonesha kuwa hii moja ya sababu kuu zinazofanya wengi kukimbilia kupima ili kujua kama kweli ni wajwazito. Hata hivyo, fahamu kwamba kutokuona siku za hedhi au hedhi kuchelelwa siyo lazima itokane na kuwa una ujauzito. Kumbuka uwepo wa ujauzito unaweza kusababisha kutokwa na damu ukeni hivyo ni vizuri kumuuliza daktari kama kutokwa damu ni dalili ya hatari na ni kwa kawaida.
Jua kwamba zipo sababu zingine tofauti na ujauzito zinazoweza kuchangia kutokuona hedhi. Baadhi ya sababu hizi ni kuwa na ongezeko kubwa la uzito wa mwili, mabadiliko ya vichocheo (homoni), uchovu kupindukia, msongo, n.k. Baadhi ya wanawake wanakosa hedhi baada ya matumizi ya dawa za uzazi wa mpango. Kama umechelewa kuona siku na unahisi ni mjamzito pima ujauzito ili kuwa na uhakika.
Dalili nyingine za awali za ujauzito ni pamoja na:
Ujauzito huambatana na mabadiliko katika kiwango cha uwiano wa vichocheo katika mwili wa mama. Tofauti ya uwiano huu huweza pia kusababisha dalili za awali za ujauzito nyingine, mfano:
Kukojoa mara kwa mara
Hata hivyo ni vizuri kukumbuka kuwa kukojoa mara kwa mara kunaweza kusababishwa na maambukizi katika njia ya mkojo (UTI), kunaweza kusababishwa na ugonjwa wa kisukari na mara kadhaa kunaweza kusababishwa na matumizi ya dawa za diuretiki zinazotumika kushusha shinikizo la juu la damu.
Kufunga choo
kipindi cha ujauzito kiwango cha juu cha progesteroni kinawaweza kusababisha kufunga choo. Hii ni kwa sababu progesteroni husababisha chakula kupita taratibu tumboni. Unashauriwa kunywa kiasi kikubwa cha maji, kula vyakula vyenye utajiri wa nyuzinyuzi/ufumwele.
Kubadilika badilika kwa hisia
Hali hii ni kawaida katika miezi mitatu ya kwanza. Hali hii pia inachangiwa na mabadiliko ya vichocheo.
Maumivu ya kichwa na mgongo
Uwapo mjamzito unaweza kupatwa na maumivu kiasi ya kichwa na pengine unaweza kupata maumivu ya mgongo.
Kizunguzungu.
Kizunguzungu huchangiwa na kutanuka kwa mishipa ya damu kunakopelekea kushuka kwa shinikizo la damu. Hali hii pia inaweza kusababishwa na kushuka kwa kiwango cha sukari kwenye damu.
Kumbuka dalili za awali za ujauzito..
Uwapo Mjamzito unaweza usiwe na dalili hata moja ya zilizotajwa hapo juu. Vilevile unaweza ukawa na dalili zote hizo kwa pamoja. Pale ambapo dalili mojawapo au zote zinakuletea maudhi basi wasiliana na daktari kwa ufumbuzi.
Vyanzo
https://medlineplus.gov/ency/patientinstructions/000583.htm
Kuhusu Mwandishi
GEKURA MATARO, Clinician, Councellor, Mwanjelwa health Center
Jamani mimi naombeni msaada mimi seem y matiti kwenye chuchu kunauma san nikishika. Alafu Leo usiku nimekojoa kama mara sita kitu ambacho si kawaida mimi nimedhani n ujauzito lakini Jana nimepima hamna mimba. Je tatizo ni mini. Naombeni msaada tafadhali
Kwa kawaida matiti huuma ukikaribia hedhi yako, kama umekaribia siku za hedhi yako, haina shida, baada ya siku kupita utakuwa sawa. Ujuzito unaweza kusababisha matiti kuuma, hasa siku za awali. ili ujauzito kuonekana kwenye kipimo cha mkojo ni lazima uwe na angaau wiki 2. kama wiki 2 hazijapita subiri mpaka zipite ndio upime tena. Pima tena
Sawa mm nataka kuuliza swali nina girlfriend wangu anapata maumivu ya kichwa, kichefuchefu, na matone ya damu kutoka ukeni na tumbo kuuma ila nilijua mimba alipima na ikiwa hamna je tatizo nini
pole sana, zungumza nasi kupitia namba zetu kwa ushauri zaidi, tunahitaji maelezo zaidi
mjibu humu kwa manufaa ya wenginevpia, kwa maelezo zaidi ndo hakutafutee
Wakati mwingi, swali linaloulizwa hapa huwa halijitoshelezi kwa maelezo, baadhi ya maswali yanahitaji maelezo na majibu ya maswali mengine ndio daktari atambue sababu ni nini. Kama swali linawezekana kujibiwa katika chumba hiki, tutalijibu kwa ajili ya faida ya umma. kama sivyo tutakuelekeza kuonana na daktari wetu.